2016-02-02 16:00:00

Watawa wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha!


Kanisa tunaadhimisha Sikukuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, ambapo katika tukio hili pia tunaadhimisha Huruma ya Mungu ya zawadi na kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Hii ni Siku ya neema na baraka kwa watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanapojiunga pamoja ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwekwa wakfu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

JAMBO LA KWANZA LA KUTANGULIZA:

Adhimisho la kutolewa Bwana hekaluni, asili yake ni agizo la Mungu kwa wanawaisraeli kutolea watoto wao wazaliwa wa kwanza kwa Bwana Mungu, baada ya Yeye Mungu kuwakinga watoto hao wa kwanza wasiuawe kama walivyouawa watoto wa kwanza wa wamisri, kutokana na kiburi cha Mfalme Farao kutowaruhusu waisraeli waondoke nchini Misri na kwenda kumwabudu na kumtumikia Mungu wao katika nchi ya ahadi ya Kanaani(Kut.13:1-2).

Wazazi wa Yesu, Maria Mtakatifu na Yosefu Mwenyeheri walitimiza agizo hilo la Mungu kwa kumpeleka mtoto wao Yesu ili mtoto wao awe wa Bwana (Lk.2:22-24). Katika kutumiza wajibu huu wa sheria ya Bwana wazazi hawa walikutana na mzee Simeoni ambaye alitambua kwamba mtoto Yesu atakuwa Nuru ya kuyaangazia mataifa. Kristo kweli ni Mwanga wa ulimwengu. Anaiangaza mioyo ya watu na kuijaza uzima wake. Mwanga huu wa Kristo watu wote tunaomwamini Kristo tumeupokea katika Sakramenti ya ubatizo kwa kupewa mwaliko wa wito wa maisha ya utakatifu, kama Mungu wetu alivyo Mtakatifu.

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, kwa kuona uzito na umuhimu wa tukio la kutolewa Bwana Hekaluni, aliamua kuitangaza siku hii ya tarehe Mbili mwezi Februari kuwa ni siku kila mwaka ya kuadhimisha maisha ya wakfu na utawa katika Kanisa. Maisha ya wakfu na utawa ni matokeo ya matunda ya kuishi tunu ya zawadi ya Sakramenti ya ubatizo. Maisha ya wakfu na utawa ni furaha ya kujitoa upya kwa Bwana baada ya kuondolewa si katika utumwa wa Mfalme Farao wa Misri, bali ni furaha ya kujitoa upya kwa Bwana baada ya zawadi ya Sakramenti ya Ubatizo, ubatizo uliotutoa katika utumwa wa dhambi na kifo.

Uwanawakfu na utawa ni kujitoa tena kwa Mungu baada ya kusikia Bwana anatuita kwa namna ya pekee kwa ajili yakushuhudia makuu ya mapendo yake, kamawalivyoitwa kwa namna ya pekee taifa teule la Israeli ili kushuhudia makuu ya upendo wa Mungu kwao na upendo huo kudhihirishwa kwa watu wote ili wamjue Yeye Mungu kwa kupitia taifa lake teule. Baba Mtakatifu Francisko kwa hati yake ya Injili ya furaha na kwa adhimisho la mwaka wa wanawakfu na watawa anatualika wanawakfu na watawa wote kuadhimisha zawadi ya furaha ya KUITWA NA KUTEULIWA NA MUNGU kwa maisha ya wakfu na utawa katika Kanisa.

Jambo la pili muhimu la kushika vizuri ni kwamba maisha ya wakfu na utawa ni kushiriki furaha itokanayo na kuitwa na Mungu kadiri ya karama ya waanzilishi wetu. Asili ya maisha ya wakfu na utawa katika kanisa ni kazi ya Mungu mwenyewe anayeendelea kujifunua kwa watu wake kadiri ya wakati kwa utendaji wa ROHO MATAKATIFU. Maisha ya wakfu na utawa ni WITO ambao wanawakfu/watawa tuanasikia sauti inayoongea nasi. Ni kama alivyosikia Musa Mtumishi wa Mungu, mwana wa taifa teule la Israeli alipokuwa anachunga kondoo wa baba mkwe wake Yethro kuhani wa midiani(Kut.3:1-3). Musa anaitwa licha ya alivyo na mazingira aliyopo ili Mungu adhihilishe uwezo wake, upendo wake na huruma yake kwa watu wake. Maisha ya wakfu/utawa ni wito wa sauti ya pekee ya Mungu kwa mtu husika kwa nafsi yake ayashiriki mapendo ya pekee ya Mungu anayoyapata mtu husika kwa huruma tu kwake binafsi, na kwa huruma tu na mapendo yake Mungu kwa ajili ya taifa la Mungu, kwa yeye mwanawakfu/mtawa kushirikishwa kazi na utume wa pekee ambao Mungu anataka kutenda kwa kumshirikisha mtu husika. Mwito huu wa Mungu humtaka mtu husika akubali kusikiliza na apende na atake kusikiliza kwani Mungu anataka siku kwa siku kuendelea kuongea na anayemwita, hususani hapa mwanawakfu/mtawa, kama kwa mfano mzuri vile Mungu alivyokuwa anaongea siku kwa siku na Musa ili kufanikisha lengo la kuitwa kwake.

