2016-03-24 09:29:00

Mapadre ni mashuhuda na wahudumu wa huruma ya Mungu!


Mapadre ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu linalowapatia mapadre dhamana ya kutangaza Neno la Mungu, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kushuhudia upendo wa Mungu katika maisha ya watu, hususan kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: Fumbo la imani linaloadhimishwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Watu wa Mungu. Mapadre ni wahumu wa Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma, Siku ya Alhamisi kuu, Kanisa linapotafakari kuhusu siku ile Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu, Ekaristi na Amri ya mapendo inayomwilishwa katika huduma makini anasema, Padre anapaswa kukumbuka daima kwamba, ni chombo, shuhuda na kielelezo cha Yesu mwenye huruma na mapendo.

Waamini wanapomwangalia Padre wamwone kweli Yesu Kristo, ufunuo wa huruma ya Baba wa milele. Mapadre ni mwendelezo wa huduma ya Kristo anayefundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wake kwa njia ya Neno na Sakramenti, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Mapadre wanawasaidia waamini kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa njia Sakramenti ya Upatanisho, pale waamini wanapokimbilia katika kiti cha huruma ya Mungu. Padre asiyependa kukaa kwenye kiti cha huruma ya Mungu huyo anawafungia waamini hazina ya huruma na msamaha wa Mungu.

Padre ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu pale anapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inayofanyika katika hali ya kimya kikuu, ili kumpatia nafasi Kristo Yesu kuzungumza na watu wake. Padre Asiopotekeleza dhamana hii kwa moyo wa ibada na uchaji, Yesu wa Ekaristi atabaki mbali na waja wake. Wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Mapadre wakubali kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Wawe makini kusoma alama za nyakati, ili kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili huduma ya upendo kwa Watu wa Mungu.

Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma anawatakia Mapadre wenzake wakati huu wa Mwaka Mtakatifu uchomvu mtakatifu unaotokana na huduma kwa watu wa Mungu katika kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; katika pilika pilika za huduma za kichungaji, hija na matendo ya huruma. Hii ndiyo furaha inayobubujika kutokana na Upadre wa huduma; huduma inayohitajika na Watu wa Mungu! Padre akiona kwamba, haitajiki hapo atambue kwamba, maisha na wito wake unakosa mashiko na mvuto na kwamba, huo sio Upadre wa huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.