2015-12-28 10:15:00

Alijiandalia safari ya kukutana na Yesu kama: Mkristo, Padre, Askofu na Mtawa!


Marehemu Askofu Gervas Nkalanga alikuwa ni Askofu mzalendo wa nne kuwekwa wakfu nchini Tanzania. Anakumbukwa na Kanisa la Afrika Mashariki kwa kushiriki kuanzisha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati. Alishiriki katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kushuhudia cheche za uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Katika maisha na utume wake kama mtawa, alionesha jeuri ya kufanya kazi kwa juhudi, bidi na maarifa! Akajifunza kusali kwa ibada na uchaji mkuu, kiasi cha kuwa ni mtawa na mkulima bora wa ndizi Songea huko alikokuta “ndizi pori”. Miaka 33 ya Utawa si haba kama kiatu cha raba anastahili kuvuliwa kofia! Yataka moyo kweli kweli! Kama hutokwi na machozi ya shukrani, wewe ujue kwamba, unalo lako moyoni!

Tarehe 18 Desemba 2015 Saa 7:45 jioni baada ya safari ndefu ya maisha, Askofu mstaafu Gervas Nkalanga wa Jimbo Katoliki Bukoba na Mtawa wa Shirika la Wabenediktini wa Abasia ya Mt. Mauro Hanga, Jimbo kuu la Songea, Tanzania amepumzika katika Bwana wa milele. Tarehe 29 Desemba 2015 Familia ya Mungu nchini Tanzania inakusanyika ili kumtakia heri na kumuaga, ili akaonane na Yesu na kufurahi pamoja naye milele yote baada ya utume na maisha yake hapa duniani kama Mkristo, Padre, Askofu na Mtawa! Marehemu Askofu mstaafu Nkalanga maarufu kwa jina la kitawa kama Frt. Placidius, OSB, alianza safari yake hapa duniani tarehe 19 Juni 1919 akiwa mtoto wa nne kati ya watoto sita, kwa wazazi Norbertus Kasimbazi (1886-1948) na mama Flavia Kabonesa (1893-1965) huko kijijini Buhanga-Ruti Bukoba. Siku hiyo hiyo ya kuzaliwa akabatizwa na kupewa jina Gervas katika Parokia ya Mugana na kupewa namba 1950 ya ubatizo, na huo ukawa ni mwanzo wa hija yake ya maisha ya Kikristo!

Akiwa na umri wa miaka 10 yaani mwaka 1929 akaanza shule ya msingi Mugana. Baada ya miaka miwili akapata Komunio ya kwanza. Chakula hicho cha Bwana kilimpa nguvu ya kutaka kutanguzana na Yesu Kuhani mkuu katika safari zake za kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Mwaka 1931 alipofika darasa la tatu, akafanya mtihani wa Seminari ndogo ili awe Kuhani. Akiwa na umri wa miaka 12 kama ya Yesu alipoenda Hekaluni na wazazi wake na kuachiliwa huko, Gervas naye aliingia Seminari hadi mwaka 1937. Baada ya kuhitimu darasa la nane, mwaka 1938 akajiunga na chuo cha Ualimu Kajunguti na kupata Cheti cha Ualimu daraja la Pili.

 Mwaka 1939 akaenda Seminari kuu Katigondo-Uganda kusoma Kilatini, Falsafa na Taalimungu. Safari ya masomo aliihitimisha tarehe 15 Julai, 1950 mwaka wenye namba inayolingana na ile ya ubatizo. Akawekwa Wakfu wa ukuhani na kukabidhiwa mikoba ya Yesu ya kumtumikia Mungu na watu kwa unyenyekevu na upole. Askofu aliyempadrisha, Monsignori L. Tetrault akamtuma kufanya kazi Kashozi – Parokia mama ya Jimbo la Bukoba. Baada ya miaka mitatu akahamishwa na kupelekwa Parokia ya Rutabo katika Jimbo au Vicariat ya Lower Kagera, chini ya Askofu Laureani Rugambwa. Mwaka 1955 aliteuliwa kuwa Katibu wa Elimu wa Jimbo hadi mwaka 1961 akitumia Taaluma yake ya ualimu.

