2016-04-29 15:06:00

Siku ya Wafanyakazi Duniani: Utu na heshima ya binadamu!


Mei Mosi ni Siku ya Wafanyakazi Duniani; siku ya mshikamano na wafanyakazi katika kusimamia na kuunga mkono haki, wajibu na dhamana ya wafanyakazi katika mchakato wa maendeleo endelevu! Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Kazi inapaswa kupewa hadhi yake inayofumbatwa katika ubinadamu. Hapa kuna haja ya kuwepo na ushirikiano wa dhati kati ya shule na fursa za ajira sanjari na uwiano bora wa maendeleo katika nchi! Pasiwepo eneo la Kaskazini ambako watu wameendelea sana na Kusini, ambako kuna watu wanateseka kwa umaskini, ukosefu wa ajira na vitendo vya kigaidi!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya Mei Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani. Ujumbe wa Maaskofu wa Italia unaongozwa na kauli mbiu “Kazi: uhuru na utu wa binadamu katika nyakati za myumbo wa uchumi na kijamii”. Ukosefu wa fursa za ajira nchini Italia unachangia kwa kiasi kikubwa athari katika maisha ya watu kwani unagusa: utu, haki na afya mambo ambayo baadaye hayapewi tena kipaumbele cha pekee.

Waathirika wakubwa wa ukosefu wa fursa za ajira ni vijana wa kizazi kipya pamoja na wanawake, changamoto kwa watunga sera, wachumi na wawekezaji kuwajibika barabara ili kupambana fika na ukosefu wa fursa za ajira! Hata wafanyakazi nao wanapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwani haki inakwenda sanjari na wajibu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kugundua kwa mara nyingine tena kwamba, kazi ni wito unaosaidia kujenga na kudumisha utu, heshima na maisha ya binadamu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakaza kusema, kazi inapaswa kuwa ni jukwaa la mahusiano bora kati ya watu na Muumba wao; kati ya watu na mazingira, ili kuweza kupata ukamilifu wa maisha ya mwanadamu. Daima kazi iwe ni kielelezo cha ushuhuda wa utu na heshima ya binadamu, zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amemkiria mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake. Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, visaidie kuwafunda vijana katika mchakato wa kupata soko la ajira. Ili kuweza kufikia lengo hili, vijana waandaliwe vyema kitamaduni, kitaaluma, kimaadili, kiutu na hata katika maisha ya kiroho, ili kuweza kupata wafanyakazi waliofundwa na kuiva barabara katika kanuni maadili; haki msingi za binadamu; mshikamano sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa kuwafunda vijana katika dhana ya kazi!

Elimu na Kazi ni chada na pete, mambo yanayotegemeana na kukamilishana, ili kuweza kupata ufanisi bora, tija na maendeleo ya wengi. Hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha vipaji na karama za vijana katika ulimwengu wa kazi, ili hatimaye, kuwa na vijana wanaoshiriki kikamilifu katika kudumisha mshikamano wa dhati na jirani zao. Leo hii changamoto kubwa ni mchakato wa utandawazi wa teknolojia, dhana inayopaswa kujikita katika mshikamano, ustawi na maendeleo ya wengi.

Vijana wapewe nafasi ya kushiriki katika ugunduzi utakaosaidia kuendeleza sekta mbali mbali za uzalishaji na huduma kwa jamii. Serikali, Makampuni na watu binafsi wanapaswa kuonesha mshikamano, ili kusaidia kusongesha mbele gurudumu la maendeleo na ustawi wa wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, kuna haja ya kuwa na uwiano bora wa maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii, kwani hadi sasa Kusini mwa Italia kunataliwa na umaskini mkubwa, wakati ambapo Kaskazini mwa Italia wananchi wengi wanajivunia maendeleo makubwa na huduma bora zaidi.

Kuna wimbi kubwa la vijana wasomi, watafiti na wafanyabiashara maarufu wanaolazimika kukimbia Italia ili kutafuta maisha bora zaidi sehemu nyingine za dunia. Hali hii inachangiwa pia na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi ya kihalifu nchini Italia. Ili kukabiliana na changamoto hii, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa kupambana umaskini; kuwasaidia watu wasiokuwa na fursa za ajira; kuanza mchakato wa mageuzi ya kiteknolojia kwa kuwapatia vijana nafasi ya kuwa wagunduzi, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Maaskofu Katoliki Italia wanakiri kwamba, njia hii ni ndefu inayowajumuisha wengi na kwamba, inajikita katika ekolojia shirikishi, dhana muhimu sana katika maisha ya hapa duniani! Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linavyohitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.