2016-03-04 15:54:00

Iweni na huruma kama Baba!


Ndugu zangu karibuni tena katika tafakari ya neno la Mungu dominika hii ya nne ya kwaresima. Tumesikia juma lililotangulia juu ya wito wa Mungu kwetu sisi wa kuwa tayari kumtumikia. Musa anaitwa na anaambia avue viatu vyake. Atoke katika mazingira yake aende apeleke habari ya ukombozi kwa taifa lake. Sisi nasi tukaalikwa kutoka katika mazingira yetu na kuwa tayari kutumika na Mungu. Wito uliowekwa wazi na somo la injili ukitualika kubadilika na kuongoka, kuwa tayari kuvua hali zetu za kibinadamu na kuvaa viatu vya Mungu na kuwa tayari kumtumikia.

Leo tunasikia kuhusu kukubali au kukiri kosa. Si jambo rahisi kibinadamu inawa inawezekana. Tumepata bahati wakati wetu huu kushuhduia uwezekano huo. Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini aliunda kamati ya usuluhishi na upatanisho. Mbele ya wengi ilionekana kitu kigumu na hatari lakini mwishoni ilitoa mafanikio makubwa. Ni mahali hapa mtenda maovu na aliyetendewa maovu walipata nafasi ya kukutana uso kwa uso, kukaa pamoja, mmoja akakiri kosa lake dhidi ya mtendewa, kuomba msamaha na msamaha kufikiwa. Tunafahamu kuwa tendo la upatanisho ni jambo gumu sana kwani hata mtenda jema aweza kuonekana tishio mbele ya baadhi ya watu. Angalia injili ya leo – linaanza shitaka –  huyu hula na wenye dhambi. Jibu la Yesu ni kuwa Mungu humpokea bado mdhambi na kumpa nafasi ya kutubu dhambi.

Kupatana na adui ni kitu kigumu sana kwa mwanadamu. Tunaona jinsi watu wanavyohangaika kulipa kisasi kwa waliowakosea. Au jinsi mtu anavyohangaika kutafuta haki ikiwa amekosewa. Lakini kutafuta haki huku hupelekea pia hata kumdhuru mwingine. Hutokea pia hata hilo hitaji la kutafuta haki likaongeza uadui zaidi. Katika somo la kwanza tunaona jinsi watu wanvyohangaika kulipa kisasi. Mtoto mmoja mdogo alisikika akisali hivi – utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wale waliokufa dhidi yetu. Tunaambiwa kuwa msamaha wa kweli huanza toka ndani. Mtume Petro alipomwendea Yesu na kuuliza habari ya msamaha anatufundisha jambo kubwa sana. Tukisoma Mt. 18:21 – kuhusu kusameheana – kisha Petro akamwendea, akasema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Mtume Petro hakusema aliyenikosea aniombe msamaha mara ngapi

Kadiri ya mafundisho na mapenzi yake Mungu, tiba sahihi ya ugomvi ni upatanisho, pamoja na ugumu wake ulivyo. Mungu ametaka upatanisho nasi na kati yetu wenyewe. Masomo yetu ya leo yaonesha mapenzi ya Mungu juu ya upatanisho. Kinachoonekana wazi ni kuwa  ili upatanisho utokee ni lazima Mungu aingilie kati. Sisi tunaalikwa kushiriki katika tendo hili. Hili liko wazi katika somo la kwanza na la pili. Mtume Paulo anasema mpatanishwe na Mungu. Na anasema kwa vile sisi ni watu wake Bwana, sisi ni viumbe vipya. Tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe na katika mstari wa 18 wa somo hili la pili tunasoma kuwa naye anatupa sisi huduma ya upatanisho. Mtakatifu Francisko wa Assis husali katika sala zake ‘Ee Bwana unifanye chombo cha amani yako”. Hivyo huu unakuwa ni wajibu na si hiari. Katika somo la kwanza tumeona kuwa Mungu yuko daima na anawakumbusha watu wasahau ile hali ya utumwa na waishi kama watu huru. Tendo la upatanisho lina asili yake ndani ya Mungu na sisi watoto wake tunapaswa kuwa watu wa upatanisho. Mtume Paulo anasisitiza haja ya mwanadamu kuupokea huu upatanisho.

Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu aliitwa Edwin McMasters Stanton. Alikuwa tayari kufanya lo lote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa baraza la mawari jina la Stanton likawepo. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza Rais chuki ya Stanton dhidi yake. Rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni. Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuongoza Marekani na  watu wake. Akamfanya waziri wa ulinzi na akaifanya kazi ile kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.

Habari ya Baba mwenye huruma katika somo la Injili nayo yatupa changamoto kubwa. Lakini kubwa zaidi ni ile roho ya yule mtoto kutambua na kukiri kosa. Anaamua kufunga safari ya kurudi kwa baba na kuomba msamaha. Huyu anajitambua na kukiri kosa lake. Wengi wetu hatuwezi kufikia hali hii ya juu kabisa ya kiroho.

Ilitokea siku moja bwana jela alitaka kutoa msamaha kwa mmoja kati ya wafungwa katika gereza lake. Yeye alitaka kutoa msamaha kwa mfungwa atakayezungumza wazi kile kilichomsibu. Kila mfungwa alidai kuwa ameonewa na hakutendewa haki kuwa pale gerezani. Mwishoni kabisa akatokea mfungwa mmoja aliyetamka wazi kosa lake na kukubali kuwa kuwepo kwake pale gerezani ilikuwa sawa kabisa. Huyu alikiri kosa lake. Bwana jela akamfungua pingu na kumwacha huru kwa vile alikiri kosa lake. Wengi wetu hatufikii hatua hii ya kukiri na kukubali makosa. Na hii inagharimu sana maisha yetu na mahusiano kati yetu na Mungu.

Habari ya kaka anayechukia kurudi kwa ndugu yake inasikitisha sana. Pengine anawakilisha hali zetu sisi ambao hatuko tayari kutoa msamaha. Kwake huyu ndugu yake alikuwa tayari adui. Tunakumbushwa kuwa hatuna budi kuwa tayari kuukubali msamaha wa baba kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.