2016-02-09 14:49:00

Siku 40 za kiti moto Jangwani!


Mahojiano ni mtindo wa mazungumzo ya maswali na majibu. Aina ya mahojiano hutegemea mada husika, kama vile mada ya kisiasa, ya kidini, ya kimahakama au ya kifalsafa ambapo wataalamu wanahojiana maswali na kupeana majibu. Mahojiano haya ya maswali na majibu ya kujieleza huitwa pia kiti moto. Katika Biblia Waisraeli waliwekwa kiti moto na kuzunguka jangwani kwa muda wa miaka arobaini. Hapa duniani binadamu amekalia kiti moto, kwani daima anahojiwa maswali ya maisha yanayodai majibu ya papo kwa papo. Muda wa maisha ya binadamu hapa duniani unafumbwa na namba arobanini, kama isemavyo nahau: “mwizi siku zake arobaini.”

Wakristo tumeanza rasmi kipindi cha siku arobaini, kwa hiyo ni kipindi kinachoakisi maisha ya kiti moto chetu hapa duniani. Katika kipindi anachoishi hapa duniani binadamu huyo anakuwa na mahusiano na vitu mbalimbali, anahusiana na binadamu wenzake, anayo pia mahusiano na Mungu aliyetuumba. Mahusiano hayo yanaweza kuwa mazuri au mabovu. Kwa hiyo maswali ya maisha yamejikita katika mada hii ya mahusiano. Yesu aliishi kama sisi hapa duniani. Siku alipoanza maisha ya hadharani baada ya ubatizo akawekwa kiti moto. Hebu tumfuatilie alivyohojiwa na kutoa majibu ili kutusaidia sisi kujibu maswali ya mada hii ya mahusiano katika maisha yetu tukianza na kipindi hiki cha Kwaresima.

Mahojiano ya Yesu juu ya mada hii ya mahusiano yameandikwa na Mwinjili Marko kwa kifupi sana tena bila maelezo kwamba: “Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani;” (Mk. 1:12-13). Katika aya hizi mbili, tunapata picha ya mang’amuzi ya mahusiano ya kibiblia, pale waisraeli jangwani walipowekwa kiti moto kwa miaka arobaini. Muda huo unawakilishwa kwa siku arobaini za maisha ya Yesu hapa duniani. Wainjili Mateo na Luka wanalipanua wazo hilo la Marko na kulitengenezea katekesi na kuliwakilisha kwa mtindo wa mifano mitatu ya maswali na majibu anayoweza kuulizwa kila mmoja wetu katika maisha yake. Maswali hayo yamejikita katika mada ihusuyo mahusiano kati ya mtu na vitu au mali, na watu, halafu na Mungu.

Nyanja hizi tatu za mahusiano ndiyo mada kuu ya kiti moto alichowekwa Yesu na shetani baada ya ubatizo, hasahasa mara baada ya kusikika sauti iliyomtangaza kuwa yu Mwana mpendwa wa Mungu, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa niliyependezwa naye. Msikilizeni yeye.” Shetani anaonesha umahili wake wa kuuliza maswali katika mahojiano hayo. Mara moja Yesu anapotangazwa kuwa ni mwana mpendwa wa Mungu, naye anaonesha kukiri kuwa Yesu ni kweli mwana wa Mungu. Kutoka hapo naye anatoa mapendekezo yake ili kuthibitisha ukweli huo, kisha anauliza swali.

Pendekezo la kwanza lahusu mahusiano na vitu. “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.” Pendekezo hili ni zuri kabisa. Ni kweli kwamba Mungu anataka watoto wake waishi vizuri hapa duniani. Watoto wapate chakula na wastawi wasikose chochote. Kwa hiyo, pendekezo hili linamtaka Yesu  aliye Mwana mpendwa wa Mungu aachilie mbali mambo mengine na ajitikite katika kuwatekelezea watu hitaji hilo la msingi. Tendo hili la kula linatokea mara mia tisa na kumi katika Agano la kale, na mara nyingi zaidi katika Agano jipya. Kwa hiyo kula na kuwashibisha wenye njaa ni jambo muhimu. Aidha, siku ya hukumu Yesu hatutahukumiwa kutokana na kusali, bali tutapimwa kama tuliwapa chakula wenye njaa, na maji walio na kiu, na tumewavika walio uchi, na kuwapa makao wasio na nyumba. Kwa hiyo, Yesu anapendekezewa jambo jema kuwa: “Wewe wekeza nguvu zako kwenye kuzalisha chakula, kwani hilo ndilo hitaji muhimu la binadamu.” Yesu anajibu: “Imeandikwa, mtu haishi kwa mkate tu.” Yesu hapingi kuwajibika na kutosheleza mahitaji ya kimwili, lakini hicho siyo chakula pekee kinachotosheleza maisha ya kibadamu, bali yako maisha ya kiroho, maisha ya kimungu, maisha ya kiutu yanayofanana na uso wa Mungu unaaonekana katika mwana mpendwa.

