2016-02-23 13:18:00

Mchakato wa kufuta adhabu ya kifo Barani Afrika!


Dunia pasi na adhabu ya kifo ndiyo kauli mbiu inayoongoza mkutano wa tisa wa kimataifa unaowashirikisha mawaziri wa sheria kutoka katika nchi 30, wanaokutana mjini Roma kuanzia tarehe 22 - 23 Februari 2016, ili kuangalia uwezekano wa kufuta adhabu ya kifo kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kulinda na kudumisha maisha ya mwanadamu sanjari na kuendelea kufanya maboresho makubwa katika magereza ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao, waweze kurejea na kupokelewa katika jamii wakiwa watu wema zaidi! Baada ya Ulaya, Bara la Afrika linaendelea kuonesha dalili za kutaka kufuta adhabu ya kifo kwa wananchi wake.

Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani akishiriki katika mkutano huu wa kimataifa amekumbusha kwamba, dhana ya huruma ina uso wa binadamu aliyehukumiwa adhabu ya kifo; akathubutu kuwasamehe watesi na wauaji wake. Ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu, Jamii inapaswa kukwepa kishawishi cha kutaka kulipizana kisasi. Adhabu ya kifo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Haki inaambata huruma na kwamba, utekelezaji wa adhabu ya kifo kama sehemu ya mchakato wa kudumisha haki ndani ya jamii ni dhana iliyopitwa na wakati.

Kwa upande wake Michael Masutha, Waziri wa Sheria kutoka Afrika ya Kusini anasema, wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, adhabu ya kifo ilikuwa inatumika kwa ajili ya kuzima machafuko ya kijamii. Kuanzia mwaka 1996 adhabu ya kifo nchini Afrika ya Kusini imefutwa na sasa kipaumbele cha pekee ni zawadi ya maisha inayopaswa kudumishwa na kuendelezwa. Adhabu ya kifo inakwenda kinyume kabisa na haki ya uhai, utu na heshima ya binadamu. Historia inaonesha kwamba, adhabu ya kifo Afrika ya Kusini kama ilivyo pia katika nchi nyingine imekuwa na sura ya ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Naye Joseph Fitzgerald Kamara, mwanasheria mkuu na waziri wa sheria nchini Sierra Leone anasema, Sierra Leone ambaye imepitia katika janga la vita ya wenyewe kwa wenyewe na baadaye ugonjwa wa Ebola ambo pia umefyeka maisha ya watu wengi, lakini ni nchi ambayo inaendelea kukamilisha mchakato wa kufuta adhabu ya kifo, ili kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu katika ujumla wake. Sierra Leone imeridhia itifaki dhidi ya ubaguzi wa wanawake na mateso kwa watu. Inaendelea kutekeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani, ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa. Tangu mwaka 2004, Sierra Leone imeanza mchakato wa kufuta adhabu ya kifo na katika kipindi cha miaka 20 iliyopita hakuna mtu aliyenyongwa hadi kufa baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo! 

Serikali inaendelea kuimarisha utawala wa sheria na uongozi bora sanjari na kuboresha hali ya magereza ili kutoka katika vituo vya mateso na kugeuka kuwa ni mahali pa mafunzo ya tabia. Wafanyakazi katika vyombo vya sheria na haki wamepandishiwa mishahara ili kutenda kwa haki pasi na kuingia katika kishawishi cha kupokea rushwa. Nchini Sierra Leone kumekuwepo na mchakato wa kuimarisha demokrasia na ushiriki wa wananchi kwa kutoa maoni yao kwa vyombo vinavyohusika. Licha ya mafanikio yote haya, bado pia kuna changamoto zinazoendelea kuiandama Serikali ya Sierra Leone, changamoto ambazo zinafanyiwa kazi, ili kuhakikisha kwamba, maboresho ya utawala bora, uongozi bora na demokrasia vinakuzwa na kuendelezwa, sanjari na kulinda usalama na ustawi wa watoto wa Sierra Leone.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.