2016-03-02 11:19:00

Familia ya Mungu Afrika Magharibi: Mshikamano, Amani na Familia!


Shirikisho la Mabaraza  ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA-CERAO limehitimisha mkutano wake mkuu wa pili uliofanyika hivi karibuni huko Accra, Ghana kwa kushutumu vita, mauaji na madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo; kwa kuwataka wananchi Afrika Magharibi kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia sanjari na kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Maaskofu katika mkutano huu, watoa mapendekezo na ujumbe kwa Familia ya Mungu Afrika Magharibi.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linasema katika ujumbe wake kwamba, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya demokrasia inayojikita katika haki na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma inayopaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa misingi ya ukweli, uwazi na usawa kati ya watu sanjari na kukazia utawala bora unaosimikwa katika sheria na maridhiano kati ya watu.

Demokrasia ni chachu ya mwingiliano na mahusiano bora ya kijamii. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana kwa kuheshimiana na kusaidiana. Viongozi wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa kuwa karibu na wananchi wao wakati wa raha na shida. Maaskofu wanaendelea kusema kwamba, misimamo mikali ya kidini na kiimani ni saratani inayojenga na kuimarisha utamaduni wa kifo na maafa kwa watu na mali zao, vitendo vinavyotekelezwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Maaskofu wanawahimiza viongozi wa Serikali huko Afrika Magharibi kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kurejesha tena: haki, amani, usalama na utawala wa sheria. Viongozi wa dini mbali mbali hawana budi kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Kanisa Barani Afrika mintarafu Waraka wa Dhamana ya Afrika, Africae munus uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Dini zinapaswa kuwa ni vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu na wala si chanzo cha vita na mipasuko ya kijamii. Kanisa kwa upande wake, litaendeleza dhamana ya haki, amani na upatanisho Afrika Magharibi. Familia inapaswa kutambuliwa kuwa ni shule ya kwanza ya haki, amani, maadili na utu wema. Ni chombo cha imani, matumaini, huruma na mapendo; chachu muhimu sana ya upatanisho wa kijamii na kitaifa. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa vijana wanaounda asilimia 65% ya idadi yote ya wananchi wa Afrika ya Magharibi. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wawasaidie vijana kupata fursa za elimu na ajira ili kukuza na kuendeleza vipaji na karama zao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na upatanisho, mbali kabisa na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya; uvunjaji wa sheria na utu wema. Waamini watambue kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata huruma na upendo wake katika uhalisia wa maisha.

Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi katika ujumbe wao kwa Familia ya Mungu wanakaza kusema, Kanisa Barani Afrika halina budi kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwekeza katika mchakato wa utamadunisho ili Injili ya Kristo iweze kugusa mila, tamaduni na mapokeo ya watu, kwa kusafisha pale ambapo kuna misigano na Habari Njema ya Wokovu.

Wakristo kwanza kabisa wakubali kuinjilishwa, ili wakishaimarika zaidi, wawe pia ni vyombo vya Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji katika medani mbali mbali za maisha. Wakristo wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kujitahidi kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika maisha yao ya kila siku. Wawe kweli ni vyombo vya haki, amani na upatanisho huko Afrika Magharibi, ili kuondokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya watu huko Afrika Magharibi.

Kanisa Afrika Magharibi linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Wakristo wanaoendelea kuuwawa, kuteseka na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Maaskofu wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yake na kukataa katu katu kumezwa na utamaduni wa kifo. Kanisa litaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Shirikisho la Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kusimama kidete kujenga, kudumisha, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia inayojengwa kati ya bwana na bibi kadiri ya mpango wa Mungu na wala si vinginevyo. Tunu msingi za maisha ya kifamilia zisipolindwa na kudumishwa, hapo: amani na utulivu viko mashakani. Waamini wawe tayari kutoka kimasomaso kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kuna haja pia ya kuwafunda vyema wakleri na watawa katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kujisadaka bila ya kujiachia kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Waamini walei wawe mstari wa mbele katika kushuhudia imani yao katika uongozi kwa kujitahidi kumuiga Kristo aliyekuja kuhudumia na kutoa maisha yake ili yawe ni fidia ya wengi.

Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi wa Kanisa 120 kutoka katika nchi 16 na umeongozwa na kauli mbiu “Uinjilishaji mpya changamoto maalum kwa Kanisa, Familia ya Mungu Afrika Magharibi: Upatanisho, maendeleo na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa Shirika la Habari za Kanisa Barani Afrika, CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.