2016-02-09 06:55:00

Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka wa Huruma ya Mungu 2016


Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2016 unaongozwa na kauli mbiu “Nataka rehema na wala si sadaka”  (Mt. 9:13). Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: mwaliko wa kumwangalia Bikira Maria, kielelezo cha Kanisa linaloinjilisha kwa sababu limekwisha Injilishwa; Agano kati Mungu na binadamu linajikita katika historia ya huruma ya Mungu na kwamba, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha imani tendaji, ambayo waamini wanaalikwa kuishuhudia kwa namna ya pekee wakati wa kipindi cha Kwaresima.

Baba Mtakatifu anasema katika kipindi cha Kwaresima anawatuma Wamissionari wa huruma  ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia ili kuwaondolea watu dhambi zao, tayari kuingia katika utajiri wa fumbo la imani linalojikita katika huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini wenye vikwazo mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanautumia maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kujipatanisha na Mungu, tayari kuanza safari ya maisha inayojikita katika neema ya Ubatizo na kuendelea kumkazia macho, Kristo Yesu, Kuhani mkuu mwenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu.  

Huu ni muda muafaka wa kusali na kufunga, kutafakari, kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa pamoja na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma. Kwaresima iwe ni fursa ya kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutenga muda wao kwa ajili ya kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kushiriki kikamilifu Sakramenti ya Upatanisho, mchakato wa kugundua safari inayowarudisha waamini katika kugundua maana halisi ya maisha kwa kuguswa na huruma ya Mungu, ili kwa njia ya toba ya kweli, mwamini aweze kupata amani ya ndani.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Kwaresima anakaza kusema Fumbo la huruma ya Mungu limejionesha kwa namna ya pekee katika historia ya maisha ya mwanadamu, hata pale mwanadamu alipokengeuka na kumwasi Mungu, lakini Mungu bado aliendelea kuwa mwaminifu kwa ahadi zake. Yesu Kristo ni huruma ya Mungu iliyofanyika mwili; Sheria inayomwalika binadamu kukumbatia upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza Neno la Mungu na Katekesi ili kujenga mahusiano mema na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumwonjesha upendo na matumaini mapya ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, matendo ya huruma: kiroho na kimwili yatasaidia kuamsha tena dhamiri za waamini ili kwa kuguswa na huruma pamoja na upendo wa Mungu waweze kuonja tena ndani mwao upendo mkamilifu, tayari kuwashirikisha ndugu na jirani zao. Matendo ya huruma ni mchakato unaopania kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha; mambo ambayo Mwenyezi Mungu atayatumia kwa ajili ya kuwahukumu wazima na wafu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa waamini kutafakari na kuyamwilisha matendo ya huruma: kiroho  na kimwili katika uhalisia wa maisha, kwa kumtambua Kristo kuwa yuko kati ya maskini na wale wanaowahudumia. Huu ni mwaliko pia wakuonesha mshikamano na Wakristo wanaoendelea kuuwawa, kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini wawe na ujasiri wa kuona umaskini wa akina Lazaro wanaowazunguka kila siku ya maisha, ili kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuondokana na kiburi na majivuno ya kutaka kujifananisha na Mungu. Uchu wa mali na madaraka ni mambo yanayowafanya watu kushindwa kuwa na sera na mwelekeo sahihi wa maendeleo na kwa nchi tajiri duniani kufunga milango na kuziba masikio ili kutosikiliza kilio cha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa muafaka ya kujikita katika mambo msingi ya maisha ya Kikristo kwa kusikiliza, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha, kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo yanayogusa udhaifu na mapungufu ya kibinadamu kwa kutambua kwamba, mwanadamu ni mdhambi anahitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake. Mwamini atambue kwamba, ni mdhambi na anahitaji kuonjeshwa huruma ya Mungu.

Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” uwasaidie watu wote kutambua kwamba, wanapendwa na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Yeye peke yake ni chemchemi inayozima kiu ya furaha na mapendo kamili. Waamini wawe na ujasiri wa kusikiliza sauti ya Mungu kwa njia ya Neno la Manabii wake, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonesha ushindi dhidi ya dhambi na kifo! Kwaresima anasema Baba Mtakatifu ni kipindi muafaka cha toba na wongofu wa ndani, waamini wanaalikwa kukitumia kwa ukamilifu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.