2016-03-16 08:36:00

Kanisa letu ni Kanisa la mashuhuda!


Tangu mwanzo, Kanisa limeshuhudia watoto wake wakiyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na damu yao, imekuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. “Kanisa letu ni Kanisa la mashuhuda” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza majiundo endelevu ya kimissionari yaliyoandaliwa na Kituo cha ushirikiano wa kimissionari na Makanisa ya Jimbo kuu la Roma na kufanyika kwenye Seminari kuu ya Roma.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican akishiriki katika majiundo haya amesema kwamba mashuhuda wa imani na wafiadini wanaonesha ukuu wa Kanisa, kwani hawa ni watu waliokuwa na ujasiri wa kujitosa bila ya kujibakiza, ili kumwambata na kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yao, ili kutetea Ukweli wa Injili!

Katika miaka ya hivi karibuni, nyanyaso, dhuluma na mauaji ya Wakristo yameongezeka kwa wingi sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na ubaguzi; mambo ambayo yanahatarisha uhuru wa kuabudu na mafungamano ya kijamii. Hizi ni changamoto zinazoendelea kujitokeza katika medani mbali mbali za kimataifa, zinazohitaji ujasiri kwa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu; demokrasia na usalama wa kimataifa.

Taarifa zinaonesha kwamba, wafungwa wa masuala ya kidini, wanateseka zaidi ikilinganishwa na wafungwa wengine. Biashara haramu ya silaha; uchu wa mali na madaraka ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kugumisha mchakato wa haki, amani na maridhiano huko Mashariki ya Kati na matokeo yake na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya Wakristo huko Iraq inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka.

Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria, kimesababisha Wakristo zaidi ya laki moja kukimbia kutoka Jimbo Katoliki la Maiduguri. Makanisa 350 yamechomwa moto na kuharibiwa vibaya. Hali ni mbaya kuliko maelezo nchini Libya. Changamoto zote hizi zinaonesha umuhimu wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirikiano wa kimataifa ili kusimama kidete kupinga mauaji, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo kwa kuimarisha uhuru wa kidini na haki msingi za binadamu. Mauaji  kwa misingi ya kidini yana athari kubwa katika uhuru wa binadamu na haki zake msingi.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, pengine leo hii kuna mashuhuda wengi wa imani kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, watu wengi wamemezwa na malimwengu, hawataki kusikia kweli za Kiinjili zikitangazwa na kushuhudiwa na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Ndiyo maana katika baadhi ya nchi Mkristo akikutwa na Biblia au anafundisha Katekesi, anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela! Haya ni mambo yanayokinzana na uhuru wa kuabudu, haki ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Msimamo wa Vatican katika masuala kama haya: daima ni kutetea mafao ya wengi, haki, amani, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Vatican inapenda kuhimiza kwa namna ya pekee, majadiliano ya kidini na kiekumene; ukweli na uwazi; haki na amani pamoja na kuheshimu Sheria za Kimataifa kwa kutambua kwamba, kila serikali inawajibika kuwalinda wananchi wake. Huu ndio ukweli unaosimamiwa na Vatican katika masuala ya Kimataifa. Wakristo kama walivyo wananchi wengine wana haki ya kushiriki katika ustawi na maendeleo ya nchi yao bila kubaguliwa wala kutengwa kwa misingi ya udini! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwalinda watu wanaokumbana na vita, nyanyaso na dhuluma, kadiri ya sheria za kimataifa; ingawa sheria hizi bado zinapwaya kwa kiasi kibwa!

Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha majadiliano ya kidini na kiekumene; ya kisiasa na kimataifa katika misingi ya ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi na kwamba, tofauti za kidini na kiimani ni utajiri mkubwa unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wengi. Mauaji ya Wakristo 21 nchini Libya pamoja na yale ya wanafunzi 142 kutoka katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya, yalitoa changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani kwa miaka mingi, Wakristo wanauwawa kikatili, lakini Jumuiya ya Kimataifa bado haijawa makini kuwalinda na kuwatetea.

Uhuru wa kuabudi unapaswa kuendelezwa sanjari na kukuza utamaduni wa majadiliano ya kidini, kwani kwa kuzingatia misingi ya haki, ustawi na maendeleo ya wengi; utu na heshima ya binadamu, dini zinaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya watu! Misimamo mikali ya kidini na kiimani; kisiasa, kijamii na kiuchumi ni mambo hatari sana kwa haki, amani, usalama na mafungamano ya kijamii.

Vatican kwa kutumia Mabaraza mbali mbali ya Kipapa inaendeleza mchakato wa majadiliano kwa kutambua kwamba, hii ni huduma makini kwa binadamu inayopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya ukweli na upendo; amani na utulivu. Kanisa linaendeleza mshikamano wa huduma na upendo katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa Kikristo unaomwilishwa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ushuhuda huu wakati mwingine una gharama kubwa ya maisha kama ilivyojitokeza hivi karibuni kwa Watawa wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama watawa wa Mama Theresa wa Calcutta kuwawa kikatiliki huko Yemen. Kumbe, wamissionari wanahamasishwa na Mama Kanisa kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha ya kila siku. Ushirikiano wa kimissionari ni muhimu sana katika kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.