2016-01-12 08:07:00

Jumuiya ya Kimataifa bado ina uwezekano wa kutoa faraja kwa walimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbali mbali ya Kimataifa siku y aJumatatu tarehe 11 Januari 2016 mjini Vatican ameitaka kwa namna ya pekee, Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wahamiaji na wakimbizi wanaotaka kusalimisha maisha kutokana na vita, machafuko na kinzani mbali mbali za kijamii. Hili ni kundi la watu wanaotaka maisha bora pamoja na kujenga matumaini kwa siku za usoni.

Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kutatua migogoro na kinzani za kijamii, ili kusalimisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kukumbana na maafa pamoja na majanga ya maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, mshikamano na maridhiano kati ya watu;  kuna haja ya kupambana na ujinga na umaskini na uharibifu wa mazingira, sanjari na kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kwa kujikita katika kanuni msingi za ubinadamu!

Kwa upande wake, Balozi Armindo Fernandes do Espirito Santo Vieira, kutoka Angola ambaye ni Dekano wa Mabalozi wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa mjini Vatican, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na Wanadiplomasia mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 11 Januari 2016 amesema kwamba, katika maafa na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu, bado kuna uwezekano wa kupata chakula cha kutosha ili kushibisha njaa ya walimwengu.

Hata maskini katika umaskini wao wanayo mambo wanayoweza kuwashirikisha wengine katika ustawi na maendeleo ya watu kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki na amani inayojikita katika upatanisho na msamaha wa kweli, mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ujumbe wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unapania pamoja na mambo mengine kutoa nuru inayoangaza na kuamsha dhamiri za watu.

Balozi Armindo amegusia matukio makuu yaliyojiri katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2015 kwa kusema kwamba, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia imekuwa ni fursa muhimu kwa Kanisa kuonesha upendo na mshikamano na familia katika kudumisha maisha na utume wake ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo, ili kweli familia ziweze kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Balozi Armindo anakaza kusema, hija za kitume zilizotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko sehemu mbali mbali za dunia imekuwa ni fursa ya kuhimiza majadiliano ya kidini na kiekumene; haki, amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu; ushirikiano wa kimataifa na kikanda, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa linaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa utume wa vijana ulimwenguni ili kuwajengea imani na matumaini, tayari kuambata tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kiroho. Baba Mtakatifu Francisko kwa kufungua Lango la huruma ya Mungu kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati, amewasha moto wa matumaini, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ameonesha na kushuhudia jinsi Kanisa linavyoguswa na mahangaiko ya maskini na wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Balozi Armindo, Dekano wa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa mchango wake katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuendelea kukazia majadiliano ya kidini ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa kwa maisha ya watu na mali zao. Bado Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini sanjari na kukabiliana na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi linalohitaji usalama na maisha bora zaidi. Ni matumaini ya Dekano wa Mabalozi kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yatawasaidia watu kumwilisha ari na moyo wa huruma, msamaha, neema na mapendo kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.