2016-02-24 06:57:00

Papa Francisko amewakuna wananchi wa Mexico!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico amekuwa kweli ni mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, aliyebahatika kukutana na watu zaidi ya millioni kumi waliotanda njiani ili kumsalimia na kumtakia matashi mema na wale waliobahatika kuhudhuria katika ibada na mikutano mbali mbali iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 12- 18 Februari 2016. Hayo yamebainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Kanisa Katoliki nchini Mexico linaundwa na Majimbo 93. Waamini kutoka katika majimbo haya wameitikia kwa ari na moyo mkuu ujumbe wa Maaskofu uliowahamasisha kukutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico. Waamini waliokuwa wanahudhuria kwenye ibada na mikutano ya Baba Mtakatifu ni wale waliokuwa na tiketi zilizokuwa zimetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, lakini kabla ya matukio haya kuanza rasmi, waamini pamoja na watu waliokuwa wamekusanyika katika maeneo haya waliweza kuruhusiwa kushiriki, ili kukutana na Mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, tayari kuwahamasisha ili nao waweze kuandika ukurasa mpya kwa ajili ya nchi yao.

Taarifa inaonesha kwamba, Maaskofu kutoka Mexico walioshiriki kikamilifu katika hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico walikuwa ni 134, kati yao Maaskofu 37 ni wale waliokuwa wanatoka katika nchi jirani hususan Amerika ya Kati na Marekani. Ibada iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu huko Ecatepec, ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya waamini, ikifuatiwa na Misa takatifu iliyoadhimishwa Ciudad Juàrez, Eneo lililoko mpakani kati ya Mexico na Marekani.

Mkutano kati ya Baba Mtakatifu na familia; Ibada ya misa takatifu na wenyeji wa Chiapas ni kati ya matukio ambayo pia yalikuwa na idadi kubwa ya waamini na watu wenye mapenzi mema, bila kusahau mkutano kati ya Baba Mtakatifu na vijana, ambao ni jeuri, utajiri na matumaini ya Mexico. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Mexico limekuwa ni tukio ambalo limefuatiliwa na vyombo vingi vya habari kimataifa. Waandishi wa habari kutoka Mexico na nchi jirani walikuwa ni 4, 077.

Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico linakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko, mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, ameweza kugusa maisha, matumaini, matatizo, changamoto na kutoa matumaini kwa Mexico iliyo bora zaidi, ikiwa kama itafanikiwa kutumia rasilimali watu na utajiri wake kwa ajili ya mchakato wa maendeleo na ustawi wa wananchi wote wa Mexico. Baba Mtakatifu amegusia tatizo la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara haramu ya binadamu na madhara yake katika mafungamano ya kifamilia; amesikitishwa na magenge ya kihalifu yanayokumbatia utamaduni wa kifo; amekemea nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana; amekazia haki msingi za Wahindu wekundu; umaskini na athari zake pamoja na changamoto ya wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amekaza kusema, hija yake ya kichungaji nchini Mexico imekuwa ni tukio lenye mang’amuzi ya kugeuka kwa sura, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kwa wanafunzi wake walioshuhudia utukufu wake, kabla ya kukabiliana na Fumbo la Pasaka. Akiwa nchini Mexico, ameonja imani thabiti ya familia ya Mungu na anawataka kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.