2016-02-24 08:11:00

AMECEA na Caritas katika mapambano dhidi ya Umaskini!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashari na Kati, AMECEA kwa kushirikiana na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kikanda, Caritas, wameamua kwa pamoja kulivalia njuga tatizo la ukosefu wa usawa pamoja na umaskini unaowakabili wananchi wengi wa Afrika Mashariki na Kati. Maamuzi haya yamefikiwa kati ya AMECEA na Wakurugenzi wa Caritas kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanayounda AMECEA, katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni Jijini, Nairobi, Kenya.

AMECEA na Caritas wanasema, wameamua kutekeleza changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika kupambana na umaskini, kwa kushikamana na maskini na kwa ajili ya maskini, kama njia ya kutoa huduma makini kwa Familia ya Mungu. Huduma hii inakwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, huduma za kijamii pamoja na amani huduma ambazo zinapaswa kububujika kutoka katika undani wa mtu.

AMECEA na Caritas wameamua kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, kwa kubadilishana taarifa, ujuzi na mang’amuzi, ilikweli familia ya Mungu Afrika Mashariki iweze kushiriki kikamilifu katika mapambano ya biashara hii inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Biashara hii kwa upande mwingine inafumbatwa pia katika wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi. Wanapenda kushughulikia haki, amani na maridhiano; kwani ukosefu wa tunu hizi msingi katika nchi nyingi za AMECEA kumepelekea makundi makubwa ya wahamiaji.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukaza kwamba, biashara haramu ya binadamu ni uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu! AMECEA na Caritas zinaomba nchi zile ambazo zinatoa hifadhi kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu, kuwahudumia watu wao kwa kuheshimu na kuthamini utu wao kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ili kudumisha haki, amani na utulivu, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuheshimu na kutekeleza sheria za nchi zinazowapatia hifadhi, vinginevyo, itakuwa ni vigumu sana kuweza kusaidiwa kutokana na hofu ya uvunjifu wa sheria za nchi.

AMECEA na Caritas wanasikitika kusema kwamba, sekta ya madini inayoendelea kukua na kupanuka Afrika Mashariki na Kati, haijachangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi husika kutokana na mikataba mibovu inayoyatajirisha makampuni kutoka Nchi za nje na wananchi kubaki wakipata fedha “kiduchu” ikilinganishwa na faida kubwa inayopatikana kutokana na madini. Hapa pia viongozi wa Serikali wanapaswa kuwa makini na mikataba, ili kweli sekta ya madini iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi husika badala ya kuyatajirisha makampuni kutoka ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Kumbe, umefika wakati wa kusimamia ukweli, ili haki iweze kutendeka na Serikali husika kupata kodi inayostahili. Si haki kuona Makampuni ya madini yakiendelea kufaidika na kuacha wananchi wakiwa wanaathirika kutokana na uhalibifu mkubwa wa mazingira baada ya kumalizika kwa shughuli za uvunaji wa madini. Wananchi pia wanahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mafao ya wengi, kwa kuwahusisha wananchi wote na kamwe asiwepo mtu anayetengwa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi, waamini wanapaswa kufundwa barabara ili kutambua na kumwilisha katika medani mbali mbali za maisha yao Mafundisho jamii ya Kanisa.

AMECEA na Caritas wanatambua kwamba, sehemu kubwa ya wananchi wa eneo lao ni vijana, kumbe, hapa kuna haja ya kuwekeza katika utume miongoni mwa vijana pamoja na kuwa na Mfuko maalum ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika Nchi za AMECEA. Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA inapaswa kusimama kidete kukuza na kudumisha haki jamii sanjari na kuwasaidia vijana kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara, ili wasitumiwe na wanasiasa uchwara kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.