2016-03-04 07:34:00

Dumisheni kanuni maadili na utu wema; tunzeni mazingira!


Watanzania na watu wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaendelea kuridhika pamoja na kuwa na matumaini makubwa kwa uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Pombe Magufuli ambaye tangu kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania amejipambanua katika kukuza na kudumisha: Sheria, Kanuni na Maadili ya watumishi wa Serikali. Amekazia ukweli, uwazi na maadili kwa kupambana na ufisadi, wizi mkubwa bandarini pamoja na kuendelea kuboresha huduma ya afya na elimu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi.

Rais John Pombe Magufuli, tangu kuchaguliwa kwake ameonesha matumaini makubwa kwa watanzania katika mchakato wa ujenzi wa miundo mbinu ili kuikwamua Tanzania kutoka katika changamoto za ukosefu wa nishati ya umeme; msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam pamoja na kufufua Shirika la Ndege la Tanzania.  Elimu bure ni kati ya pongezi kubwa zinazotolewa kwa Serikali ya awamu ya tano, ingawa bado kuna changamoto zinazopaswa kufanyiwa marekebisho, ili kuweza kufikia lengo linalokusudiwa. Kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa na uchaguzi wa marudio Zanzibar ni kati ya changamoto zinazoikabili Tanzania kwa wakati huu!

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anapoangalia mafanikio, fursa na changamoto zilizoko mbele ya Serikali ya Dr. John Pombe Magufuli wa Tanzania, anawaalika watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuonesha ushirikiano, mshikamano na kumuunga mkono Rais Magufuli ambaye ameamua kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi, hasa maskini na wanyonge.

Kuna matumaini makubwa katika maboresho ya huduma ya elimu, afya na ujenzi wa miundo mbinu. Idadi ya watoto walioandikishwa shule ya msingi kwa mwaka 2016 imeongezeka maradufu, dalili kwamba, wazazi wengi wanatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao, bali umaskini, ulikuwa unakwamisha nia hii njema. Wazazi na walezi sasa wanapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, kwa kuhakikisha kwamba, watoto wanakwenda shule kama inavyotakiwa.

Askofu Telesphor Mkude anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa. Waamini wamuunge mkono Baba Mtakatifu kwa kutunza mazingira katika hali ya usafi ili kupambana na magonjwa ya milipuko ambayo pia yamekuwa ni tishio kwa maisha ya watu! Kipindi hiki cha Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni nafasi pia ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wahitaji zaidi, ili kujiwekea hazina mbinguni na rehema katika maisha ya hapa duniani.

Ni matumaini ya Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu itakuwa ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu; kudumisha kanuni maadili, ukweli na uwazi katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali pamoja na kuendelea kuwa kweli ni wachamungu na watunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote! Yote haya yafanyike kwa sifa na utukufu wa Mungu, ustawi na maendeleo ya watanzania wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.