2016-01-21 10:46:00

Mchakato wa Uinjulishaji mpya unaojikita katika majadiliano na utamadunisho!


Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa nchini Ufilippini, litakaloanza hapo tarehe 24 hadi 31 Januari 2016, Jimbo kuu la Cebu, linaongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”. Askofu mkuu Piero Marini, Rais wa Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho haya ni nafasi ya kujikita katika Uinjilishaji mpya Barani Asia kwa njia ya majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu mambo msingi katika Uinjilishaji.

Maadhimisho haya sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kutaka kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kushikamana na kuambata huruma ya Mungu katika mikakati na mipango ya maisha yao kwa siku za usoni. Itakumbukwa kwamba, Ufilippini na Timor ya Mashariki ni mataifa mawili ambayo yana idadi kubwa ya Wakatoliki Barani Asia.

Watu wengi bado wana kiu ya kutaka kumfahamu Kristo Yesu na kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji. Haitoshi kufahamu Maandiko Matakatifu na Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini watu wanataka kuona imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Maadhimisho haya ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha.

Changamoto ya pili ni utamadunisho, ili kweli tunu msingi za Kiinjili ziweze kupenya na kugusa maisha ya wananchi wa Bara la Asia; Injili isafishe na kuponya pale ambapo kuna misigano kati ya Injili ya tamaduni za Bara la Asia. Jimbo kuu la Cebu ni kitovu cha Uinjilishaji wa awali nchini Ufilippini, dhamana iliyotekelezwa kunako mwaka 1521, Wamissionari wa kwanza walipotua nanga nchini humo. Ufilippini ni kielelezo makini cha utamadunisho ambao umeiwezesha imani kupenya katika maisha na vipaumbele vya watu.

Askofu mkuu Piero Marino anakaza kusema Uinjilishaji mpya, Utamadunisho na Majadiliano ya kidini ni mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi Barani Asia, ili kweli Injili ya Kristo iweze kusonga mbele. Imani inayoungamwa, haina budi kuadhimishwa katika maisha ya watu; kumwilishwa katika maisha adili na Sala. Imani iwasaidie waamini wa dini mbali mbali kukuza na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na maridhiano, kwani wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu.

Askofu mkuu Piero Marini anaendelea kufafanua kwamba, Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni sehemu ya maisha na vinasaba vya Kanisa. Ni matukio yanayotaka kufafanua na kushuhudia imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ni nafasi ya kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kujikita katika katekesi makini na mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti za Kanisa na umuhimu wake katika maisha ya waamini. Makongamano haya yanapania pamoja na mambo mengine kuhamasisha ari na mwamko wa kimissionari, ili waamini waweze kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Kimataifa yamelisaidia Kanisa kuwa na mwelekeo mpana zaidi kuhusiana na maadhimisho haya, kwa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya waja wake. Ni nafasi ya kuonesha umoja na mshikamano wa Kanisa zima katika imani, matumaini na mapendo.

Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yanafanyika Jimbo kuu la Cebu, katika eneo ambalo watu wake ni maskini, lakini hata katika umaskini wao ni watu ambao wana imani thabiti; ni watu wenye kushuhudia Injili ya uhai pamoja na Injili ya furaha. Wakatoliki nchini Ufilippini ni mashuhuda wa uaminifu wa tunu msingi za maisha ya Kikristo; imani, umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.