Kazi katika safari yake ya maisha iliongezeka lakini ilikuwa nyepesi kama alivyosema Yesu mwenyewe: “Mzigo wangu ni laini na mwepesi. Mkiwa wanyofu na wanyenyekevu wa moyo mtaweza kubeba.” Ndipo tarehe 18 April 1961 akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Kardinali Laurean Rugambwa  wa Jimbo la Bukoba. Terehe 21 Mei 1961 akatiwa wakfu na Mtakatifu Yohane XXXlll – Papa. Wakati wa Madhehebu haya wasaidizi walikuwa Askofu Fulton Sheen wa New York, rafiki mkuu wa Askofu Gervas, na Askofu Edoardo Mason, F.S.C.J. Katika safari yake kama Askofu, Gervas akamchagua Mama Bikira Maria kuwa kinga yake, akiongozwa na maneno ya utenzi alioupenda kuuimba daima kwa Kilatini na kurudia zaidi maneno matatu aliyoweka kwenye ngao yake ya kiaskofu: “iter para tutum = Uniandalie vizuri safari yangu.” Wakati huo alikuwa askofu wa nne mzalendo katika Tanzania.

Mwaka huo huo mwezi Julai baada ya kuwekwa wakfu, akahudhuria mkutano wa kwanza wa Umoja wa Maaskofu Afrika Mashariki –ITEBEA (Inter-Regional Episcopal Board in Eastern Africa) Dar-es-Salaam. Wazo la kwanza la kuwa na umoja huo ni la Maaskofu wa Tanzania mwaka 1960 pindi Gervas akiwa Katibu wa Elimu. Mwaka 1964, ITEBEA ikabadilika kuwa AMECEA. Kwa hiyo Askofu Gervas ni Muasisi wa AMECEA. Mwaka mmoja baada ya kuaskofishwa, akashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican ulioanza kutimua vumbi mwaka 1962 hadi 1965. Kwa hiyo Askofu Gervas ni “Baba wa Mtaguso mkuu.”

Baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kunako mwaka 1966 akatumwa kwenda kuanzisha Jimbo jipya la Kabale huko Uganda kama Msimamizi wa Kitume utume alioutekeleza kwa miaka mitatu hadi mwaka 1969. Katika kipindi hicho alilijenga jimbo na kulistawisha kwa miradi mingi ya kiroho na kimwili. Kazi yake ilikuwa nzuri hadi Papa Paulo Vl akamrudisha Tanzania mwaka 1969, kuwa Askofu wa Jimbo la Bukoba badala ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliyehamishiwa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Mwaka huo huo akachaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1970.  “Roho ina nguvu na mwili ni dhaifu,” ndivyo alivyoanza kujisikia katika safari yake ya utumishi wa Kristo.

Afya yake ilianza kutetereka na nguvu za mwili kumpungua. Ndipo mwaka 1973 akastaafu kuwa Askofu wa Jimbo akachagua kuwa mtume katika Parokia ya Kishogo. Hadi hapa safari ya maisha ya Askofu Gervas iliyoandaliwa na Mama Maria “iter para tutum” imeenda vizuri. Akawa amefanya utume mkubwa ulioonekana machoni pa ulimwengu na ameacha fundisho la kuwa wanyenyekevu na wanyofu katika utumishi wa Kanisa wakati wote alipokuwa akifundisha, akiongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu.

