2015-12-10 09:21:00

Watawa iweni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili iliyoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 8 Desemba 2015 imekuwa na maana ya pekee kabisa kwani Kanisa limeadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha maadhimisho ya Mtaguso wa Pili, Kanisa likatoka kifua mbele ili kujenga madaraka ya kukutana na watu, tayari kuamsha ari na moyo wa kimissionari unaojikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!

Tarehe 8 Deseamba 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukumbatia huruma ya Mungu katika maisha yao. Huruma ya Mungu ni muhtasari wa maisha na utume wa Kanisa ni sifa kuu ya Mungu inayomwambata mwanadamu katika historia ya maisha yake.

Waamini kwa kupitia Lango kuu la Jubilei watambue kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na Wasamaria wema wa huruma ya Mungu kwa jirani zao. Hii ndiyo changamoto hata kwa watawa sehemu mbali mbali za dunia walioweka nadhiri zao za kwanza au kufunga nadhiri za daima katika mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume. Nchini Tanzania, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma ameongoza Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya watawa waliokuwa wanaweka nadhiri zao za kwanza kutoka katika Shirika la Masista wa Immakulata, Miyuji, Jimbo kuu la Dodoma.

Askofu mkuu Kinyaiya amewataka watawa nchini Tanzania kuhakikisha kwamba, wanamuiga Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili kwa kuishi kikamilifu nadhiri ya utii, usafi kamili na ufukara kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu sanjari na huduma makini kwa jirani. Watawa wawe watii kwa Mungu na kwa viongozi wao halali wa Mashirika; wajitahidi kusimama imara katika nadhiri za usafi na ufukara na kamwe wasikubali kukengeuka na kumezwa na malimwengu.

Watawa wamwendee Bikira Maria wakati wa furaha, shida na mahangaiko yao ya ndani; waweke matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Watawa hawa wangeweza kuwa kweli ni wanawake wa shoka katika familia zao, lakini wameamua kuacha yote kwa ajili ya kumtumikia Mungu, Kanisa na jirani, wawe waaminifu kwa nadhiri ya usafi kamili. Wazazi na walezi waendelee kuwasaidia watoto wao kwa kuwaombea na kuwapatia nafasi ya kuweza kuishi kikamilifu utawa wao bila ya kuwa na mashinikizo kutoka ndani ya familia, mambo ambayo wakati mwingine yanawapelekea watawa kukengeuka na kutumbukia katika malimwengu na huko wanakutana na cha mtema kuni: patashika nguo kuchanika!

Watawa wawe ni wahudumu wa Injili na vyombo makini vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na mwaka wa Watawa Duniani. Jimbo kuu la Dodoma litafungua lango kuu la Jubilei ya huruma ya Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, yaani hapo tarehe 13 Desemba 2015 majira ya saa moja kamili asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Watawa waliowekwa nadhiri zao za kwanza katika Shirika la Bikira Maria Immakulata, Miyuji, Jimbo kuu la Dodoma ni Sr. Maria Gaudia, Sr. Melania Mushi  Sr. Lucy Muzuba, Sr. Rosaria Mlimi, Sr. Sabina Mnyeka pamoja na Sr. Winfrida Maduhu.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, Makamu Askofu Jimbo kuu la Dodoma na Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, tarehe 8 Desemba 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili la Ivrea. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu Masista kumi na mmoja wameweka nadhiri zao za kwanza, tayari kumshuhudia Kristo aliyekuwa: mtii, fukara na msafi kamili.

Padre Msaga amewataka watawa hawa kuwa waaminifu kwa nadhiri zao, huku wakiendelea kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, tayari kuishuhudia kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watambue kwamba, wameanza rasmi safari ya maisha na utume wa kitawa katika mapambazuko ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na mwendelezo wa Mwaka wa Watawa Duniani.

Masista walioweka nadhiri zao za kwanza ni: Sr. Janet Aoko Omundo, Sr. Dokras Atieno Okite, Sr. Aldegunda Augusti Mshanga, Sr. Elizabeth Patrice Roche, Sr. Rose Kunzugala Luwagila, Sr. Janet Bosibori Yamao, Sr. Anastasia Aloyce Mtunya. Wengine ni Sr. Rebecca Auma Sidere; Sr. Ester Lepasher Mollel, Sr. Demetria Caroli Shayo pamoja na Sr. Quuenter Atieno Omwanda.  Mama mkuu wa Shirika hili Sr. Palma Porro anawatakia heri na baraka watawa hawa wanapoanza safari ya maisha na wito wao wa kitawa ndani ya Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria mkingiwa dhambi ya Asili.

Na habari zaidi kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania, zinasema kwamba, Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya katika Ibada ya maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili na mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu, watawa kumi na wawili wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume, Mbeya wamefunga nadhiri za daima. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya.

Masista walioweka nadhiri zao za daima ni pamoja na: Sr. Liebaratha Mgalla, Sr. Annamaria Mboya; Sr. Hilda Mwakyelu, Sr. Yusta Nyumbanitu; Sr. Filomena Mwalyego, Sr. Cesilia Ntongolo na Sr, Serafina Menda. Wengine ni Sr. Aloyce Aloyce, Sr. Editha Hasunga, Sr. Josephina Mbawala, Sr. Wema Kabigi pamoja na Sr. Rosemary Uledy. Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya amewataka watawa walioweka nadhiri za daima kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na mapendo ya Mungu kwa maskini, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hata hawa wanapaswa kutangaziwa Injili ya huruma, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Rodrick Minja, Dodoma na Thompson Mpanji, Mbeya, Tanzania.

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.