2016-02-05 17:13:00

Yaliyojiri Jimbo kuu la Dodoma wakati wa kufunga Mwaka wa Watawa Duniani


Maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Watawa Duniani imekuwa ni fursa kwa watawa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kujikita katika mambo msingi ya maisha, wito na utume wa kitawa ndani ya Kanisa. Watawa wanahimizwa kujitosa kikamilifu katika bahari ya upendo wa Mungu, ili waendelee kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wao miongoni mwa familia ya Mungu. Watawa wawe ni watu wa shukrani kwa Mungu kutokana na hazina ya wito waliokirimiwa na Mungu, tayari kutumia neema hii kwa ajili ya kujenga madaraja ya watu kukutana.

Hizi ni kati ya changamoto ambazo, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma amewashirikisha watawa wa mashirika mbali mbali wanaotekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Dodoma, wakati wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani katika ngazi ya Kijimbo. Watawa wametakiwa kukuza na kudumisha mambo yanayowaweka karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari, Sakramenti na huduma makini, kielelezo cha karama na huruma ya Mungu inayomwilishwa kati ya watu wake. Watawa wawe na ujasiri wa kumfuasa Kristo aliyetolewa sadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Watawa wawe waaminifu kwa karama, sheria na mashauri ya Kiinjili, kielelezo makini cha ushuhuda wa maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Watawa wayaishi mashauri haya kwa kina pasi na kubabaisha kwani ndivyo inavyompendeza Mungu na binadamu. Askofu mkuu Kinyaiya amewashukuru na kuwapongeza watawa kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Wawe na ujasiri wa kuendelea kutafakari karama za mashirika yao, tayari kusoma alama za nyakati, ili kuzimwilisha karama hizi ambazo ni zawadi kubwa ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa lake.

Ulimwengu mamboleo una shida na changamoto zake, kumbe watawa wawe makini kuziona changamoto na shida hizi, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, amani na matumaini kwa wale waliokata tamaa. Jumuiya za kitawa ziwe ni shule ya upendo, umoja na udugu kwa kusaidiana na kusumbukiana kwa hali na mali; tayari kumtumikia Mungu na jirani pasi na makunyanzi.

Wakati huo huo, Padre Egidius Seneda, Katibu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania amewataka wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu Jimbo kuu la Dodoma kuwa na malengo makini katika maisha; kwa kumshirikisha Mungu katika vipaumbele na matarajio yao kwani Mungu ndiye asili ya wema na utakatifu wa maisha. Wawe makini katika kutumia rasilimali na utajiri ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi.

Wanafunzi wakiwa Chuoni wahakikishe kwamba, masomo yanapewa kipaumbele cha kwanza ili kuwajengea stadi, ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kuwahudumia watanzania kwa weledi na majitoleo makuu. Wanafunzi wajifunze pia kuwa na moyo wa shukrani kwa fursa mbali mbali ambazo wanajaliwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Na habari nyingine kutoka Jimbo kuu la Dodoma inasema, Familia ya Mungu nchini Tanzania inapaswa kushirikiana kwa dhati, ili kusimama kidete katika kulinda tunu msingi za maisha ya binadamu: kiroho na kimwili; kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bila fadhila ya utii, unyenyekevu, upendo na imani, taifa linaweza kuzama katika maafa na utepetevu wa misingi bora ya maisha.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Padre Atilio Mnyenyelwa kutoka Jimbo kuu la Dodoma wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Kitaifa kwa ajili ya kuiombea Tanzania, lililoadhimishwa hivi karibuni mjini Dodoma. Wakristo wanapaswa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili aweze kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu wao anayewaongoza na kuwanesha dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Wakristo wawe na ujasiri wa kumshirikisha Mungu katika mipango ya maisha yao, ili kupata baraka. Watambue kwamba, kazi ya Mungu haitaki ubinafsi, uchoyo au majigambo, bali utii, unyenyekevu na huduma ya mapendo.

Na Rodrick Minja,

Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.