2016-02-06 16:46:00

Mwaka wa huruma ya Mungu nchini Cuba: Kipaumbele ni wafungwa!


Askofu Jorge Enrique Serpa wa Jimbo Katoliki la Pinar del Rio, nchini Cuba anasema, kuna idadi kubwa ya wananchi ambao wamefungwa magerezani. Baadhi yao ni wafungwa wa kisiasa ambao wamefungwa kwa miaka mingi. Kanisa Katoliki nchini Cuba, linaiomba Serikali ya Cuba wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kuangalia kesi zao na pale inapowezekana kuwapatia msamaha. Askofu Serpa anakiri kwamba, kuna kundi kubwa la wafungwa ambao wamefungwa kutokana na makosa ya jinai, rushwa na ufisadi. Kanisa katika shughuli na mikakati yake ya kichungaji linapaswa kuwasikiliza kwa makini watu hawa, ili kuwapatia nafasi ya kuanza kuandika tena kurasa mpya za maisha yao wanapomaliza adhabu zao magerezani.

Kwa bahati mbaya hawa ni watu wanaosahaulika, lakini wanapaswa kuonjeshwa upendo na huruma ya Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake wanaotaka kutubu na kumwongokea, ili kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Ili kuhakikisha kwamba, utume wa Kanisa Magerezani unaendelea kama sehemu ya umwilishaji wa matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu; mara moja kila mwezi, Askofu Serpa anahakikisha kwamba, anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafungwa na askari magereza, ili kuwaonjesha huruma na mapendo ya Mungu yanayovuka hata kuta za Magereza.

Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linataka kwa namna ya pekee kabisa, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maadhimisho haya katika magereza nchini Cuba; ili kuwaonjesha uhuru wa wana wa Mungu mahali popote pale walipo! Itakumbukwa kwamba, hata wafungwa magerezani wanaweza kupata rehema kamili ikiwa kama watatekeleza masharti yanayotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea nchini Cuba akiwa njiani kuelekea Marekani, aliwakumbusha waamini nchini Cuba kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anapania daima kuwanyanyua juu kabisa ili utu na heshima yao iweze kulindwa na kuthaminiwa na wengi. Hata kama wafungwa hawa wako magerezani bado ni sehemu ya Familia ya Mungu inayoteseka na kwamba, hawajatengwa hata kidogo, ndiyo maana Mama Kanisa anataka kuendelea kushikamana nao, ili kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.