Zawadi hii ilianzia kwa mababa wa Imani, manabii wote na hasa kama ilivyoelezwa awali wazi kabisa katika nafsi ya Musa ili kudhihirisha matendo makuu ya Mungu anayeokoa watu wake. Matendo ya mfano yaliyofanywa kwa ISHARA na Musa, YAMEKUWA YA KWELI NA HAKIKA yakijirudia tena kwetu SASA baada ya TUKIO LA YESU KRISTO kuja, kuteseka, kufufuka, kupaa mbinguni na kumpeleka Roho Mtakatifu ndani ya waanzilishi wa mashirika ya wakfu na utawa, kwao wao waanzilishi moja mmoja na baadaye sasa kwa kila mwanawakfu na mtawa binafsi.

Ni Mungu anayeongea nasi na kutuomba wanawakfu na watawa wote kwa kupitia MAANDIKO MATAKATIFU, ambamo tunamkuta NENO WA MUNGU anayeongea kwa nyakati zote na kila mmoja, kwa kupitia matukio mbalimbali ya maisha yetu, kwa kupitia nafasi za kututana naye kwa sala, kwa kupitia huduma takatifu za masakramenti na huduma za utume wetu. Katika hayo yote YEYE anatuambia TUMTAZAME USO WAKE TOKA NDANI KABISA YA MIOYO YETU. Atualika tumwangalie Yeye kwani Yeye anatutegemeza na kututegemea katika KUSHUHUDIA UPENDO WAKE KWETU NA KWA WATU WAKE.

Baba Mtakatifu Francisko ametukumbusha hili kwa kutupa fulsa hii ya adhimisho la Mwaka wa Wanawakfu/Watawa akituambia kwa himizo na msisitizo katika hati yake ya Injili ya furaha, Baba Mtakatifu anasema kwamba ”Mungu kwa kuwaiteni ninyi anawaambieni: ‘Ninyi ni muhimu kwangu, nawapenda, nawategemea. Yesu anasema haya kwa kila mmoja wetu! Furaha inazaliwa katika hili! Ni furaha inayotokana na pale Yesu anaponiangalia mimi. Kuelewa, kusikia na kulijua hili ndiyo siri ya furaha yetu. Kujisikia napendwa na Mungu, kujisia kwamba kwa Yeye Mungu sisi si ilimradi idadi yetu bali tu watu wake na ndiye Yeye anayetuita.

Mzaburi namba 139:14 anasema “Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu!” Mzaburi anawakilisha maelezo ya shukrani na upendo wa huruma yake Mungu kwetu wanawakfu/watawa katika kuitwa kwetu licha ya asili tutokayo, namna tulivyo na shirika tulilopo. Maneno ya Mzaburi yatuletee maana na uzuri katika maisha yetu. Roho Mtakatifu ni tajiri wa kuita awatakao kwa ajili ya Kristo na ni mwingi wa Utajiri wa Karama kwa mtindo uliomwingi wa mashirika ya wakfu na utawa, kwa ajili ya kazi ya pekee katika kanisa na jamii. Wajibu wetu tujipokee wenyewe kama tulivyo na kujifunua kwa zawadi ya neema ya huruma ya Mungu tukifanyika bora zaidi ili tuende tukitenda kadiri yak arama na utume tulioitiwa kama mashirika na kadiri ya mashirika yetu na tukujibidiisha kuinjilishwa na utume tuufanyao.

