2016-03-11 08:25:00

Vitimbwi Mahakamani! Patashika nguo kuchanika!


Kwa wale wasiowahi kuburuzwa kortini au mahakamani kwa makosa au hata kama mashahidi basi wajipongeze wenyewe. Lakini leo tunaalikwa kuingia mahakamani kusikiliza kesi ya mwanamke mmoja aliyefumaniwa kwenye ngono. Kesi hii ni ya namna yake kwa sababu mlalamikaji siyo bwana mwenye mke. Mtuhumiwa amesimamishwa katikati ya jopo la mahakimu wanaodai haki itendeke na sheria ichukue mkondo wake. Kabla ya kuisikiliza kesi yenyewe tuangalie kwanza makandokando ya tuhuma hizo kihistoria. Katika kipindi cha karne ya 1 hadi 5 kulikuwa makosa matatu ya jinai yasiyosameheka nayo ni: Uuaji, Uasi wa dini na Uzinzi. Wakristo wa karne ya kwanza wakakinyofolea mbali katika Biblia kile kipengee ambacho Yesu anasema “mimi sikuhukumu”.

Kadhalika Mtakatifu Augustino aliongeza kusema kuwa matamshi hayo yalipotosha jamii, kwani yalionesha kana kwamba amempa “ruksa” kusharatisha na kumwaga upupu mtaani!. Hivi wakosefu walitengwa kabisa na jamii. Katika karne ya pili ya Haermae Pastor ndipo wakosefu walirudishwa tena katika jamii lakini kwa masherti magumu sana. Hadi ilipofika karne ya tatu ndipo maneno ya Yesu “mimi sikuhukumu” yakaingizwa tena katika Injili na kuyapatia masharti kwamba mtu“ajute na asirudie tena.”

Lakini utata zaidi wa fasuli upo kwa mwandishi wake. Kesi ya mama huyu mzinzi haiko pahala pake katika Injili ya Yohane kwani haina mantiki, wala lugha yake siyo ya Yohane. Kumbe, yasemwa imenyofolewa kutoka Injili ya Luka inakoleta mantiki na kuendana na mada, lugha na msamiati wa Luka sura ya 21. Huko kituko hiki kinakosekana. Hebu angalia maneno ya Yohane kabla ya kituko hiki: “Naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea naye akaketi, akawa akiwafundisha.” Kumbe maneno hayo yamekaa vizuri katika Injili ya Luka: “Basi kila mchana alikuwa akifundisha hekaluni na usiku huenda kulala katika mlima uitwao wa Mizeituni. Na watu wote walikuwa wakiamka mapema waende hekaluni ili kumsikiliza.” (Lk 21:37-38). Kumbe, watu walienda Hekaluni asubuhi, muda unapochomoza mwanga wa jua. Yesu ni mwanga na jua la kweli. Halafu Hekaluni palitumika pia kama mahakama ya kuhukumu kesi kwa haki kadiri ya sheria na Torati ya Musa.

Asubuhi linapotokea jua la haki yaani Yesu, lwapo pia Waandishi na Mafarisayo wenye haki. Wote wanakutana hekaluni (mahakamani). Hapo ndipo anapandishwa kizimbani mama mzinzi na kuwekwa katikati ya jopo la mahakimu hawa. Watazamaji tunatamani kuona jinsi gani kesi itakavyounguruma na watu wanavyochezeshwa pachanga kwa sheria!“Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.”. Wanamtuhumu na kusema: “Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika Torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?” Sheria iliagiza waziwazi kuwa kama mwanamke aliyefumaniwa alikuwa amechumbiwa (kuolewa) lakini hajaenda kukaa kwa mume, huyo anapigwa mawe. Mwanamke aliyeolewa na anakaa na mumewe huyo alinyongwa shingo. Mwanamke huyu kumbe aliolewa lakini hakwenda kwa bwana hivi alistahili apigwe kwa mawe hadi kufa! Tobaa!

Hapa ieleweke pia kwamba adhabu hii ilikuwa inawaficha wauaji. “Kifo cha wengi arusi.” Hakuna aliyejulikana kuwa ameua kwani wameshirikiana. Kwa hiyo hakukuwa kuwajibika kwa mtu binafsi. Wauaji hawa wanataka kuondoa uovu ulimwenguni bila kujua kwamba uovu uko ndani ya kila mtu, naye anajaribu kujificha katika kundi ili kuepa kuwajibika. Hii ni sawa ni ule ukatili uliozuka wakati fulani katika jamii nyingi za kuwachoma wahalifu kwa moto, ili watoweke katika uso wa dunia! Mahakimu hawa wanasafisha uovu kwa kutumia haki. Wao walijua sheria moja tu kwamba wema una thawabu na ubaya una adhabu. Sasa imebaki hukumu ya Yesu! Katika Agano la kale neno haki linatokea mara 276 likieleza juu ya haki ya Mungu.. Haki ya Mungu ni huruma na kukufanya uishi vyema ndani mwako.