Kipindi cha miaka nane aliyoishi Parokiani Kishogo, kilikuwa muhimu sana kwa Askofu Gervas na tunaweza kukilinganisha na maisha ya Yohane Mbatizaji mtangulizi wa mkombozi wetu. Yohane Mbatizaji alitegemewa kurithi mikoba ya ukuhani wa Baba yake Zakaria, lakini akaiacha na kwenda Jangwani kuishi na watawa wa Kumrani. Hao walikuwa watawa walioyatoroka mazingira ya mji wa Yerusalemu na Makuhani potofu wa Hekaluni. Huko Jangwani Kumran ndiko tunasikia “Neno likamjia Yohane” la kutumwa kuandaa safari ya Yesu hapa duniani. Ndivyo Mama Maria alivyomwandalia mazingira ya safari nzuri Askofu Gervas. Akiwa Kishogo akapata wazo la kuingia utawa. Akachagua kuingia utawa wa Wabenediktini unaoongozwa na kauli mbiu Ora et Labora - Sala na kazi. Sera hii ya Sala na Kazi ndiyo iliyoleta maendeleo ya Ulaya na popote duniani yaani “Mungu tu na Kazi tu.” Rais John Pombe Magufuli angekaza kusema “Hapa kazi tu!”

Kwa bahati mbaya, Askofu hakukubaliwa kirahisi kujiunga, kama isemavyo kanuni ya Mtakatifu. Benedikto “Zijaribuni roho hizo kama zimetoka kwa Mungu.” Kwa hiyo, Shirika zima la Wabenediktini ulimwenguni liliingiwa na hofu na mshangao kumwona Askofu kujiunga na utawa. Ikikumbukwa kuwa lengo la watawa wa kwanza wa Misri kutorokea Jangwani ni kujitenga na wanawake na Askofu kama Yohane Mbatizaji. Ombi lake lililetwa kwa Prior Frt. Gregory Mwageni OSB, naye alipoona ni maji marefu akalipeleka ombi kwa Abate mkuu Notker Wolf OSB wa Shirika –Ujerumani. Akaridhia akubaliwe kwani maisha ya utawa ni ya upendo kamili- Perfectae Caritatis, kila mmoja ameitwa kuishi. Ndiyo maana Kanisa linampongeza na kumshukuru kwani ameona pia cheche za maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani wanaohimizwa kwa namna ya pekee kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasam na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Mwaka 1983 alipofika utawani siku ya kwanza, mkuu wa utawa Prior Frt. Gregory Mwageni OSB pamoja na watawa wakamwinamia kwa heshima na kumshangaa. Naye akasimama na kuwaamkia watawa kwa unyenyekevu: “Tumsifu Yesu Kristo, Waheshimiwa Watawa! Ninamshukuru Mungu kufika hapa utawani. Ninaomba mnipokee katika Jumuia yenu ili niweze kujiandaa kufa vyema.” Watawa waliposhtuka akaendelea: “Hii, msishtuke. Tena kutokana na afya yangu naomba mnitunze kwa miaka mitatu tu maana sitegemei kuishi zaidi. Mimi siyajui maisha haya, ninawaomba mnifundishe na mniombee. Ee!, na mimi nitawaombea kidogo kidogo.” Baada ya kukaa miezi mitatu, jioni ya tarehe 7 Desemba1983 akapokewa daraja la unovisi.

Siku hiyo Mhashamu Askofu Gervas Nkalanga akabadili jina na kuacha vyeo vyote vya kiaskofu, akachagua kuitwa Frater Placidus, OSB, jina la mmoja wa wanafunzi wa kwanza wa Mt. Benedikto, walio pia walinzi wa Abasia ya Hanga. Akakabidhiwa kwa Mlezi wa wanovisi Frt. Basil Ngaponda OSB, na kuingizwa mara moja katika kundi la Wanovisi wenzake vijana wadogo saba. Akaanza taratibu kufanya mazoezi ya kiroho na ya kutumikiana. Kutokana na afya yake ilibidi mara nyingi aende kupima afya hospitalini Peramiho. Anapokuwa utawani alishiriki kwa unyenyekevu kazi za kawaida kama kupika jikoni, kutumikia mezani, kufagia na kulima bustani. Akaingia darasani kujifunza Kanuni ya Baba Benedikto kwa bidii sana, na historia ya Wabenediktini kama Wanovisi wengine. Kutokana na kulinganisha vizuri sala na kazi, baada ya nusu mwaka wa Unovisi, akapata afya njema, na akatupa mbali mkongojo aliofika nao kwa mara ya kwanza Utawani hapo!

