2016-04-30 07:56:00

Jubilei ya vikosi vya ulinzi na usalama!


Vikosi vya ulinzi na usalama vinaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu kwa kutafakari kwa kina na mapana vita na haki msingi za binadamu kwa kutambua kwamba, vita kimsingi haina macho! Mtutu wa bunduki unaporindima waathirika ni raia na askari, ambao wakati mwingine wanajikuta wakifanya mauaji ya kimbari. Familia za askari pia zinateseka wakati askari wakiwa mstari wa mbele kutekeleza dhamana na majukumu yao.

Makundi yote haya anasema Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la huruma, ili Kanisa liweze kuwasaidia waathirika katika ujumla wao. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Taasisi ya Kipapa ya Agostinianum, iliyoko mjini Roma, kuanzia tarehe 29 hadi Mei Mosi, 2016 inafanya kongamano la kimataifa linalowashirikisha Mapadre wa kiroho wanaohudumia vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho haya ni kumbu kumbu ya miaka 30 tangu kuchapishwa waraka wa kitume kuhusu “Maisha ya Kiroho kwa Wanajeshi” “Spirituali militum”.

Askofu mkuu Gallagher anasema Vatican na Kanisa katika ujumla wake, linapenda kwa namna ya pekee kabisa kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Kumbe, ni wajibu wa viongozi wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama kutambua haki msingi za binadamu na kuhakikisha kwamba, zinalindwa na wahusika wote hasa wakati wa kinzani, vita na mipasuko ya kijamii.

Viongozi hawa waendelee kuwasaidia wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na familia zao. Vatican kuanzia mwaka 2000 imekuwa mstari wa mbele kusaidia majiundo makini ya haki msingi za binadamu kimataifa kwa Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi pamoja na Mapadre wanaowahudumia wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia. Vatican pia imeridhia mikataba na itifaki kadhaa zinazotambua na kuheshimu haki msingi za binadamu. Lengo anasema Askofu mkuu Gallagher ni kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu hata wakati wa vita na mipasuko ya kijamii na pale inapowezekana kuzuia vita isitokee kabisa kwani madhara ya vita ni makubwa kwa wote, waliomo na wale wasiokuwemo!

Kwa upande wake, Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu amegusia kwa namna ya pekee utume maalum wa Maaskofu kwenye Majimbo ya Kijeshi unaopania kuendeleza shughuli za kichungaji kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na familia zao. Wanajeshi wana maisha na ratiba ambayo mara nyingi inawafanya wajikute nje ya familia zao!

Hawa ni watu ambao wanacheza na silaha kila siku, kumbe mbele yao kuna picha ya maisha na kifo daima! Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama hawana budi kusaidiwa kikamilifu ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa: uzalendo, umoja na udugu; nidhamu, sheria na kanuni za maisha; uhuru, maisha ya kiroho pamoja na kujihinisha. Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi wanawajibu wa kuwasindikiza wanajeshi katika utume wao kimataifa, kiasi hata cha kuweza kuyamimina maisha yao kwa ajili ya ndugu zao, changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuwa kweli ni shuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama wanakuwa kweli ni wasamaria wema wa amani duniani. Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba kweli wanajeshi wanakuwa ni Wakristo na wanajeshi kweli, daima wakijitahidi kushuhudia imani yao. Kwa upande wake, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini ya matumaini kwa vikosi vya ulinzi na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.