2016-03-04 15:34:00

Hapa ni mnuso kwenda mbele! Mwenye roho ya kwanini atajiju mwenyewe!


Mara nyingi katika familia kunatokea sintofahamu kati ya wazazi na watoto wao. Wazazi wanaweza kuwatakia mema watoto wao. Kumbe watoto wanadhani wanaburuzwa na kunyimwa uhuru. Hivi wanajiengua na wazazi na kwenda kuishi mbali. Mapato yake mara nyingi uhuru huo unawatokea puani. Leo tutashuhudia sintofahamu ya namna yake iliyotokea kati ya baba na watoto wake wawili wa kiume. Watoto walitaka kumfundisha baba yao jinsi ya kuwalea wakati hawakumfundisha jinsi ya kuwazaa. Hali hii ya watoto iko ndani ya kila mmoja wetu. Hebu tufuatilie kwa karibu mambo yalivyokuwa katika familia hiyo. Mtoto mmoja anatoka nyumbani na kujitenga kabisa na baba kwa sababu alimwona baba yake kuwa tishio na mnyanyasaji. Mtoto mwingine alibaki nyumbani lakini naye mahusiano yake na baba yalikuwa na dosari kubwa. Tabia za watoto hawa wawili unaziona katika makundi mawili ya wahusika wanaotajwa katika maingilio ya Injili ya leo.

Hebu angalia jinsi fasuli hii inavyoanza: “Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize, Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Kundi la kwanza ni la wa wadhambi ndio wanaovutwa kuja kumsikiliza Yesu. Watu hawa wanasukumwa kumwendea Yesu na kumsikiliza ili kupata neno la furaha, neno la matumaini, neno linalojibu maswali yanayowatia uchungu na masikitiko katika maisha yao. Kumbe inampa mtu uchungu, masikitiko na mahangaiko, hiyo ndiyo inayowapelekea watu kutafuta furaha ya kweli iliko kama walivyofanya wakosefu hawa Watoza ushuru na wenye dhambi ndiyo wakamkimbilia Yesu na kumsikiliza. Hii ndiyo hali ya mwana mpotevu. Kwa hiyo ni rahisi sana kuwaongoa wakosefu. Kundi la pili ni la Mafarisayo na waandishi. Hawa ni watu wenye haki, waaminifu, watoa sadaka, watu wa dini, lakini wako nje wakimkosoa Yesu kwa hoja kwamba anakula na wenye dhambi. Hii ndiyo hali ya kaka mkubwa. Ni vigumu sana kuwabadilisha watu wenye fikara za kuwa bora.

Lengo la mfano huu siyo kuwaongoa wenye dhambi kama alivyo mwana mpotevu au kuwaongoa wenye haki kama kijana wa kwanza. La hasha, bali ni kusahihisha picha waliyokuwa nayo watu hawa juu ya Mungu, kama zilivyokuwa fikra potovu za vijana hawa dhidi ya baba yao. Sisi pia tunaalikwa kubadili fikra zetu kwa kumtazama na kumfasiri Mungu itakiwavyo. Tusiendelee kumwabudu Mungu tunayemtaka sisi, bali Mungu yule wa Yesu wa Nazareti anayewapenda wadhambi. Huu ndiyo mwito wa wongofu wa ndani tunaoagizwa kuufanya katika mfano wa leo.

“Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.” Kwa kawaida urithi hugawiwa baada ya kifo cha wazazi. Kumbe kwa kijana huyu, baba yake alionekana kama vile ameshakufa. Hakutaka tena kutegemea thamani za kiutu zinazothaminiwa kifamilia na za kijamii yake. Ili kupata furaha, uhuru na kujikamilisha mwenyewe akaamua kufuata kichwa chake: “Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali” asijue kwa kufanya hivyo alijikimbia wenyewe na utu wake. Huu ndiyo uchaguzi tunaofanya sisi pale tunapotaka kufanya mambo yetu bila kumwamini Mungu. Mapato yake kijana akapoteza kila kitu: “Akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.” Dhambi ya kujitenga na baba na kujitafuta sisi wenyewe, na furaha zetu yanaishia kufilisika bila kujitambua na tunabaki uchi kama Adamu na Eva baada ya kumwacha Mungu.

“Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikaana na mwenyei mmoja wa nchi ile; naye alipeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu alimpa kitu.” Kama hufuati mantiki ya Mungu, unaishia kuwa mtumwa wa miungu yako. Hatimaye unaishia kufanya mambo yanayokutia aibu mwenyewe kama kitendo hiki cha kunyang’anyana chakula na nguruwe. Hakuna mtu aliyemsaidia kwa sababu katika ulimwengu wetu wa mashindano hakuna cha bure bali “Nipe nikupe, mkono kwa mkono.” Unabaki peke yako “ukilia na kusaga meno” kwavile “hapakuwa na mtu aliyempa chochote.”