Baada ya mwaka mmoja na siku moja ya Unovisi akaruhusiwa kufunga Nadhiri za kwanza  akiwa peke yake. Ilikuwa ni Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, yaani tarehe 8 Desemba1984. Siku hiyo alifurahi sana kwani aliimba wimbo wa majitoleo pamoja na watawa wote. “Unipokee Ee Bwana  kama ulivyoahidi na nami nitaishi. Wala usiniaibishe katika matumaini yangu.” Wakati wa Sala ya Kanisa ukaimbwa utenzi wa Bikira Maria alioupenda wenye maneno ya nembo ya uaskofu “Iter para tutum.” Misa ya nadhiri iliongozwa na Prior Gregory Mwageni ndiye aliyepokea majitoleo ya mnovisi Frt. Plasidus, ikishuhudiwa na Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa na Askofu Yakobo Komba wa Songea. Kwa kufunga nadhiri za kibenedikti, Frt. Plasidus alifanya idadi ya Maaskofu wabenediktini wote ulimwenguni kuwa 40. Kati yao mmoja alikuwa Kardinali, maaskofu wakuu, maaskofu na maabate wakuu wa majimbo.

Baada ya nadhiri, Frt. Plasidus akaomba kupewa kuongoza idara ya kilimo cha ndizi katika monasteri. Wakubwa walisita kumpa kazi hiyo kwa kumheshimu kama Askofu, lakini mwenyewe aliomba atendewe kama mtawa mwingine yeyote, ndipo akaruhusiwa. Lakini hoja nyingine ya kusisitiza kupewa idara hiyo aliitoa miaka ya karibuni alipoulizwa, kama alikuta ndizi alipofika Songea kwa mara ya kwanza. Alijibu “Mimi sikukuta ndizi kama za Bukoba ila nilikuta ndizi mshare lakini sio mshare kabisa, ila labda ndizi mwitu.” Frt. Plasidus akaagiza aina nyingi ya mbegu za migomba na kupanda. Akaandaa pia miche mingi ya migomba na kuigawa bure kwa wanakijiji na kuwafundisha bure jinsi ya kulima migomba.

Mwaka 1986 akaagizwa kulea Wapostulanti – vijana waliokuwa wanaanza safari ya maisha ya kitawa. Akawafundisha darasani na kufanya nao kazi za nje hasa kulima migomba. Frt. Plasidus akawa pia anafanya kazi zote na kuishi mazingira yote kama watawa wengine. Hata ilipobidi watawa kwenda kukaa mashambani porini kwa wiki moja au mbili kulima ngano mlimani, au kulima mahindi huko Nakagugu, au kulima, kung’olea na kuvuna mpunga huko Ruhimba walikuwa daima pamoja. Watawa wakamzoea na kumkimbilia kuomba ushauri mbalimbali. Wakati tukitaka kuwa na Padre mtawa aliagizwa yeye kumpadrisha. Mwaka 1990 akaruhusiwa kufunga nadhiri za daima na kuendelea na idara yake ya kilimo cha migomba na kulea vijana.

Mwaka 1996 Askofu wa Bukoba Mhashamu Nestori Timanywa, aliuomba utawa kufungua nyumba ya Wabenediktini katika jimbo lake. Abate mhusika akamtuma Frt. Plasidus pamoja na watawa wawili kwenda kuanza utawa huko Nkindo Itahwa, Jimboni, Bukoba. Akafanya kazi ya kupanda migomba na kuboresha mazingira mahalia. Baada ya miaka mitatu, akaitwa kurudi Hanga na huko utawa ukaachwa mikononi mwa Padre wa Jimbo la Bukoba Fr. Renald Rutaihwa. Aliporudi tu akakabidhiwa kuwa msimamizi wa watawa Waprofesi wa muda kazi aliyofanya hadi mwaka 1999. Kisha akagizwa kulea miito ya “Mabradha” Watawa wa Jimbo la Same walioanzishwa na Askofu Lebulu aliyeomba walelewe na utawa wa Hanga.

