2015-11-30 11:47:00

Papa atembelea hospitali na kuwafariji watoto wagonjwa!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili jioni tarehe 29 Novemba 2015, kabla ya kwenda kuadhimisha uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati aliwatembelea watoto wagonjwa kwenye Hospitali ya watoto Bangui. Lango la Jubilei ya huruma ya Mungu ni; lango la haki, ambamo waamini wanapita kumtolea Mungu sifa na shukrani; lango la Bwana wanamoingia wenye haki; lango la Nyumba ya Mungu ambamo waamini wanakwenda kumwabudu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Uso wa huruma Misericoriae vultus anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufungua macho na mioyo yao ili kuona machungu ya ulimwengu; majereha ya ndugu na jirani wanaonyimwa hadhi yao kama binadamu. Huu ni mwaliko wa kusikiliza kilio chao ili hatimaye, kubomoa kizingiti cha kutojali, unafiki na majigambo. Ni mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa Hospitali hapo anasema Padre Federico Lombardi msemaji wa Vatican kwamba, alitoa zawadi ya dawa alizokuja nazo kutoka Vatican kama mchango wake katika mchakato wa tiba kwa watoto wadogo. Anakumbusha kwamba, uamuzi huu umefanywa na Baba Mtakatifu mwenyewe na wala haukuwa kwenye ratiba ya siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.