2016-04-04 12:57:00

Jengeni na kudumisha urafiki ili kukuza amani na udugu!


Kardinali Orlando Quevedo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cotabato, nchini Ufilippini katika ujumbe wake wa Pasaka anawataka wananchi wa Ufilippini kujenga na kudumisha umoja na urafiki, ili kukuza na kudumish misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mchakato huu unawezekana hata kama watu wanatofautiana katika misingi ya imani na dini zao, lakini amani na urafiki ni tunu ambayo inawaamba watu wote pasi na ubaguzi.

Ujumbe wa Pasaka unabeba uzito mkubwa kwa Wakristo na Waislam ambao wote wanaishi nchini Ufilippini lakini kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, wamejikuta hata katika udugu wao wanakinzana kiasi hata cha kupigana vita. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ameikabidhi mikononi mwa binadamu kuitunza na kuiendeleza; kumbe hakuna sababu ya kupigana vita wala kunyanyasana!

Watu wajifunze utamaduni wa kushirikiana, kushikamana na kusaidiana kama ndugu licha ya tofauti zao msingi ambazo zinapaswa kuwa ni utajiri mkubwa wenye mvuto na mashiko! Wananchi wakijikita katika uelewa huu, amani, amani na utulivu; udugu upendo na mshikamano vinaweza kukita mizizi yake katika maisha ya wananchi wa Ufilippini. Vitendo vya kigaidi vinavyoendelea sehemu mbali mbali za dunia ni tishio la usalama, amani na mafungamano ya kijamii.

Yesu Mfufuka alipowatokea wafuasi wake waliokuwa wameelemewa na wasi wasi na woga kutokana na madhulumu ya Wayahudi, aliwaabia amani kwenu! Haya ndiyo matashi mema ambayo Mama Kanisa anapenda kuwatakia watu wote duniani wakati huu wa maadhimisho ya Kipindi cha Pasaka. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, lakini kwa namna ya pekee, Wakristo wanaalikwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na mabalozi wa amani duniani, kwa kuvunja na kuvuka vizingiti vya maamuzi-mbele ambayo ni chanzo kikuu cha kinzani na mipasuko ya kijamii.

Mchakato wa Serikali ya Ufilippini wa kutaka kuunda eneo linalojitegemea kutokana na kuwa na idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam, umegonga mwamba, baada ya Bunge la Ufilippini kutoridhia mchakato wa utengano huu ambao ungelifanya eneo la Mindanao kujitegemea. Muswada umerudishwa tena Serikalini kwa marekebisho na utajadiliwa tena hapo tarehe 9 Mei 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.