2016-04-28 06:59:00

Mwaka wa Wanaume ulivyofunika Jimbo kuu la Mwanza! Yaani we acha tu!


Maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania yaliyoongozwa na kauli mbiu “Mwanaume mkatoliki ni mhimili imara wa Taifa la Mungu” limekuwa ni tukio la kihistoria ambalo limeibua changamoto nyingi katika maisha na utume wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza. Umekuwa ni wakati muafaka wa kuenzi tunu ya wanaume na ubaba; nafasi ya kujiona na kujitathmini kwa unyofu na ukweli; kutambua, kutafakari na kutekeleza wito sanjari na kuboresha ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, amesukumwa kwa mwono adilifu, maisha na utume wa Kanisa kuona na kutathmini kwa kina na mapana nafasi na utume wa wanaume ndani ya Kanisa. Kwa kawaida wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa kusukumwa na mwono chanya kwa Wanaume wa Wakatoliki, ametaka watambua na kuthamini uwepo wao kama utashi wa Mungu mwenyewe na kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili waweze kukamilishana kwa kushirikishana neema, vipaji na baraka. Wanaume ni watu wenye vionjo na mielekeo ambayo ni changamoto kubwa katika maisha yao!

Kumbe, ilikuwa ni muhimu kujitathmini, kujipanga na kujikubali, ili kutambua fursa yao ndani ya Kanisa ili waweze kuwa ni nguvu inayo Injilisha zaidi kuanzia kwa Kanisa la nyumbani yaani familia, Kanisa la ujirani yaani Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Kanisa la Parokia, Jimbo na Kanisa la Kiulimwengu. Wanaume ndani ya Kanisa ni hazina muhimu ambayo wakati mwingine imefichika. Hazina hii haina budi kutoka na kujitokeza zaidi ili kuifaidisha familia ya Mungu. Wanaume ni baraka na zawadi ya Mungu.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza inatambua kwamba, wanaume wana utume halali usiokuwa na mbadala katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Lakini, wanaume wamekuwa wakitupiwa “madongo” kwa kutoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kuwashirikisha wanaume zaidi kwa kuwahamasisha kufurahia uwepo wao; wajikusanye na kujitosa zaidi katika kutekeleza dhamana na wito wao, huku wakijiamini.

Askofu mkuu Ruwaichi anasema, maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Mwanza yamefungwa rasmi wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu, hapo tarehe 3 Aprili 2016, hapo Watu wa mataifa waliposhika tama kuona umati wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza wakiwa vifua mbele kutangaza na kushuhudia utume wao ndani ya Kanisa. Hii ilikuwa ni nafasi ya kuendeleza na kuimarisha utume wa wanaume wakatoliki ndani ya Kanisa, kwani wao wanashiriki Ubaba wa Mwenyezi Mungu. Ilikuwa ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea ili ushiriki wao uwe na tija, mvuto na mashiko zaidi. Ilikuwa ni nafasi ya kufanya majumuisho ya maadhimisho ya Mwaka wa wanaume wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza, tayari kujiwekea sera, malengo na mikakati ya kutekeleza kwa sasa na kwa siku za usoni.

Jumapili ya huruma ya Mungu ilikuwa pia ni nafasi ya kuomba toba kutokana na mapungufu na udhaifu ambao umeoneshwa na wanaume wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza katika maisha na utume wao, ili kuwa na ari na mwamko mpya! Itakumbuka kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa wanaume wakatoliki ni mwendelezo wa matunda ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Mwanza, cheche ya mwanzo mpya katika maisha na utume wa Kanisa; maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Mwaka wa familia na kwa wakati huu maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu. Zote hizi ni juhudi za familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza kuhakikisha kwamba, inakuwa kweli chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.