Pamoja nao akatumwa rasmi kulea na kuwafunda vijana wadogo wa utawa huko mashambani Nakagugu km 4 toka Hanga. Akapewa kitendea kazi, gari aliloliendesha mwenyewe hadi siku za hivi karibuni. Frt. Plasidus akajisadaka maisha yake katika kulea vijana. Akawajengea mabweni, akawajengea Kanisa zuri lililobarikiwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Akatengeneza barabara na kujenga madaraja. Katika bonde kubwa la Nakagugu akalima ndizi, ndizo sehemu moja wapo ya zao la biashara kwa Monasteri na kijijiini. Akawafundisha vijana kuwatwika miche ya miti ya mbao na kupanda. Hivi karibuni alianza kujenga nyumba ya kuishi walezi, ambayo alisikitika kuiacha bila kumaliza aliposema: “Ninasikitika sana kuacha nyumba bila kumaliza kuijenga, natumaini itabaki bila kumalizia kama ilivyobaki nyumba aliyoanza kujenga Frt. Pirmin.”

Safari ya Frt. Plasidus utawani imedumu miaka thelathini na tatu umri wa Yesu hapa duniani badala ya miaka mitatu aliyotabiri mwenyewe alipofika. Umri wa mtu mzima, akionesha uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya kitawa yanayofumbata: Sala na Kazi; maisha ya pamoja na huduma kwa familia ya Mungu. Ameonesha ari na moyo wa kutaka kulitegemeza Kanisa na taifa kwa njia ya kazi inayotekelezwa kwa bidii, juhudi na maarifa; uadilifu na uchaji wa Mungu. Wanakijiji wa Hanga na vijiji vingine watamkumbuka Frt. Plasidus wanapopata kipato cha ndizi alizowafundisha kulima. Baadhi ya watu wanasema, kwa hakika hata ndizi zilizokuwa zinazalishwa kwenye shamba alilokuwa analishughulikia hata katika uzee wake zilikuwa ni tamu! Wengi watazikosa!

Utume wa maisha ya Ubenediktini ni kutoa ushuhuda wa maisha kama moyo unavyofanya kazi kubwa mwilini lakini hauonekani kwa nje. Ameushuhudia wito na maisha kitawa; aliwavuta mapadre wa Jimbo zaidi ya watatu kujiunga na wabenediktini kutoka ndani na nje ya nchi. Ni dhahiri amewafungulia mlango pia Maaskofu kuingia utawani. Anasifiwa kwa fadhila ya unyenyekevu na unyofu na roho ya kutumikia kwa upendo kama alivyozoea kusema “utawani hatuishi kwa maslahi bali tunatafuta fadhila.” Hali yake ya afya ilikuwa nzuri ila mara chache sana alienda kupima afya kwa daktari wake binafsi huko Dar es Salaam. Miaka ya karibuni akapata vidonda katika mguu wake wa kulia akaenda KCMC Moshi kwa uchunguzi na kupata matibabu. Baada ya kupata nafuu kidogo akarudi utawani akipitia kumwona rafiki yake Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha na watawa wa Jimbo katoliki la Same. Tarehe 14 Desemba 2015 alirudi Hanga. Akakaa siku mbili tu ndipo siku ya Jumanne akaanza tena kujisikia vibaya.

