2016-02-19 10:53:00

Utajiri wa Nyaraka za Mtaguso kwa maisha ya kiroho!


Padri Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa, Ijumaa, tarehe 19 Februari 2016 ameanza kutoa farakari za kipindi cha Kwaresima ya maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutafakari kuhusu Tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia, Sacrosanctum Concilium, kwa kujikita katika umuhimu wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa; nafasi ya Roho Mtakatifu katika Liturujia ya Kanisa; umuhimu wa kumwabudu Mungu katika roho pamoja na sala ya maombi. Huu ndio mwelekeo wa kiroho unaofumbatwa katika Tamko la Liturujia.

Tafakari hii imehudhuriwa na Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu. Padre Cantalamessa anafafanua kwamba, maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yamekuwa na umuhimu wa pekee sana katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo cha Mapokeo hai ya Kanisa, yaliyoliwezesha Kanisa kuadhimisha Pentekoste mpya kwa kutambua kwa namna ya pekee dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika Liturujia ya Kanisa, mwaliko wa kusoma na kutafakari tena Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa mwanga wa maisha ya kiroho.

Roho Mtakatifu aliliwezesha Kanisa kuwa na imani na kuliwezesha kutunga Kanuni ya Imani inayofumbata Ufunuo wa Mungu Baba kwa njia ya Kristo Yesu; chachu ya Uinjilishaji mpya, changamoto iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Roho Mtakatifu ana nafasi ya pekee katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwani Mwenyezi Mungu anapewa utukufu na mwanadamu anatakatifuzwa na kwamba, daima Kristo Yesu anajitambulisha na Kanisa lake kwani hiki ni kielelezo cha Ukuhani wa Kristo unaowatakatifuza waamini kwa kutumia alama makini katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani kanisa.

Wadau wakuu katika maadhimisho ya Liturujia ni: Kristo, Roho Mtakatifu na Kanisa kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ni ukweli na uzima na kwamba, Yesu anatekeleza dhamana yake ya Kikuhani katika maisha na kifo chake. Padre ana wajibu wa kusali na kutolea sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo na Roho Mtakatifu; wanaounda Fumbo la Utatu Mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Roho Mtakatifu analitakatifuza Kanisa, ili kuwawezesha waamini kumwabudu Mungu katika roho kwani Roho Mtakatifu analijalia Kanisa maisha mapya, kumbe Liturujia ya kazi ya Mungu anayesali na waja wake kwa njia Roho Mtakatifu na Kristo Yesu. Roho Mtakatifu ni nguvu ya sala inayowaimarisha waamini. Roho Mtakatifu anauhisha sala ya kuabudu kiini cha maadhimisho ya Kiliturujia, kumbe anapaswa kuabudiwa. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kumrudia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, maombi ni sehemu muhimu sana katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kujiombea, kuwaombea walimwengu; watu wenye haki na wadhambi; wazima na wafu; sala hii inawezeshwa na Roho Mtakatifu anayewaimarisha waamini na kuwaombea mbele ya Mwenyezi Mungu sanjari na kuwaunganisha katika imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni Roho Mtakatifu anayewaweka waamini wakfu katika ukweli na Kristo anawaondolea dhambi zao. Hapa mwaliko ni kwa ajili ya kusali na kuwaombea wengine pia. Ni sala inayoonesha uhuru dhidi ya ubinafsi, tayari kuambata utashi wa Mungu, ili wote wawe wamoja! Wakuu wa sala wanawajibu wa kuwambea na kuwatetea watu wao mbele ya Mungu kama alivyofanya Musa kwa Waisraeli.

Kwa njia yake, pamoja naye, na ndani yake wewe Mungu Baba Mwenyezi katika Umoja wa Roho Mtakatifu unapata heshima na utukufu wote, daima na milele. Amina. Na kwa sala hii, Padre Raniero Cantalamessa amehitimisha mahubiri yake ya kwanza kwa kipindi cha Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kujikita katika utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.