Tuamini kwamba, huduma ya kweli, ya juu na iliyotukuka tunayoitoa kwa kumpenda mungu aliyetuita; na kwa ajili ya uteule wetu kwa ajili ya utume tuliopewa kwa ajili ya watu wake ni muhimu ili kudhihirisha hadhi wapayo mungu watu wake kwa kupitia sisi! Maisha yetu wanawakfu/watawa yatafikia kipeo hiki kama tutaendelea kukutana na Mungu katika FUMBO LA SALA ambamo ndimo tunaendelea sana kuisikia sauti ya Mungu, kumtukuza, kumshukuru, kumtafakari na humo kujibidiisha kuyajua mapenzi yake kwetu. Wito wa kumsikia Mungu na kumwitikia katika kushika amri zake, kwa kuishi mashauri ya Injili na kujikuza katika fadhila za kikristo ni msingi wa kufurahia wito wetu wa kutakasika, kutakatifuzika na kuishi kadiri ya karama na utume wa mashirika yetu katika kanisa na ulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutafakari upyaisho uhitajikao katika maisha ya wakfu na watawa, tangu kuundwa upya kwa maisha ya wakfu na utawa kwa kupitia Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, amependa wanawakfu na watawa tujitafakari iwapo tunu za maisha ya wakfu na utawa zimeendelea kuwa zawadi ya furaha ya upendo mungu kwetu binafsi, mashirika yetu, kanisa na jamii inayotuzunguka. Maana yake kila Shirika kadiri ya karama yake na wanashirika wake lijitafakari na wajitafakari kazi ya mwanzilishi wao na mavuvio ya Roho Mtakatifu yanavyoleta matunda kwao na kwa namna ya pekee katika wakati wetu. Pia alitualika tuwetumejitathmini iwapo kwa kujitoa kwetu katika wakati wetu kwa Mungu na Kanisa kwa namna ya pekee kwa ajili ya kazi ya pekee ya shirika husika iwapo bado tunafuraha na amani ya kutegemewa na Mungu?

Jambo la tatu la kusisitiza wanawakfu/watawa ni watu walio nafsi inayoitwa kuwa=Mungu ni mimi niliye (kut.3:13-17). Baba Mtakatifu Francisko alipotoa zawadi ya mwaka wa wanawakfu/watawa, ni kama aliyetafakari jibu la Mungu kwa Musa, Musa alipouliza jina la Mungu. Mungu anajitambulisha kuwa YEYE anaitwa “MIMI NDIYE NILIYE”. Kumbe kama Mungu anavyojitambulisha ni waSASA na siUKALE upitwa na wakati hivyo kutokufaa, ndivyo ambavyo Papa Francisko anatukumbusha wanawakfu/watawa wote tuwe watu tunaitwa kuwa tuwe hai kiwito na utume kadiri ya karama, katika wakati, bila kuacha kazi ya roho mtakatifu katika roho ya mwanzilishi, hali tukifurahia wito wetu na utume wetu siku kwa siku tukijifunua kwa roho mtakatifu kwa furaha, si huzuni au kununa.

Yaani kila mwanawakfu/mtawa katika Shirika lake iwapo mimi ni Padre Mvinsenti, wa Shirika la Misioni, lililoanzishwa na Vinsenti wa Paulo mwaka 1617, kule Ufaransa ni wajibu wangu na wetu kama shirika kuishi leo na kila mahali karama yetu ya KUMFUSA KRISTO MWINJILISHAJI WA MASKINI. Ni wajibu wangu kwa kuazimisha mwaka wa wanawakfu/watawa, mimi na sisi kama shirika kujitafakari furaha ya kuitwa kwetu na kufurahia utume wetu. Ulikuwa ni muda wa kujiuliza iwapo utume wetu unamatokeo chanya au hasi kwa kanisa na watu? Au pengine ni wito na utume jina tu ambao hauna matokeo yoyote kwetu wenyewe binafsi, shirika na kwa taifa la Mungu! Sisi kama wavinsenti na wote katika maisha ya wakfu na utawa bila kujalishirika gani mradi tumijifunga kwa nadhiri na viapo vya mashauri ya Injili iwe ni Wabenedikto, Wafransisko, Wakrara, Wasalvatori, Wanaunitas, Masista wa huruma, Mabruda wa Damu Azizi, Ndugu wadogo, Wagraili na wote wengine nisiowataja mwaka huu uliofikia kilele ni mwanzo wa kuanza vipya; tumetafakarishwa na kualikwa kujitambua kutokana na zawadi ya mwaka huu kwa kuionja FURAHA YA KWELI.

