2016-01-10 11:51:00

Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu!


Wakristo wa Makanisa mbali mbali kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 25 Januari 2016 wanaadhimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, ambalo kwa mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu “Mpate kuzingataza fadhili za Mungu”. Hapa Wakristo wote wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuhakikisha kwamba, wanazitangaza fadhili za Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko.

Muswada wa mwongozo wa maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo umeandaliwa na waamini wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanaoishi huko Lithuania, kwa mwaliko wa Askofu mkuu Zbignevs Stankevics wa Jimbo kuu la Riga, Lithuania. Muswada huu ukapitiwa na kuhaririwa na Tume ya Imani inayoundwa na wajumbe kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na Baraza la Kipapa na Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.

Wawakilishi wa Makanisa mbali mbali wanawaalika Wakristo kugundua ukweli unaofumbatwa katika Kanisa la mwanzo, lililokuwa limeanzishwa hivi punde tu na hivyo kuanza hija ya kukutana na Injili ya Kristo, iliyowawezesha kumpokea Kristo Yesu na hivyo kufanyika kuwa ni sehemu ya Taifa la Mungu, baada ya kupokea mwaliko wa Kristo na kubatizwa katika Maji na Roho Mtakatifu. Kabla ya hapo hawakubahatika kuonja huruma na upendo wa Kristo, lakini kwa sasa wanaogelea katika bahari ya huruma na upendo wa Kristo, Hapo mwanzo hawakuwa na neema, lakini kwa sasa wamekirimiwa neema juu ya neema.

Wakristo wanakumbushwa kwamba, wameteuliwa na Mwenyezi Mungu kadiri ya upendo na huruma yake na wala si kwamba, wanastahili, bali Mwenyezi Mungu ana mpango maalum kwa ajili ya watu wake, yaani kutangaza na kushuhudia fadhili za Mungu. Katika mwelekeo kama huu, Jumuiya za Kikristo zinahamasishwa kuhakikisha kwamba, zinawakumbuka na kuwaenzi Mashuhuda wa imani, waliyoyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.