2016-02-20 15:26:00

Lengo la Liturujia ni utukufu kwa Mungu na ukombozi kwa mwanadamu!


Kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa muhimu sana kwa Kanisa kupitia nyaraka mbali mbali zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuendelea kuzifanyia kazi kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania anachambua maana na umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa.

“‘Maana kwa njia ya liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu’. Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waonyeshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea.

Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utumilifu wa Kristo. Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri Kristo; na kwa njia hiyo inawaonyesha wale walio nje (nalo) Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja, mpaka liwapo zizi moja na mchungaji mmoja (SC 2).

Asili ya neno liturujia ni maneno mawili ya kigiriki :Laos = watu      ergon = kazi. Hivyo neno hilo lilikuwa likitumika kuonyesha :

Lakini Biblia ya Kigiriki (OT) ilitumia neno liturujia kumaanisha: Kumtukuza Mungu. Tuseme kwa ujumla mambo ya ibada.  Katika Agano Jipya limetumika mara 15 kumaanisha Makuhani (mf. Zakaria Lk. 1:23), Walawi na huduma yao,  Sadaka ya Kristo. Wakristo hufanya liturujia, n.k. Katika mafundisho / maandishi ya Kanisa

  1. Kadiri ya Mediator Dei iliyotolewa na Papa Pius XII, Nov. 20, 1947.

Ni adhimisho la hadhara ambamo, Kristo Mkombozi wetu anamtukuza Mungu Baba; pia ni adhimisho la hadhara ambamo Kanisa linamtukuza Kristo, mwanzilishi wake; na kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, Kanisa linamtukuza Mungu Baba. Kifupi ni tendo la kumtukuza Mungu lifanywalo na Mwili wote wa fumbo, yaani Kichwa na mwili.

Hivyo:

  1. Kadiri ya Sacrosanctum Concilium  (Des. 4, 1963)

Ni utekelezaji wa kazi ya kikuhani ya Yesu Kristo. Katika Liturujia, kwa ishara zinazoonekana, huonyeshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na maana ya pekee. Katika Liturujia, ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo, yaani na Kichwa na viungo vyake. Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kile kile na kwa daraja ile ile (SC 7).

Hivyo:

  1. Asili ya liturujia ya Kanisa

Mtaguso wa II wa Vatican unaeleza kuwa liturujia, ambayo yaweza pia kuelezwa kuwa ni mkutano kati ya mtu na Mungu katika Kristo, ndani ya Kanisa katika alama takatifu, ni tendo la hali ya juu sana, na hasa ni kilele cha maisha ya ukristo. Katika kusherehekea mafumbo ya liturujia tunamtukuza Mungu kadiri Mungu mwenyewe anavyotaka. Hivyo inaweza kuelezwa kuwa liturujia: Mungu Baba: Kiini cha liturujia ni Mungu mwenyewe. Mkutano huo kati ya Mungu na mtu ni mkutano kati ya pande mbili zisizo sawa. Ni kati ya Muumba na kiumbe; kati ya Mungu mkamilifu na mtu ambaye anamtegemea Mungu kwa kila kitu. Mungu ndiye anayeanzisha / anayeitisha mkutano huo.

Lengo la liturujia ni utukufu kwa Mungu. Maisha ya binadamu lazima yaelekezwe kumjua Muumba wake. Agano kati ya Mungu na Mwanadamu ni kati ya pande zisizo sawa: Udogo huu wa binadamu mbele ya Mungu huonyeshwa kwa namna binadamu anavyotakiwa kujinyenyekesha mbele ya Mungu kwa kumsifu, kumwomba, n.k. Mungu Mwana ametukomboa: Katika liturujia tunakutana na Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo katika Roho Mtakatifu. Kristo yupo katika maadhimisho ya liturujia yetu kwa namna mbali mbali: Katika Neno lake, Sakramenti, Mwili na Damu, Watumishi na mkutano wa kidini. Kwa namna ya pekee, kwa fumbo la Pasaka Kristo anatupatanisha tena ulimwengu na Mungu. Rejea. Roho Mtakatifu: Hakuna awezaye kusema kuwa Kristo ni Bwana ila kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (IKor 12:3). Ndiye anayetufundisha na kutukumbusha yote aliyosema Kristo (Yoh 14:26).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.