2016-01-28 08:20:00

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya huduma ya huruma na upendo!


Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu yawasaidie waamini kujikita katika huduma ya mapendo kwa kumwilisha matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama kielelezo cha  imani tendaji. Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika tafakari yake kwenye maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaloendelea Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”.

Tafakari ya Kardinali Turkson imewasilishwa kwa wajumbe wa kongamano hili la kimataifa na Askofu mkuu Antonio J. Ledesma wa Jimbo kuu la Cagayan de Oro. Kardinali Turkson anafafanua kwa kina na mapana uhusiano uliopo kati ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama anavyochambua Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Laudato si. Bara la Asia linakabiliwa na umaskini mkubwa wa hali na kipato kwa wakazi wake; hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kumbe, waamini wanapaswa kutambua kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote na kwa njia hii, wataweza kugundua kiini cha maisha na wito wao kama waamini wa Kanisa Katoliki. Hii inatokana na ukweli kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kama wanavyofundisha Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ekaristi Takatifu inaweza kuangaliwa kwa mapana kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Taalimungu juu ya ekolojia inawahamasisha waamini kuguswa na kilio cha maskini, wagonjwa na wenye njaa, tayari kuwasaidia kwa hali na mali. Ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha chakula kinachotupwa kwenye mapipa ya taka, hii ni haki ya chakula ambayo maskini wamepokwa kutoka midomoni mwao. Baadhi ya wanataalimungu kutoka Amerika ya Kusini wanasema, ni kufuru kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kutumia mkate ulioibwa. Matoleo ya sadaka yanayofanywa na waamini wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ni matunda na kazi ya mikono ya wanadamu. Huu ndio uelewa mpana zaidi wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu mintarafu Wakristo wa Kanisa la mwanzo.

Familia ya Mungu inapaswa kuonesha upendo na mshikamano unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa wale waamini ambao wamekirimiwa utajiri na maisha mazuri zaidi wanapaswa kuguswa na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili matoleo yao yasaidie pia kuganga njaa, magonjwa na kiu ya maskini wa hali na kipato katika maeneo husika. Hapa Ekaristi Takatifu inapata mwelekeo wa kijamii unaojikita katika huduma makini inayotolewa na Mashemasi.

Kardinali Turkson anakaza kusema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitambua umuhimu wa Ekaristi inayofumbatwa katika huduma ya upendo na mshikamano, wakatilia mkazo uwepo wa Mashemasi ili kudhihirisha huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashemasi wanatekeleza dhamana ya huduma ya upendo wanapozunguka Altare wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini pia wanapokuwa mitaani wakiwahudumia maskini, wazee, wagonjwa na wale wote wanaohitaji msaada na huruma ya Mama Kanisa.

Mashemasi wanahamasishwa kuonesha ile fadhila ya unyenyekevu katika huduma, kama ambavyo wanapaswa kushuhudia Wakleri wote ambao kimsingi ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Liturujia haina budi kumwilishwa katika maisha ya watu, ili kupata ile maana inayokusudiwa na Mama Kanisa, yaani Liturujia ya maisha inayoadhimishwa katika hija ya maisha ya waamini kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu.

Ikumbukwe kwamba, matoleo ni mazao na matunda ya kazi ya mikono ya wanadamu, yanayopaswa kutumiwa kwa busara na nidhamu. Hapa dhana ya kazi inaingia moja kwa moja kwani kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Wafanyakazi wanapaswa kupatiwa haki zao ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kwa familia na jamii katika ujumla wake. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafafanua kwa kina na mapana juu ya dhana ya kazi, wajibu wa kufanya kazi, heshima ya kazi, haki ya kufanya kazi, haki za wafanyakazi, mshikamano na mambo mapya katika ulimwengu wa kazi.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira kwani kazi za binadamu pia zimechangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu na uchafuzi wa mazingira na madhara yake ni watu wengi kuendelea kutumbukia katika umaskini, magonjwa pamoja na mipasuko ya kijamii inayozalisha makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yana mwendelezo makini katika maisha ya waamini wanaohamasishwa kutambua, kuheshimu na kuthamini utakatifu wa kazi ya uumbaji katika medani mbali mbali za maisha. Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha ushindi wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mahusiano haya kati ya ushindi wa maisha dhidi ya kifo; kati ya wema na ubaya; yawasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na uwinao bora katika matumizi ya mali na rasilimali ya dunia, ili iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.