2015-12-10 16:04:00

Burundi yakataa usuluishi wa Umoja wa Afrika


Serikali ya Burundi imeuwekea Umoja wa Afrika kizingiti kwa kukataa kuuhusisha katika mchakato wa kutafuta amani ya kudumu kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea kufuka moshi kiasi hata cha kutishia kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Umoja wa Afrika ulikuwa umemtuma Rais Thomas Yayi Boni wa Benin kwenda Bujumbura, Burundi kuangalia uwezekano wa Umoja wa Afrika kuanzisha mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na vyama vya upinzani, lakini Rais Pierre Nkurunziza akakataa kukutana na Rais Thomas Yayi Boni, lengo lilikuwa ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya amani unaoendelezwa kwa sasa na Serikali ya Uganda.

Tangu mwezi Aprili, 2014 Burundi imejikita ikitumbukia katika mpasuko wa kisiasa pale ambapo Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kugombea na hatimaye kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Burundi hivi karibuni, kinyume cha Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni Sheria Mama. Lakini Burundi inaendeleza pia majadiliano kati yake na Umoja wa Ulaya unaoitaka Burundi kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha haki msingi za binadamu.Ikiwa kama Burundi haitatekeleza dhamana na wajibu wake barabara iko hatarini kuwekewa vikwazo vya uchumi, ambavyo wengi wanasema, watakaoathirika zaidi na raia wa kawaida kama ilivyo pia kwa nchi nyingi ambazo zimewekewa vikwazo vya uchumi!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.