2016-01-28 12:03:00

Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa!


Ekaristi Takatifu ni fumbo la imani ambalo linapaswa kusadikiwa, kuadhimishwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu kama ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Hii ni Sakramenti ya upendo, zawadi kuu kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Ni chakula cha kweli katika maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli mashuhuda wa Ekaristi kwa jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendani.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na Maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa anasema kwamba, hili ni tukio la Kikanisa, ambalo, waamini wanapaswa kweli kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuliwezesha Kanisa Katoliki kuwa na utamaduni wa kuadhimisha Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa na Mwaka huu Kanisa linaadhimisha Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaloongozwa na kauli mbiu“Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”.

Maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa yanawapatia waamini fursa ya kumtafakari Kristo Yesu, tumaini na uhai wa Kanisa. Makongamano ya Ekaristi Takatifu iwe ni ngazi ya Kimataifa au kitaifa yanawashirikisha wawakilishi kutoka katika Makanisa mahalia, kama ilivyo kwa wakati huu huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini. Lakini, ikumbukwe kwamba, hata wale Wakatoliki ambao hawakupata nafasi ya kushiriki moja kwa moja wanapaswa kuungana kwa moyo wote na Kanisa zima katika kumwabudu, kumtukuza, kumsifu na kumwadhimisha Yesu Yesu, sanjari na kulitafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Ruwaichi anawaalika waamini kumpokea Yesu wa Ekaristi Takatifu ndani ya maisha na mioyo yao kwa namna ambavyo inakidhi mahitaji yao kama watu wa Mungu. Ni changamoto kwa Wakatoliki wote kukuza na kudumisha roho na moyo mmoja katika kumshuhudia Yesu wa Ekaristi na kuendelea kumwabudu kama Kanisa moja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.