2015-12-16 09:08:00

Amani ya kweli inafumbatwa katika huruma, upendo na mshikamano wa dhati!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016 unaoongozwa na kauli mbiu shinda kutojali ambata amani ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata moyo wa huruma ya Mungu ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, kila mtu anatekeleza wajibu wake ili huruma, amani, upendo na mshikamano viweze kutawala katika maisha na nyoyo za watu katika medani mbali mbali za maisha.

Kardinali Peter Turkson ameyasema haya wakati wa kuwasilisha kwa waandishi wa habari, Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 49 Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016. Baba Mtakatifu anawahamasisha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha huruma, upendo na mshikamano kwa maskini, watu wasiokuwa na fursa za ajira, wanyonge, wafungwa, wakimbizi na wagonjwa. Umoja na udugu viwe ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Familia ya Jumuiya ya Kimataifa. Dhamana hii inaweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa kuwajali watu wanaoteseka na vita, kinzani na majanga asilia; kwa kufuta deni la nje kwa nchi maskini zaidi duniani na mwishoni kujenga na kudumisha sera na mikakati ya ushirikiano wa kimataifa inayoheshimu tunu msingi za wananchi mahalia pasi na kukumbatia utamaduni wa kifo na ukiukwaji wa kanuni maadili na utu wema, kama sehemu ya masharti ya upatikanaji wa misaada.

Kwa upande wake, Dr.  Flaminia Giovanelli, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la kipapa la haki na amani amegusia kwa kina na mapana mwendelezo wa Mafundisho ya Viongozi wakuu wa Kanisa katika masuala ya haki, amani na ushirikiano wa kimataifa; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha, utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi. Haya ni mambo yanayodhalilisha utu wa binadamu na ni chanzo cha hali ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia uhusiano kati ya binadamu na mazingira na kwamba, pale ambapo binadamu ameshindwa kulinda na kutunza mazingira madhara yake yamekuwa ni makubwa kiasi cha kuhataraisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii. Huu ni mwelekeo wa watu kutojali wala kuwajibika na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, lakini, madhara yake hayachagui wala kubagua! Hizi ni dalili za ubinafsi na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuambata huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Tabia ya ukanimungu inahatarisha kwa kiasi kikubwa amani, usalama na mafungamano ya kijamii kwani binadamu anapenda kujikuza na kusahau kwamba, ni kiumbe na anapaswa kutambua nafasi na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Pale Mungu anapowekwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, hapo mwanadamu anakumbana na ukatili wa hali ya juu anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Watu wanapaswa kutenda mintarafu haki msingi za binadamu ili kuambata amani ya kweli.

Mtakatifu Yohane Paulo II anakumbusha kwamba, hakuna amani pasi na haki wala amani pasi na msamaha. Baba Mtakatifu Francisko anaunganisha yote haya na kusema: haki na amani; msamaha na upatanisho; huruma na mshikamano ni mambo msingi katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kukombolewa kutoka katika mambo yanayo kwamisha mchakato wa haki na amani. Huruma ni kiini cha habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya Mwenyezi Mungu, mwamini anaalikwa kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha yake ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.