2016-01-21 15:43:00

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.


Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaanza kuadhimishwa tarehe 24 Januari 2016 na litahitimishwa hapo tarehe 31 Januari 2016. Maadhimisho haya yanafanyika kwenye Jimbo kuu la Cebu, nchini Ufilippini kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu”. Hii inatokana na ukweli kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na lengo la utume na maisha ya Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ufilippini linasema maandalizi yote tayari yamekwisha kukamilika. Zaidi ya wajumbe elfu kumi kutoka nchini Nchini Ufilippini wanatarajiwa kuungana na wawakilishi elfu nane na mia tano kutoka katika mataifa sabini na moja. Hili ni Kongamano la pili kimataifa kuadhimishwa nchini Ufilippini. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1937, Kongamano la thelathini na tatu la Ekaristi Takatifu Kimataifa liliadhimishwa Jimbo kuu la Manila, wakati wa Uongozi wa Baba Mtakatifu Pio wa kumi na moja.

Tema iliyochaguliwa kwa maadhimisho ya Mwaka huu wa 2016 ni mwendelezo wa tema iliyoongoza maadhimisho ya Kongamano la 50 ya Ekaristi Takatifu Kimataifa lililoadhimishwa Jimbo kuu la Dublin nchini Ireland kunako mwaka 2010. Mada hii inataka kukazia pamoja na mambo mengine tafakari ya msingi kuhusu maisha ya mambo ya nyakati mintarafu Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Hapa waamini wanahamasishwa kuwa na matumaini katika maisha, huku kila mmoja wao akitekeleza dhamana na majukumu yake ndani ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake, kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa Barani Asia linataka kuwajengea vijana matumaini katika hija ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni. Vijana wajengewe matumaini kwa kupambana kufa na kupona na umaskini wa hali na kipato.

Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa kwa mwaka huu yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, chemchemi makini ya mchakato wa kupyaisha imani, matumaini na maisha ya kiroho miongoni mwa Wakatoliki. Fursa ya kuambata matumaini kwa wale waliokuwa wanaanza kukata tamaa anasema Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilippini. Kuna umati mkubwa wa watu waliokata tamaa kutokana na vita, maafa na majanga mbali mbali ya maisha, kumbe, Jubilei ya huruma ya Mungu na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi takatifu, vinakuwa ni chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na maridhiano kati ya watu.

Ni matumaini ya Kardinali Tagle kwamba, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa, yatasaidia waamini kujichotea utajiri mkubwa unaobubujika kutokana na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kardinali Timothy Dolan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la New York Marekani, Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, Kardinali Oswald Graciusa wa Jimbo kuu  la Mumbai pamoja na Askofu msaidizi Robert Barron wa Jimbo kuu la Los Angeles, Marekani ni kati ya wawezeshaji wakuu wakati wa maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, linaloadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, nchini Ufilippini. Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon, Birmania ndiye aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa mwakilishi wake wa kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.