2016-01-09 09:48:00

Ujumbe wa mwanga wa matumaini ya amani Sudan ya Kusini!


Askofu Edward Hiiboro Kussala wa Jimbo Katoliki la Tombura-Yambio, Sudan ya Kusini, anawaalika waamini pamoja na wananchi wote wenye mapenzi mema nchini Sudan ya Kusini kutokata tamaa wala kutoa mwanya kwa woga na wasi wasi kutawala katika mioyo na akili zao, mambo yanayoweza kuisambaratisha Sudan ya Kusini na hivyo kushindwa kujinasua kutoka katika mzunguko wa machafuko ya kivita na mpasuko wa kijamii.

Sudan ya Kusini inaendelea kuogelea katika dimbwi la vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kinzani za kisiasa, mambo ambayo yanaendelea kukwamisha mchakato wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Mwaka 2015 umemalizika kwa Serikali kupambana na vikosi vya waasi, licha ya juhudi za Jumuiya ya Kimataifa za kupatanisha pande hizi mbili zinazosigana na hatimaye, kuweka sahihi kwenye mkataba wa amani huko Arusha, Tanzania.

Tangu Desemba 2013 Sudan ya Kusini imetumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe jambo linalokwamisha ustawi na maendeleo ya wengi pamoja na kuendelea kuzalisha umati mkubwa wa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baa la njaa na magonjwa ni mambo yanayoendelea pia kuwanyemelea wananchi wengi wa Sudan ya Kusini. Mashambulizi haya ya kivita yanaendelea kuharibu miundo mbinu kama vile shule, mahali ambapo watoto wangepaswa kupata elimu, itakayowasaidia kupambana na maisha kwa sasa na kwa siku za usoni.

Askofu Kussala kwa masikitiko makubwa anasema shule zinazoshambuliwa ni matunda ya ushirikiano na mshikamano na watu wenye mapenzi mema kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Askofu Kussala anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati kupinga vita na vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa haki, amani na utulivu; wote kwa pamoja wasimame kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa, haki, amani na maridhiano.

Viongozi wa kisiasa wanapaswa kutekeleza dhamana yao kwa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika makubaliano ya Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi Jijini Arusha, Tanzania. Wananchi washinde woga na wasi wasi ili kujenga ari na matumaini mapya kwa Sudan ya Kusini iliyo bora zaidi, inayojikita katika misingi ya haki, amani, udugu na mshikamano wa kitaifa. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini kwa namna ya pekee, wanahimizwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, huruma na mapendo ya Mungu.

Viongozi wa kisiasa waoneshe ujasiri na ukomavu wa demokrasia kwa kutekeleza kwa dhati kabisa makubaliano ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kimataifa ili kukata mzizi wa vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Haya ni makubaliano yaliyofikiwa kunako mwezi Agosti 2015, lakini hadi leo hii makubaliano haya yamehifadhiwa kwenye makabati na watu wanaendelea kupoteza maisha na mali zao kutokana na vita. Askofu Kussala anaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuimarisha ulinzi na usalama Sudan ya Kusini, ili kuhakikisha kwamba, makubaliano ya amani yanatekelezwa na wahusika, ili watu waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida.

Wananchi wengi wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato; ujinga na magonjwa kutokana na vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Wawezekaji wa ndani na nje waliokuwa wameanza kuonesha matumaini kwa kutaka kuwekeza nchini Sudan ya Kusini, wanaendelea kukata tamaa kila kukicha na matokeo yake, uchumi unaendelea kudorora kwa kasi ya ajabu.

Ni matumaini ya Askofu Kussala kwamba, Mwaka mpya wa 2016 utaleta mwanga wa matumaini mapya kwa wananchi wa Sudan ya Kusini, kwa kufukuza giza la vita, umaskini, magonjwa na njaa. Kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake, Sudan ya Kusini inaweza kung’amua kwa mara nyingine tena uwepo wa Mwanga wa huruma ya Mungu, yaani Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.