Mbegu ya maisha ni upendo, na chakula kinachokuza maisha hayo ya upendo ni Injili ya Kristu. Kishawishi hiki kinatupumbaza bila wenyewe kujitambua kwa kujizamisha katika maisha ya kibaolojia tu. Wakati mwingine tunatumia hata dini kwa kuomba neema kusudi maisha yatuendee vizuri. Mapato yake tunajilundikia mali nyingi kwa ajili ya maisha. Kumbe katika swali hili tunaalikwa kutafakari na kutambua kuwa kuna jambo muhimu zaidi ya mkate na chakula cha ulimwengu huu.

Pendekezo la pili linahusu mahusiano na watu, hasahasa ya kuwa na mamlaka na ukuu juu ya wengine. Ndiyo maana shetani anamwongoza Yesu juu na kumwonyesha ufalme wote wa duniani na kumwambia: “Ulimwengu wote uko mikononi mwangu, nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, Basi wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.”  Kama ilivyokuwa kwa Yesu, Mungu ameweka ndani ya kila mmoja wetu msukumo wa kuwa mkuu, wa kufanya jambo kubwa na kulionesha mbele ya watu na kutufanya tujisikie tumefaulu katika maisha.

Mwovu anapendekeza namna nzuri ya kuwa mkuu ndiyo maana anampandisha Yesu juu ili ajisikie mkuu. Hivi ndivyo watu wanaotaka kuonekana wakuu wanavyopanda juu. Tena wanapopanda juu wanaweza kutumia kila mbinu, ikiwa ni pamoja na kukanyaga migongo ya wengine, kutumia mabavu, kulaghai, kula rushwa, kudhulumu wanyonge nk, hivi ndivyo walivyofanya na wanavyoendelea kufanya wakuu wa hapa duniani. Kwa hiyo mwovu anamdokezea Yesu ukuu kadiri ya vigezo hivyo vya ulimwengu huu na kumsujudu mwovu.

Haina maana ya kumpigia magoti, na kuinama kichwa, bali ni kukubali mapendekezo yake. Yesu akamjibu: “Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake,” yaani kuinama kichwa na kupokea mapendekezo ya Mungu, kwani mbele ya Mungu, kuwa mkuu maana yake ni kushuka, “Ajishushaye atakweza.” Yesu alikuwa mkuu kwa kujishusha hadi akasema: “mimi niko kati yenu kama mtumishi.” Kuwa na fikra za Kristo aliyekuwa mkuu maana yake kujinyenyekea hadi kufa Msalabani.

Pendekezo la tatu ni la mahusiano na Mungu. “Mwovu akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu akamwambia, ‘Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini.’” Ama kweli binadamu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Katika pendekezo hili mwovu ananukuu hata zaburi: “Kwa kuwa atakuagizia malaika zake, wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” (Zab 91:11-13). Pendekezo hili linamhoji Mungu kama kweli ananipenda au sivyo. Kama Mungu ananipenda basi atanitunza, atanipa neema na kunifanyia upendeleo pekee hata kwa muujiza. Pendekezo na kishawishi hiki kinakuja kirahisi hasa kwa watoto waliojiaminisha kwake, kama wale wale wanaojisikia kuwa ni wakristu hodari au watawa safi, Makatekista hodari. Hapo Mungu hana budi atukirimie kila tunapomwomba.

Kadhalika na Malaika wanaotajwa hapa, hao ni kama wajumbe wanaotusaidia kwa njia ya maombezi yao. Athari yake ni kwamba endapo kuna mgonjwa anayeumwa sana, huyo anawaomba watawa, mapadre au hata vikundi vya kikarismatiki ili wamwombee. Itakapotokea mgonjwa huyo anakufa, hapo watu haohao wanaanza kuhojij: “Hivi dini ina faida gani? Hawa watawa na mapadre wanafanya kazi gani?” Kishawishi hiki unakiona pia kwa wale wenye mazoea ya kutegemea ibada mbalimbali, au masalia ya watakatifu  au medali nyingi, au wale wanaofurika kwenye mikusanyiko ya sala za uponyaji, hawa ni watu wanaotaka kuonesh ”suprise ya muujiza ili wapate kuamini”. Hiki ndicho kishawishi cha kumdai Mungu afanye muujiza. Vitu hivyo ni njia mojawapo ya kummiliki na kumbinafsisha Mungu, na kumfanya awe mtumishi wetu, yaani atutumikie sisi kadiri tunavyotaka. Hatari yake ni kugeuza dini kuwa ibada ya ushirikina na mazingaombwe.

Jibu la Yesu: “Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako,” yaani usitie shaka juu ya uwezo wa Mungu, ingawaje kwa nje unaweza kuona tofauti. Yesu mwenyewe hakuona mashaka juu ya Mungu hata katika majaribu makali ya maisha. Tusitegemee kutendewa tofauti na vile alivyomtendea mwanae aliyependezwa naye. Kila mahali tunapotaka kuepushwa na maovu, katika maumivu yabidi kusali na kulinganisha maisha hayo na mapenzi ya Mungu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.