4. Jambo la mwisho la kujikita na kushikamana nalo ni hili kwamba: mwaka wa wanawakfu/watawa unafungwa na kufunguliwa daima na huruma ya Mungu katika uzuri na changamoto zake na za maisha ya kila siku. Tukio la adhimisho la Mwaka wa wanawakfu na watawa kimekuwa ni kipindi cha neema ya kujitafiti na kujitathmini na kuanza upya kama ilivyosemwa awali. Kilele chake katika mwaka huu 2016 ni mwanzo wa kushusha kapu na mkoba tuliosafiri nao kwa mwaka mzima katika safari ya tafakari ya mwaka mzima ili kutoa zawadi ya furaha ya wito wetu, ili kuanza tena safari ya MWANAWAKFU/MTAWA MWENYE FURAHA ambaye anashirikisha furaha ya Injili, furaha itokayo kwa Mungu mwenyewe.

Huwezi kutoa usichonacho, hivyo wanawakfu/watawa wametajirishwa na mwaka huu wa neema ya huruma ya Mungu. Ni mwaliko wanaopewa wanawakfu na watawa wote kushiriki sasa kushirikisha kwa watu wote hiyo furaha yao walioinja kwa namna ya pekee kama matunda ya mwaka huu ulioisha ili uanze tena kwa maisha yote ya kujitoa kwa Mungu na kuwa na Mungu.Wanawakfu/Watawa wamepata nafasi ya kuonyeshwa hali ya umauti iliyokuwa inanyemeleza na kujificha katika mitindo na mifumo ya maisha yetu ya wakfu na utawa ambayo ilibeba furaha ya uongo na kinafiki.

Mwaka wa Watawa Duniani umefunua na kualika uwanawakfu na utawa uwe ni ule ambao unatokana  na utakatifu au utakatifuzwaji unaoendana na jitihada ya kunia ukamilifu na si tu utakatifu na ukamilifu uliotayari ambao hauna jitihada tena ya kujikamilisha na kujitakatifuza. Mwaka umeonyesha uwanawakfu na utawa ni safari ya mtu binafsi na shirika kutoka katika ubinafsi, kama walivyotoka Waisraeli, bali sisi kutoka katika utumwa wa ubinafsi wa nafsi zetu za nira ya Farao wa dhambi na kusafiri kuelekea maongozi ya Mungu hadi kufikika katika nchi ya ahadi ya neema ya huruma ya Mungu ya kuwa wanawapendwa wa Mungu wanaotimiza mpango wa mungu unaoonekana katika uso wa Yesu aliyemwilika katika wakati ili kudhihirisha wazi huruma yake kwa mwaliko wa maisha ya kuishi amri za Mungu, mashauri ya Injili, Sakramenti na hasa kitubio/upatanisho kwani Yesu alikuja kuita wadhambi, na wote ni wadhambi, na katika dhambi hakuna furaha ya kweli, hivyo ni mwaliko ya kuikataa dhambi ili kuonja wema wa Mungu katika jitihada ya kuishi vema!

Fadhila za kikristo ni sura ya haraka inayotuwakilisha wanawakfu na watawa wote katika kanisa na jamii ituzungukaya. Kila shirika limekuwa na fadhila za msingi zilizo nyenzo rahisi za kuonja uzuri wa Mungu na kuonyesha uzuri wa Mungu kama wana wa Israeli walivyopenda kuuona uso wa Musa, na Mtume Petro na wenzake walivyomwona Yesu aking’aa kabla ya kukamilisha kazi yake ili kuwatia moyo na kuwafariji, ndiyo wanawakfu na watawa tuwe na fadhila mikononi ili kujifariji na kulifariji taifa la Mungu wanapomwona Mungu kwetu na tunavyompeleka Mungu kwa watu.

Fadhila za msingi za imani, matumaini na mapendo zipambwe na: Unyofu na maisha ya ukawaida: fadhila hii itusaidie KUTAMBUA wito na utume wetu ili kuushinda ulimwengu uliomchanganyiko na kuchanganyikiwa, vinginevyo ni changamoto kwetu wanawakfu kuingia katika kudanganyika na kudanganya tunapochanganywa na ya malimwengu. Malimwengu yanajitangaza hata kwa kudanganya kidogo na dhuluma. Kujifananisha na maisha ya ulimwengu wa sasa hata kama ni kuendana na wakati ni changamoto wazi ya maisha ya wakfu na utawa. Tujitambue.

