2016-02-04 16:11:00

Leo wavuvi meno yote nje! Wamekutana na kiboko yao!


Dili ni tenda au shughuli yoyote inayolipa au inayoleta faida kubwa kwa haraka. Mathalani, tajiri akikuomba umtafutie mteja wa kununua nyumba yake, na akakuahidi kukukatia robo ya gharama ya manunuzi, basi dili hilo linalipa. Lakini kuna dili nyingine hazilipi. Leo tutaliona dili au tenda iliyotaka kuwaingiza watu mkenge. Madhari ya dili hilo yalikuwa ziwani, likiwahusisha wavuvi maarufu walioisha hangaika kuvua samaki usiku kucha wasipate hata dagaa. Ikawa mchana walipokuwa wanaosha nyavu, akatokea kijana mmoja akawapa dili la kuingia tena majini kuvua samaki waliowakosa usiku. Hapo wavuvi meno yoote nje! Ama kweli hili ni dili na kukata na shoka, si tena 10%

Jina asilia ya ziwa hilo ni Kinneret, lakini baadaye likaja kujulikana kwa majina matatu: Mosi, Galilea kutokana na mkoa uitwao hivyo. Pili, Tiberias kutokana na mtawala wa Kirumi aitwaye Tiberius. Tatu, Genezareti jina la sehemu ya magharibi ya ziwa hilo. Ziwa halikuwa kubwa sana, lakini linaoneshwa kuwa ni kubwa na lina kina kirefu hadi likaitwa bahari. Kadhalika ziwa hilo ni tulivu lakini linapewa sifa nyini za kutisha kwa mawimbi makali yanayoweza kuwachefua na kuwazamisha wasafiri.

Maji ya ziwa la Genezareti ni matamu siyo maji-chumvi na lina samaki wengi. Hivi wakazi wake wanajikimu kwa uvuvi. Vijiji na miji mikubwa ilkiyochangamka iliibuka pembeni mwa ziwa hilo kutokana na biashara ya samaki na utalii. Miji hiyo ni Bethsaida ulio kaskazini mwa ziwa unakoingia mto Yordan. Wavuvi watano walitokea huko kama vile Petro pamoja na mdogo wake Andrea, halafu Filipo, kisha Yakobo na Yohane pamoja na baba yao mzee Zebedayo. Mji wa Kafarnaumu alikoishi Yesu kwa miaka mitatu pindi anahubiri. Yesu alikaa nyumbani kwa Petro kwa vile baada ya Petro kufunga ndoa, alihama nyumbani kwake Betsaida na kufika kufanya makazi Kafarnaum kufanya kazi ya uvuvi inayolipa. Wavuvi wakibahatika kuvua samaki wengi usiku, asubuhi baada ya kuosha nyavu, walizipeleka kutia chumvi na kuzikausha katika kijiji cha Magdala alikozaliwa Maria Magdalena. Hivi Magdala kiliitwa kuwa kijiji cha wavuvi au Thalikeia maana yake mahali pa kukaushia samaki. Halafu mji wa Tiberia ulioko kusini ya Magdala. Mji huu ulijengwa na mfalme Herode Antipa, huko aliishi pamoja na Herodia. Kuna vijiji vingine viliyo mbali na ziwa kama vile Nazareti (alikolelewa Yesu). 

Halafu mji Sefforis uliojengwa awali na Herode Antipas kabla ya kuhamia Tiberia. Kisha kuna kijiji cha Kana kinachojulikana kwa sherehe ile ya ndoa. Baada ya kuona mandhari hii, sasa tuwaone walengwa wa dili tutakaloliona, tukiongozwa na fasuli ya Injili: “Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka wanaosha nyavu zao.” Hapa yanajipambanua makundi mawili ya watu waliokuwa kando ya ziwa: Kundi la kwanza ni makutano ya watu wengi wakimsonga Yesu wakilisikiliza neno la Mungu alilolihubiri. Yaonekana neno la Yesu lilikuwa muhimu na lilimvuta kila mtu, ndiyo maana,“ walimsonga kusikiliza.”

Kundi la pili ni la wavuvi:“Yesu akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka wanaosha nyavu zao.” Wavuvi walikuwa wamezama katika shughuli yao inayodai uvumilivu na utulivu. Yesu alipomaliza kuongea na kundi la kwanza, akawageukia wale wavuvi, na “akaingia katika chombo kimoja, cha Simoni.” Neno lililotumika hapa siyo “kupanda au kukwea chomboni” bali neno la kigiriki embas lenye maana ya kuingia chomboni. Halafu neno chombo au mashua katika nafasi hii humaanisha maisha ya mtu. Kwa hiyo Injili au Yesu mwenyewe anaingia katika maisha ya mtu, na huyo mtu anakuwa kiini cha ujumbe wa Yesu. Mtu huyo anakuwa moja kwa moja dili na mradi wa kutangaza ulimwengu mpya.