Kijana huyu ni mfano kwetu, tunapojitenga na jumuia na kutafuta raha ambazo mwishoni zinatutokea puani. Tunapata uchungu na kukosa furaha. Kijana huyu akajitafiti kisha akaamua kurudi nyumbani kwa baba. Sasa tutaona picha halisi ya baba ilivyo. Angalia matendo matano anayoyafanya baba kwa mtoto wake ni sawa na matendo ya Mungu kwa mkosefu, ama kweli “Uchungu wa mwana anaujua mzazi.” Kwanza kabisa “Kutoka mbali anapomwona mtoto wake. Yaonekana baba alikuwa anamsubiri, kwani alijua jeuri za mtoto wake zitamwishia na atarudi mwenyewe. Pili, akamwonea huruma (kwa kigiriki ni esplanchnisthē maana yake akavutwa na moyo wa huruma.) Tatu, akamkimbilia. Licha ya uzee hakujali hata kuanguka sababu ya upendo. Nne akamdaka shingoni, hapa yaonekana alijikwaa na hivi akaishia kumwangukia mtoto wake shingoni.  Tendo la tano akambusu. Mapokezi haya yalimchanganya kijana kwa furaha. Baba mtu hakupoteza muda kusikiliza pumba alizopanga kuzisema mwanae, badala yake anawaagiza watumishi kuleta mavazi yafuatayo: “Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike” vazi refu la mtu huru, siyo vazi fupi la watumwa. Hapa unapata picha ya nguo ya ubatizo.

Paulo anasema: “Mjivike Kristo,” au “Ninyi mliobatizwa mmevaa Kristo” yaani hilo ni vazi la Mwana mpendwa wa Mungu. Anayekutana na mbatizwa budi aone uso wa Kristo, aone huruma ya Kristo, mbatizwa ni mtumishi mnyenyekevu wa Kristu. mvikeni pete kidoleni,” hii siyo pete ya wanaarusi bali ni muhuri, kwani tendo la mkristo hata kama ukiwa mkosefu na mtenda dhambi wewe unabaki kuwa mwana wa Baba. Halafu “mvisheni viatu miguuni,” hili ni vazi la mwana sio mtumwa. Baada ya kupambwa hivyo yanafuata majichano. “Mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi, kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka, alikuwa amepotea naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.”

Kila anayefanikiwa kutatua matatizo anafanya sherehe kama vile wanaoungama dhambi, kwa vile walikosa utulivu kama mwana mpotevu, sasa hujisikia furaha. Kwa hiyo kuhani asiwakatishe tamaa wakosefu wanaofika kwenye kitubio, bali kuwapokea kwa furaha kwani wanataka kupata furaha. Sasa linafuata tatizo zito la kuutambua moyo wa baba kwa yule mtoto wa kwanza. Kijana huyu alitaka kumfundisha baba yake afanye kama anavyotegemea yeye. “Basi yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba” kwamba “alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.” Yaonekana kijana huyu hakuzizoea sherehe, kwake ilikuwa “hapa kazi tu” na kupata ujira wake. Anamwita mtumwa mmoja na kumwuliza, “Mambo haya, maana yake nini?”

Kumbe, hakujua kwamba upendo wa kweli na sikukuu ya kweli ni ile isiyo na ujira wala maslahi. Mtumwa akamjibu: “Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.” Hapo ikawa nongwa. Kijana akakasirika na kukataa kuingia ndani. Anapoulizwa na baba yake kulikoni, yeye haanzi na kumwita “baba” bali: “Tazama, au hebu angalia mzee, jaribu kupima mwenyewe, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii.” Hii ndiyo picha aliyonayo mtoto huyu kwa baba yake kama ya mtumishi: “nimekutumikia kwa miaka mingi.” Mtoto huyu anajisikia kuwa ni mfanyakazi tu na sasa anafanya mahesabu ya malipo na baba yake. Kwa hiyo, ni vigumu sana kumwongoa kijana huyu kwani anamwelimisha baba yake na kumwongoa ili afikiri kama yeye. Anasema: “Lakini alipofika huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.” Kijana anamwona mdogo wake kuwa ndiye mwana kweli wa baba yake. Baba mtu anamsahihisha mtoto wake na kumwita: “Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Kumbe huyu ndugu yako alikuwa amekufa naye amefufuka;”. Baba anamwita mtoto wa kwanza kuwa “mwanae” na kumwelewesha kuwa mdogo wake ni ndugu yake kabisa.

Nadhani kijana huyu mkubwa baadaye aliingia kwenye sikukuu, lakini bila kuridhika kwani ni vigumu kumwongoa. Na kijana mdogo pia alifurahi lakini baadaye alijijutia kosa alilofanya. Ndivyo ilivyo kwetu, tunapotenda dhambi tunajuta tunaposamehewa tunakuwa na furaha, kisha tukikumbuka tena tunaona uchungu. Lakini daima tukumbuke kuwa Mungu ni mwenye upendo na huruma bila masharti. Daima tutegemee upendo na huruma ya Mungu katika maisha yetu ili tuweze kuonja furaha ya kudumu, vinginevyo ni kulia na kusaga meno! Hata kama huna, ukajitia kuwa ni kibogoyo, utapewa meno ili ukione cha mtema kuni! Achana na Baba mwenye huruma! Iweni na huruma kama Baba ndiyo kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.