2016-01-22 15:47:00

Familia kiteni maisha yenu kwenye Sala na Tafakari ya Neno la Mungu


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linatumia kila fursa inayopatikana katika maisha na utume wake, ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo kati ya Familia ya Mungu nchini humo, ili iweze kuwa tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaobubujika kutoka katika Neno la Mungu, Mafundisho tanzu ya Kanisa na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu!

Neno la Mungu: ni nguvu ya familia na matumaini ya taifa, ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Juma la Biblia Takatifu nchini Ufilippini kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 31 Januari 2016, sanjari na Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, taifa linalompatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza, taifa hilo litakuwa na baraka na neema tele. Kwa wale wanaomwamini Mungu, wataokolewa pamoja na familia zao.

Maadhimisho ya Juma la Biblia Takatifu nchini Ufilippini yatafungwa rasmi hapo tarehe 31 Januari 2016, tayari kwa Familia ya Mungu nchini humo, kuendelea kumwilisha utajiri wa Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yake, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Juma hili litawasaidia waamini kutangaza, kutafakari na kushuhudia Neno la Mungu katika maeneo ya hadhara pamoja na kuendelea kuhamaisha umuhimu wa Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Itakumbukwa kwamba, ni katika kipindi hiki, Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yatakuwa yanaendelea kutimua vumbi Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini. Hizi zote ni fursa za majiundo endelevu kwa waamini katika maisha yao ya kiroho na kiutu, tayari kumshuhudia Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.