Tunaalikwa kuwa WANYENYEKEVU ili TUVUMBUE wito na utume wetu kwa kujua nafasi yetu katika kuishi kwetu na watu. Ulimwengu unaishi kwa majivuno na uwezo. Sisi wanawakfu katika hali zote ndogo na kubwa tukumbuke hatujuivyote na sisi si kila kitu. Unyenyekevu utusaidie kuvumbua utume wetu kwa kanisa na jamii yetu. Vinginevyo changamoto ni jitihada ya sasa ya kuiga majivuno ya malimwengu.

Tujaliwe pia fadhila ya UPOLE ili TUPOKEE utume wetu kwa kanisa na jamii, kwani upole unatupa uwezo wa kuwavuta wote pale tunapoitawala hasira yetu kwa namna ya kujenga, tukivumilia madharau na uonevu tupatao, na kujijenga katika roho ya kusamehe. Upole utatufanya kuwa wajenga amani. Yesu anasema Yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, hivyo anweza kutoa pumziko la kweli (Mt.11:28-30). Upole ni kinyume cha ulimwengu unaopambwa na ukatili, chuki na kisasi. Giza hili lisiruhusiwe tena na kuharibu sura ya maisha ya wakfu na utawa. Tujipokee, tuwapokee wote, tupokeane wanawakfu na watawa kadiri ya upana na utajiri wa maisha ya wito na hitaji la utume katika kanisa bila kudharauliana kimashirika, wenyewe binafsi na watu wengine. Upole, wema na uzuri wetu na sala vitapunguza au kuondoa changamoto ya miito mitakatifu katika Kanisa.

Zaidi sana wanawakfu/watawa tujivike fadhila ya fadhila ya KUJITIISHA ili TUJIFUNZE wito na utume wetu. Kujitiisha ni neno la kizamani, yaani ni kama limepitwa na wakati, wengi wanatafuta raha, fahari na anasa. Lakini bila kujitiisha tutaishi tutakavyo na kufuata mapenzi yetu binafsi na si  vile apendavyo Mungu. Hatuwezi kupata vyote tutakavyo na tupendavyo. Hii ni roho ya kidunia inayonyemelea maisha ya wakfu na utawa. Lazima tujitiishe kwa kujikatalia mbambo mengine ya dunia hi ina kujibidiisha kujipatia tunu za kimungu. Tunaacha baadhi ya vitu vilivyo vizuri si kwa sababu tunafikiri ni vibaya, tunatambua tunaviacha ingawa vizuri ili kupata vilivyo vizuri zaidi. Kila siku tuna mwaliko wa kufanya uchaguzi. Wanawakfu na watawa ni chumvi na mwanga katika kanisa na jamii katika kujitiisha kuipa duania kielelezo cha kuchagua vile atakavyo Mungu ili kurudisha radha ya kimungu(Mt.5:13-16),radha ya kimungu iliyopotea katika ulimwengu ulioharibika kwa kukatatamaa na kupotoshwa kwa uchaguzi wa uwongo uliopendekezwa na dunia.

Hatimaya wanawakfu/watawa tuanaalikwa  kujipamba kwa fadhila na tabia ya kuwa na ARI. ARI inatudai kuwa WABUNIFU, WENYE BIDII NA UWEZO wa kushughulika na mazingira tofauti, pia kuuelewa ulimwengu kadiri ya namna zake tofauti za kufikiri na kutafsiri mahitaji yake. Ari itatufanya tutimize utume wetu kwa kanisa na watu. Ari itufanye tuwe na hamu ya ukweli, haki na kumpenda Mungu. Ari itufanye tuachane na changamoto za tamaa za matarajio makubwa na yapekee ya sifa, madaraka na uwezo usioendana na wito na utume wetu.

Yesu anasema “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi(Yn.15:16). Wanawakfu na watawa tujiaminishe kwa Mungu, kama Mama Bikira Maria mwanafunzi wa kwanza wa Mwana Mpendwa wa Baba. Ili kama Paulo Mtume tuseme kwa furaha “Si mimi tena ninayeishi bali ni Kristo anayeishi ndani yangu(Gal.2:20). Upendo wa Kristo utubidiishe katika wito na utume wetu katika kieleleze cha Utatu Mtakatifu sana ulio Mungu Mmoja (2 Kor.5:14). Tuadhimishe daima Huruma ya Mungu iliyotufuata kwa kutuita katika maisha haya ya kujitoa kwa Mungu bila mastahili yetu.

Imeandaliwa na: Pd. Paschal M. Mbepera, wa Shirika la Misioni/Wavinsenti,








All the contents on this site are copyrighted ©.