Siku ya jumatano usiku alishikwa na “ Kwikwi” iliyopelekea akimbizwe Hospitali ya Mt. Yosefu Peramiho. Kabla ya kupelekwa huko aliomba Sakramenti ya Kitubio na Mpako wa Wagonjwa. Baada ya waganga kumshughulikia kumpa matibabu siku ya Ijumaa asubuhi alionekana kupata nafuu. Kila mwanya aliojisikia nafuu alitumia kusali. Saa kumi na nusu jioni hali ilibadilika ghafla BP ikashuka sana. Baada ya Waganga na wauguzi kumshughulikia PB ikapanda taratibu. Saa kumi na mbili jioni alianza kusali Rosari na saa moja ya jioni alisali sala inayosaliwa Wabenediktini kila baada ya saa moja. “Ee Yesu mwema, usiwe mwamuzi wangu, bali mwokozi wangu. Maria mama wa neema mama wa huruma unisimamie ukanipokee saa ya kufa, Yosefu mtakatifu uliyefaulu katika yote, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja nawe. Bwana uibariki kazi yetu na yote kwa ajili yako, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.” Baada ya sala hiyo akafumba macho na kulala usingizi wa amani. Ilikuwa Saa 7:45 jioni. Hivi ndivyo alivyomaliza safari yake hapa duniani aliyoianza miaka 96 iliyopita. Watawa tunamshukuru Mungu aliyeangalia unyonge wetu kwa kutupa heshima ya kuwa na mtawa mtakatifu kama Frt. Plasidus. Kwa njia ya Frt. Plasidus, Kanisa lote ulimwengu na watu wa taifa letu sasa wanajua Hanga ni wapi, na watawa wake wanatoa mchango upi katika Kanisa na taifa.

Tunatoa Shukrani kwa wote waliomsindikiza katika safari yake ya maisha, katika uzima na ugonjwa, hususani waganga na wauguzi wakiwa Dr. Munseli, Dr. Kibasa (marehemu), Dr. Lemmy Lugumyameto  na Mke wake Mama Lemy, Dr. Tonya, Dr. Sr. Asante OSB, Wauguzi Sr. Amana OSB, Sr. Bernarda Hyera OSB na masista wote wa Tutzing Peramiho, Watawa wa Abasia ya Peramiho pamoja na wote mliojitolea kuokoa maisha yake. Mungu awabariki sana.Tunawashukuruni wazee wa urika wake wa uaskofu mliofika kumsindikiza mwenzenu. Asante Makasisi wote, watawa wenzake Waume kwa Wake, na Waseminari, Makatekista na Waumini wote mliofika kutuzika. Tunawashukuru kwa dhati ya moyo viongozi wengine wa dini mliofika. Asante wanakijiji wenzetu wa Hanga ambao daima tupo pamoja katika raha na dhiki kwa kufika kwa wingi kumwaga baba na mfadhili wetu.

Shukrani za dhati ziwaendee viongozi wa Serikali mliofika kututuliza. Tumezoea kupata ugeni wa serikali wakati wa sherehe tu au matukio ya kimaendeleo. Mwaka 1969 tulijiwa na Rais Julius Nyerere aliyefika kushuhudia tunavyoishi kijamaa pamoja na wananchi hapa Hanga. Mwaka 2001 tulijiwa na Rais Benjamin Mkapa kwa Siku kuu ya mtoto wa Afrika. Tulijiwa pia na Waziri mkuu Edward Lowassa. Lakini leo kwa tukio la msiba huu mzito tunafikiwa na viongozi wa serikali ili kutuauni. Asante sana na Mungu awabariki.

Nyote mmeshuhudia mtawa huyu alivyotoa ushuhuda wa jinsi bora ya kufanya safari katika maisha na mapato yake katika taifa. Tunaona uchungu uliochanganyika na furaha tele kwani mwenzetu amemaliza safari yake salama. Sasa anastahili kupumzika, kama ilivyo katika utamaduni wa kabila lake, kwamba mzee wa umri hafi bali amepumzika: “Wataya.” Nasi tunasema “mzee amepumzika.”  Wataya!

Imetolewa na Abate na Watawa wa Abasia ya Mt.Mauro Hanga, Desemba 2015.








All the contents on this site are copyrighted ©.