2016-01-20 17:17:00

Maaskofu Katoliki Kenya watuma salam za rambi rambi kwa familia ya Mungu Kenya


Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa. Usiogope wala usifadhaike, kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako. Huu ni ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa familia ya Mungu nchini Kenya wakati huu inapoomboleza vifo vya askari waliouwawa kikatili na wengine bado hawajulikani mahali walipo kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab nchini Somalia.

Maaskofu katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yao na Askofu Philp Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wanasema, askari hawa wameuwawa kikatili wakati walipokuwa wanatekeza dhamana na wajibu wao. Wale waliopata majeraha wanaombewa ili waweze kupona haraka ili kuendelea na shughuli zao za kila siku. Maaskofu wanawaombea wale wote ambao hadi sasa hawajulikani mahali walipo, ili wapatikane na hatimaye, wajiunge na familia zao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanaotekeleza dhamana na wajibu wao nchini Somalia na kwamba, wako pamoja nao katika sadaka na sala zao za kila siku. Maaskofu wanaialika Familia ya Mungu nchini Kenya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa familia zilizoguswa na kutikiswa na mauaji haya ya kinyama katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na maombolezo. Damu ya mashujaa iliyomwagika nchini Somalia, isaidie kujenga na kudumisha: upendo, umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendelea kusali na kuombea amani na usalama nchini Somalia ambayo kwa miaka kadhaa sasa haijawahi kupata amani na usalama, ili Mwenyezi Mungu aweze kusaidia juhudi za upatikanaji wa amani nchini Somalia. Amani nchini Kenya itaweza kudumishwa pale tu, Somalia nayo itakuwa katika hali ya amani na utulivu. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kumhakikishia Rais wa Kenya ambaye pia ni Amiri Jeshi mkuu mshikamano na wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote wa Kenya kwa njia ya sala na sadaka yao. Wanaiomba Serikali kuendelea kuonesha mshikamano wa dhati na familia zilizoguswa na kutikiswa na mauaji ya kinyama huko Somalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.