2016-03-02 15:17:00

Amerika wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka kwa Familia ya Mungu Amerika kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Hivi ndivyo wanavyosema Maaskofu kutoka Amerika waliohitimisha mkutano wao wa siku tatu hivi karibuni huko Tampa, Florida nchini Marekani. Zimekuwa ni siku za kukutana, kujadiliana, kusali na kutafakari kwa pamoja maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mkutano huu kwa mara ya kwanza ulifanyika kunako mwaka 1967 kwa kuyashirikisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Marekani, Canada na Amerika ya Kusini.

Mkutano huu imekuwa ni nafasi ya kutafakari kuhusu: matatizo, changamoto na fursa za shughuli za kichungaji kwa Familia ya Mungu Amerika katika ujumla wake mintarafu mwanga wa changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico, Equador, Bolivia, Paraguay na Marekani. Mkutano wa maaskofu unawasaidia kushikamana na kushirikiana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kuwawezesha Maaskofu kutekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa uaminifu zaidi.

Maaskofu wanaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao. Wawe tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima wakitafakari Uso wa huruma, tayari kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji.

Viongozi wa Kanisa wawe kweli ni manabii, sura na mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha huruma ya Mungu si tu kwa maneno, bali kwa mifano bora ya maisha yao yenye mvuto na mashiko kwa Familia ya Mungu. Wakristo wanapaswa kuwa makini kwa kusoma alama za nyakati ili kutambua changamoto, fursa na matatizo yanayoendelea kuliandama Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili kweli waamini nao waweze kuwa ni mashuhuda wa uwepo endelevu wa huruma ya Mungu kwa ndugu, jirani na marafiki zao.

 Wahamiaji na wakimbizi; Uinjilishaji mpya; haki msingi za binadamu; Utamaduni wa kifo; athari za mitandao ya kijamii katika makuzi na malezi ya vijana wa kizazi kipya ni changamoto pevu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Familia ya Mungu Amerika inahamasishwa kujijengea utamaduni wa kukutana mara kwa mara na Kristo Yesu kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.