Baada ya kuingia chomboni “Yesu akamwomba Simoni akipeleke chombo mbali kidogo na pwani.” Yesu hatoi amri bali anamwomba Petro kujitenga kidogo na pwani, badala ya Simoni kumwomba Yesu kama alivyofanya alipomponya mkwe wake. Kisha Yesu “akaketi akawafundisha makutano ali chomboni.” Mtu aliyeketi hutoa fundisho muhimu na la kueleweka ndivyo afanyavyo Yesu anahubiri akiwa katika chombo cha Petro. Mashua aliyoingia Yesu ni picha ya maisha ya Jumuiya ya Kikristo, ndanimo kunatoka ujumbe wa mwalimu. Aidha, ujumbe wa Injili ni tofauti na kelele nyingine kama mawimbi ya bahari, kelele kama zinazosikika kwenye “magazeti, matelevisheni, mawatsapp, ma fesibuku, mayutubu, nk”.

Yesu alipokwisha kunena alimwomba tena Simoni, “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” Yesu anamwomba Petro kufanya mambo ambayo kadiri ya akili ya kawaida ya mang’amuzi ya uvuvi ni upuuzi na kupotezeana muda licha ya kuhatarisha maisha na kusabisha kuchekwa. Lakini Petro anaona “yewala si utumwa.” Lakini kabla ya kushika tenda hiyo anaona amweleze Yesu hali halisi: “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu;” lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Yaani suala zima la kurudi kuvua samaki majira ya mchana halina mantiki yoyote, lakini kwa vile umeagiza wewe basi mimi ninajitosa. Kwa maneno mengine Petro anataka kusema kuwa: “Dili hili halilipi, na kama angesema mtu mwingine ningemcheka tu. Lakini kwa vile tenda ni yako mimi nitatii bila wasiwasi.” Maana yake, neno la Bwana ni muhimu zaidi kuliko akili na mang’amuzi ya kitaalamu aliyo nayo mtu.

Wakristo tunaalikwa kujiaminisha daima kwa neno la Yesu na siyo kufuata maoni yetu, au kufuata ushauri wa kitaalamu na wenye mantiki ya kiakili. Kufuata Neno la Kristo kunataka kuwa na imani kuu, hata kama inaweza kunisababishia kupata fedheha na kuchekwa na ulimwengu.Mapato ya kumtii Yesu yanakuwa makubwa na ya kushangaza kwani “walipata samaki wengi mno.” Halafu, “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” Hapa haimaanishi kwamba Petro ni mdhambi, la hasha, bali anatambua na kukiri kwamba kuna tofauti kubwa kati ya neno la Yesu na fikra au mantiki ya kibinadamu, kama anavyotuambia Mungu: “Maana mawazo yangu siyo mawazo yenu” (Isaya 55:8)

Kisha Yesu anamwambia Simoni “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.” Neno la kigiriki lenye maana ya kuvua ni aliyeuein kumbe hapa limetumika neno zoogron na tendo lake ni zoogrein, maana yake ni kuleta maisha, kuleta uzima, yaani kuwafanya binadamu wawe hai na wazima kweli, kuwapa uhuru au lembuka ya bure. Kwa hiyo kazi ya wanafunzi ni ile ya Yesu mwenyewe. Petro alikuwa ametolewa toka majini alikozamaishwa na mawimbi – dhambi – wakati akitaka kutembea juu ya maji, lakini kutokana na kujiaminisha kwa Yesu, anapata utume wa kuwapa uhai wengine waliozamishwa kilindini na mawimbi ya bahari. Wavu pekee utakaowavua watu toka kilindini ni neno la Injili ya Yesu.

Ukitupa nyavu hizo kilindini utafaulu kuwavua waliokandamizwa na mawimbi ya maisha, kwani wavu una nguvu za kimungu aliyeagiza na kusema: “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” Watu hao wanapovuliwa na Neno la Yesu wanaweza kutolewa nje ya maovu na tabu zao za kukandamizwa huko kilindini mwa mateso. Kazi hiyo ya kuvua au ya kutangaza Neno la Yesu ni ya kila mmoja wetu. Mapato yake wavuvi “walipokwisha kuviegesha Pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.”

Katika maisha hatuwezi kupotea kama tunamfuata Yesu, kwani katika Yesu maisha yetu yanapata maana nyingine, unakuwa mtu mwingine kabisa. Kwa hiyo dili la Yesu linalipa na hupita akili na utaalamu wetu.

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.