2016-02-06 16:56:00

Useja ni zawadi inayopokelewa, inatunzwa na kudumishwa!


Useja wa Kipadre ni hija ya uhuru, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza kongamano lililoandaliwa na Chuo kikuu cha Kipapa la Gregorian kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 6 Februari 2016 kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa, walezi na wanasaikolojia, wanaojikita zaidi katika majiundo makini na endelevu ya Wakleri ili kuwasaidia kujisadaka zaidi kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani pasi na vizuizi vya kifamilia.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika tafakari yake ya kufunga kongamano hili la kimataifa Jumamosi, tarehe 6 Februari 2016 amekazia zaidi kuhusu useja kama hija ya uhuru unaojikita katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, unaoambata neema na huruma ya Mungu pamoja na kutambua changamoto na magumu wanayoweza kukabiliana nayo Wakleri katika maisha yao ya useja. Daima wakumbuke kwamba, wako kwenye mapambano makali yanayowataka kuwa macho na vishawishi vya dunia hii. Uhuru wao unapaswa kujionesha katika sadaka na majitoleo ya kila siku, yanayopyaishwa kwa njia ya sala, tafakari na huduma makini, kwa kutambua kwamba, huu ni uamuzi uliofanywa kwa uhuru kamili na udumu maisha yote kwa kumwambata Kristo aliyekuwa fukara, mseja na mtii!

Kardinali Parolin anawakumbusha Wakleri kwamba, wao ni Kristo mwingine, wanapaswa kupata utambulisho wao katika maisha na utume wa Kristo, ili kuendelea kufuata nyayo zake, kwani anaitwa, anatakaswa na kutumwa kushiriki kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni mtu anayetueliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu. Kumbe, useja ni wito kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa.

Useja kama wito unapaswa kugunduliwa, kupokelewa na kutunzwa kwa imani na uaminifu mkubwa, kama ile changamoto iliyotolewa na Yesu Mwenyewe kwa Mtume Petro alipomwambia kutweka hadi kilindini, akitambua uzoefu na mang’amuzi yake katika suala zima la uvuvi, lakini Petro akamjibu Yesu, kwa neno lako, nitashusha nyavu zangu! Wakleri wakuze fadhila na wito wa useja kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na ndugu pamoja na majirani zao; hawa ni wale wanaounda familia na udugu wa kisakramenti. Ni watu wanaoadhimisha mafumbo ya Kanisa, kusali na kutafakari kwa pamoja, huku wakishrikishana hazina ya maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Udugu huu unapaswa kusimikwa katika huruma na mapendo; umoja na mshikamano ili kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema useja umewekwa mahususi na Kristo kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kwa kuwapenda wote katika Yesu bila ya kuwa na mahusiano fungamanishi ni mtu awaye yote! Hiki ni kielelezo cha upendo unaoonesha uhuru na ukomavu kwa ajili ya huduma. Tasaufi ya useja ina mwelekeo chanya katika maisha ya wakleri na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu. Useja ni zawadi inayopaswa kupokelewa kwa moyo mkuu, kutunzwa kwa uaminifu na kuendelea kudumishwa kwa furaha na matumaini katika hija ya maisha ya wakleri hadi pale watakapoituma mkono dunia. Pale wanapoanguka na kukengeuka, wapige moyo konde na kusimama, tayari kumkimbilia Kristo Yesu, ili aweze kuwaganga na kuwanyanyua tena katika safari hii yenye changamoto nyingi katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.