2016-04-29 09:49:00

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu Ulaya!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, Bikira na Mwalimu wa Kanisa inayoadhimishwa na Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Aprili, amezungumzia kuhusu ujumbe wa Mtakatifu Katarina wa Siena kwa Bara la Ulaya kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha kanuni maadili, utu na maisha ya kiroho, ili kukabilia na changamoto zinazoendelea kulikumba Bara la Ulaya kwa nyakati hizi.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linaendelea kusababisha changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Ulaya kwa wakati huu: kisiasa, kiuchumi na kimaadili, kiasi cha kufumbia macho mateso na mahangaiko ya watu wanaopoteza maisha yao kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Makanisa Kisiwani Lesvos imeonesha mshikamano na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Mtakatifu Katarina wa Siena katika maisha yake aliweza kushuhudia ujumbe wa upendo kwa Mungu na jirani; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wagonjwa; akabahatika kuanzisha Utawa wa tatu wa Mtakatifu Theresa na kuwa ni mfano bora wa kuigwa na wananchi wa kawaida! Ni mwamini aliyethubutu kujitosa kimasomaso kuwahudumia maskini: kiroho na kimwili, changamoto kwa walimwengu kushinda kishawishi na ukavu wa utandawazi usioguswa wala kujali mahangaiko ya jirani zao!

Watu waoneshe ujasiri wa kumwilisha amri ya upendo katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Ni kwa njia ya huruma na mapendo, Katarina akabahatika kuvikwa taji la utakaifu ndani ya Kanisa. Bara na Ulaya linahitaji kuchangamshwa na watu kama Katarina wa Siena kwani kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko linaonekana kuchoka, limekuwa tasa na kinajitafuta lenyewe! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kujenga Bara la Ulaya ambalo linajikita katika kukuza na kudumisha utakatifu, utu na heshima ya binadamu badala ya mwelekeo wa sasa unaojikita katika uchumi na masuala ya kisiasa!

Kardinali Baldisseri anasema, hata leo hii Mtakatifu Katarina na wa Siena anayo changamoto kubwa kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo: Umoja na mshikamano; unaojikita katika: imani, matumaini na mapendo! Mtakatifu Katarina aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 33 tu alitambua kwamba, Fumbo la kifo ilikuwa ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kuanza mchakato wa maisha mapya. Kardinali Baldisseri ameiweka familia ya Mungu Jimbo kuu la Siena chini ya usimamizi na tunza ya Mtakatifu Katarina katika furaha na matumaini yake; machungu na mahangaiko yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.