Sasa watu hawa walitaka kumchokoza Yesu naye akaamua kuwajibu kwa kukaa kimya na kwa kuandika chini. “Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.” Mt. Yerome anasema kuwa Yesu aliinama na kuandika dhambi zao ardhini, na baada ya kila mmoja kuzisoma akaona aibu na kuamua kuondoka kivyake vyake akiogopa “jipu” lake lisije litashughulikiwa hadharani, hapa kungekuwa ni pata shika nguo kuchanika!. Maelezo haya ni ya uwongo na hayana mantiki kwa sababu, sakafu ya Hekalu la Yerusalemu haikuwa ya udongo au mchanga unaoweza kusoma, bali ilisakafiwa kwa marumaru yaani mawe magumu. Kwa hiyo Yesu alikuwa anaandika juu ya jiwe. Kitendo cha Mungu kuandika kwa kidole chake unakuta katika Agano la kale alipoandika amri kumi juu ya mbao za mawe. “Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.” (Kut. 32:16).

Lakini baadaye Mungu anasema kuwa ataandika sheria hizo mioyoni mwa watu. “Bwana asema: Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika.” (Yer 31:33). Kadhalika, “Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.” (Ezek. 36:27). Kwa hiyo badala ya kuandika sheria juu ya jiwe, sasa Mungu anaandika moyoni kwa sababu moyoni hutoka hukumu kadiri ya mpango wa Mungu. Kwa hiyo kitendo cha Yesu kukaa kimya chamaanisha kujiingia ndani yake mwenyewe kufikiri na kutafakari. Wakati tendo la kuchora ardhini kwa kidole, linakumbusha sheria na Torati za Musa zilizoandikwa jiweni. Hapa Yesu anataka kuwasomesha kwa matendo bila maneno, mabadiliko ya katiba kutoka ile iliyoandikwa kwenye jiwe na katiba mpya iliyoandikwa moyoni. Kwa hiyo hapa Yesu anataka kuwanusuru kwanza hawa wafarisayo kabla ya kumnusuru mwanamke huyu, kwani anataka waondokane na haki ya kibinadamu bali waione haki ya Mungu.

Hii ni njia pekee ya kuwanusuru watu wasiowajibika, watu ambao wanaficha uovu na kasoro zao katika kundi na magenge ya watu!  Hata leo wapo watu wanaoficha uovu wao katika kundi, yaani mmoja unajidai kuwa mwenye haki na unaungana na wengine kurusha mawe ya masengenyo, ya uchochezi kwa njia ya ulimi na kuumiza wengine lakini bila kujulikana kwa sababu uko katika kundi. Kumbe Yesu anakaa kimya ili kulisambaratisha kundi na kumfanya kila mmoja ajihoji mwenyewe na kuwajibika. Kumbe mafarisayo na waandishi wale hawakuwa na dogo, “wakazidi kumhoji.” Hapo Yesu akaona awatolee uvivu akawaambia: “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Mkazo unawekwa asiye na dhambi hii! Kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu! Hapo sasa kundi likayeyuka lenyewe kwani kila mmoja alifanya maamuzi yake mwenyewe binafsi. Akahoji kama kweli anamtakia mema yule mwanamke au kulikuwa maslahi ya binafsi.

Mahakimu wale wakaanza kutoka mmoja mmoja kuanzia wazee. Kuonesha kwamba haki ya binadamu inafanya mabaya, na haki ya Mungu inaokoa. Hadi mwisho “Akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.” Mazingira yaliyobaki ya Yesu na mwanamke peke yake ni fundisho zuri kwetu. Endapo unashambuliwa na kuchukiwa wewe acha wakuache kwani upo sasa na Yesu peke yenu. Ndicho anachosema Yohane katika barua yake, “hata kama moyo wako ungekugombeza kumbuka kwamba Mungu ni mkubwa kuliko moyo wako.” Waondoke wote wanaokudhulumu nawe ubaki na Yesu.

“Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, “Mwanamke hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?” akajibu “Hakuna Bwana.” Yaani kwa vyovyote katika maisha hakuna anayeweza kukuhukumu, bali kila mmoja anajihukumu mwenyewe. Wewe uwe na uhakika na kuaminia upendo wa Mungu usio na masharti. Kisha Yesu akasema: “Wala mimi sikuhukumu,” Kama vile Yesu angemwambia: “Chochote utakachofanya ukumbuke kwamba Mimi sitakuhukumu kabisa. Kwa sababu haki yangu siyo ya kuhukumu bali ni ya kuokoa maisha.” Nadhani baada ya kusheshe ile yule dada aliendelea tu na shughuli zake kama kawaida, ikiwa ni pamoja na kurudia tena kutenda makosa yake. Hii ni tabia ya binadamu kurudiarudia makosa. Lakini hata kama aliendelea tena kusharatisha, daima aliyakumbuka maneno ya Yesu: “Hata mimi sikuhukumu.” Huo ni wosia pia kwa Makuhani, yaani kujikumbusha daima kule kusamehe kwa Mungu. Kila atendaye dhambi hata kama ingekuwaje, hana budi aukute moyo mkuu wa huruma na upendo usio na mipaka ilivyojidhihirika katika moyo wa Yesu. “Hata mimi sikuhukumu.”

Ndugu zangu, hii ndiyo changamoto pevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu na kwamba, huruma ni kiini na muhtasari wa imani ya Kikristo. Ikumbukwe daima kwamba, haki ya Mungu ni huruma yake na kwamba, huruma ni jina jingine la Mungu! Mwenyezi Mungu ndiye hakimu mwenye vigezo sahihi vya kutenda haki, anayetoa fursa kwa mwamini kuweza kutubu na kumwongokea kwa kutoka katika hukumu ya kifo, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na sheria ya Mungu iliyoandikwa katika akilini na moyo wa mwanadamu! Mwaka wa huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha! Jaribu, utagundua siri ya urembo!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.