2016-05-02 07:08:00

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani na matumaini ya Kikristo!


Waamini wa Kanisa la Mashariki, Mei Mosi wanaadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana na Askofu mkuu Gennadios wa Kanisa la Kiorthodox nchini Italia na Malta, anawaalika Wakristo kusherehekea na kushangilia siku hii iliyofanywa na Bwana, yaani Fumbo la Pasaka ambalo ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu dunia mpya inayoambata wokovu ulioletwa na Kristo Yesu. Huu ndio mwanga unaowaangaza watakatifu na mashuhuda wa imani walioenea sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Gennadios anakaza kusema, Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo. Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya. Anasema, ahimidiwe Mungu wa Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi aliwazaa mara ya pili ili wapate tumaini lenye uzima, kwa kufufuka kwake Yesu Kristo kwa wafu wapate urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yao, kwani wao wanalindwa pia na nguvu ya Mungu, ili waweze kupata wokovu utakaofunuliwa nyakati za mwisho.

Kumbe, hii ni changamoto ya kuwa ni watu wapya ili kuishi katika dunia mpya kwani Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni kiini cha Imani ya Kikristo, mwaliko na changamoto kwa waamini kuambata utakatifu wa maisha, ili waweze kweli kumwona Mungu! Wawe na nyoyo safi na macho meupe, ili kushuhudia Ufufuko wa Kristo katika maisha yao, tayari kushikamana kwa pamoja ili kumwimbia Kristo Mfufuka wimbo wa utukufu kwa ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.