2016-03-03 08:49:00

Waamini walei na siasa!


Waamini walei hawana budi kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara, ili kusaidia kukuza na kudumisha mchakato wa demokrasia, haki, amani na utulivu. Waamini walei watekeleze dhamana hii kwa uhuru kamili pamoja na kuongozwa na dhamiri nyofu iliyofundwa kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Huu ni wito ambao umetolewa na Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, hapo tarehe 1 Machi 2016 hapa mjini Vatican. Tume inatarajiwa kuhitimisha mkutano wake, Ijumaa tarehe 4 Machi 2016.

Ni wajibu wa waamini walei kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ili kuchangia katika mchakato wa kulinda: utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi; haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu wanatambua kwamba, hawana wito wala mamlaka ya kuongoza shughuli za kisiasa, kumbe ni wajibu wa waamini walei kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu ili kujenga na kudumisha jamii inayojikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kutokana na changamoto ya kisiasa katika maisha na utume wa Kanisa, Tume imewaalika waamini walei watatu ili kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, lina mpango mkakati wa kuitisha kwa mara ya kwanza katika historia yake mkutano utakaowashirikisha Maaskofu na waamini walei wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kama viongozi wa serikali katika ngazi mbali mbali pamoja na wabunge ili kuchangia mawazo yatakayoboresha ushiriki wa waamini walei katika medani za kisiasa.

Kardinali Marc Ouellet amegusia kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na kumbu kumbu ya miaka kumi tangu Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipochapisha Waraka wake wa kwanza wa kichungaji, Mungu ni upendo, “Deus Caritas est” anamofafanua kwa kina na mapana uhusiano wa dhati kati ya upendo na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka huu, anawaalika waamini kuboresha fadhila ya upendo na haki katika uhalisia wa maisha ya watu wa Amerika ya Kusini.

Mchakato huu unawezekana kwa kuwa na siasa safi, demokrasia ya kweli; ushirikishwaji mkamilifu wa wananchi katika kupanga, kuamua na kutekeleza masuala yanayogusa maisha yao; kwa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi; udugu na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mambo yanayohitaji pia kuwa na sera makini katika masuala ya kisiasa na kiuchumi.

Huruma ni fadhila muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Amerika ya Kusini kwani msamaha ni chachu ya ujenzi wa urafiki wa kijamii na madaraja ya watu kukutana; msamaha na upatanisho; upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, hii ni hija makini ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Waamini walei wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara ili kudumisha mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho; ushirikishwaji mkamilifu, mshikamano na udugu katika maisha ya watu wa Amerika ya Kusini.

Amerika ya Kusini itaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa pamoja kuanzia tarehe 27 hadi 31 Agosti 2016 nchini Bogotà. Haya ni maadhimisho yanayoandaliwa na CELAM kwa kushirikiana na Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Marekani na Canada, changamoto kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.