2016-01-31 10:16:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Uongozi, majiundo na maisha ya kijumuiya


Maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Watawa Duniani yanaendelea kupamba moto hapa mjini Vatican kwa kuwashirikisha watawa kutoka sehemu mbali mbali duniani wanaoendelea kutafakari kuhusu maisha, wito na utume wao ndani ya Kanisa, tayari kuwatangazia watu wa Mataifa Injili ya furaha, upendo na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wanahamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha karama za mashirika yao katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Kardinali Joao Braz De Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, walimwengu wanataka kuona ushuhuda wa karama mbali mbali za watawa zikimwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, karama za mashirika mbali mbali ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Kumbe, karama si mali binafsi ya watawa wanayopaswa kuikumbatia kwa uchoyo, bali zawadi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ujumla wake, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati.

Mifumo mbali mbali ya maisha ya kitawa ni hazina kubwa kwa Kanisa, mwaliko wa kumwongokea Mungu katika maisha na utume, kwa kuhakikisha kwamba, Mwenyezi Mungu anapewa kipaumbele cha kwanza na watawa. Hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, ni mtawa, huku akiwa mbali na Mwenyezi Mungu. Watawa wajenge utamaduni wa kuwa karibu na Mungu kwa njia ya: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo makini cha umwilishaji wa karama ya Mashirika husika.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Watawa na Kazi za Kitume anawataka watawa kujinasua mambo yanayoendelea kuwapatia usingizi wa kifo kama ilivyokuwa kwa Lazaro alipoamriwa na Yesu kutoka kaburini na kuanza maisha mapya. Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni fursa makini ya kutathmini na kuangalia maisha ya kitawa na kazi za kitume katika mwelekeo mpya mintarafu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na ongezeko la mifumo mipya ya maisha ya kitawa na kazi za kitume, matunda ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Viongozi wa Mashirika ya Kitawa wanakumbushwa kwa mara nyingine tena kwamba, uongozi ni huduma ya mapendo. Watawa wanapaswa kupewa majiundo awali na endelevu ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Watawa wawe ni mashuhuda wa mshikamano wa upendo unaojionesha katika maisha ya kijumuiya. Uongozi wa kitawa ukichukuliwa kama huduma ya upendo, unapata mwelekeo mpya kabisa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa zamani, mkuu wa Shirika au nyumba alikuwa na mamlaka kiasi cha kujisikia kuwa kama mkurugenzi wa kampuni fulani. Lakini, kwa watawa mambo yanapaswa kuwa ni tofauti kabisa, uongozi ni chachu ya kufahamiana, kusaidiana na kusindikizana katika hija ya maisha na utume wa kitawa, kwa kutambua kwamba, hapa “kuna kutesana kwa zamu”

Mashirika ya Kitawa hayana budi kuendelea kujikita katika mchakato wa malezi ya awali yanayorutubishwa kwa malezi endelevu, hadi pale mtawa anafikia hatima ya maisha yake, tayari kuingia katika maisha ya uzima mpya kwa njia ya usingizi wa amani. Kipaumbele cha kwanza ni binadamu, utu na mahitaji yake msingi. Kabla ya yote watawa wafundwe kuwa binadamu, wakristo na hapo wanaweza kuendelea kufundwa ili wawe ni watawa wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Maisha ya Kijumuiya yanahitaji sadaka, majitoleo na uvumilivu, ili kusaidiana, kuelewana na kutaabikiana kama watawa. Maisha ya Jumuiya yanakuwa kweli ni shule ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukata mzizi wa ubinafsi na hali ya baadhi ya wanajumuiya kujisikia kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine. Maisha ya Jumuiya ni shule ya kusikilizana kwa dhati, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kuondokana na wivu, chuki, uhasama, visasi na madonda yanayojitokeza katika maisha ya watawa! Haya yasipopewa tiba muafaka, sala na tafakari hazitasaidia kitu anasema Askofu mkuu Carballo. Watawa wawe na ujasiri wa kuangalia ukweli kwa macho makavu kabisa!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe Mosi Februari 2016 anakutana na kuzungumza na watawa kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Tarehe 2 Februari, 2016, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya saa 11:30 Jioni anatarajiwa kuadhimisha Siku kuu ya Watawa Duniani sanjari na kufunga Mwaka wa Watawa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.