2015-11-30 15:27:00

Historia fupi ya maisha ya kitawa ndani ya Kanisa!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tukiwa ndani ya mwaka mpya wa Kanisa tunakusalimu tukisema, Tumsifu Yesu Kristo. Pamoja na maadhimisho mbalimbali yanayendelea kwa wakati huu ndani ya Kanisa, hatutasahau kwamba tumo pia katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa duniani, utakaohitimishwa hapo tarehe 2 Februari 2016. Katika kipindi kilichopita tulikuahidi kuangazia vipindi mbalimba vya ukuaji wa maisha ya Kitawa katika Kanisa. Kwa vile historia ni ndefu sana, kwa uchache tutafuata dhamira mtazamo wa jumla tu wa vipindi hivyo vya historia. 

Tukumbuke kwamba, mwanzoni kabisa, ilikuwa ni juhudi ya watu binafsi kuyaambata maisha hayo ya kitawa huku wakifuata mashauri ya injili ili kujikamilisha katika Ukristo wao. Na polepole baadaye, wale tuliosema waliishi katika upweke huku wakisali na kujinyima, walijipatia wafuasi ambao walipenda kuwa nao katika  maisha ya aina hiyo, na hivyo wakaaza kuunda aina kama jumuiya na mwanzilishi wa jumuiya alikuwa mmoja kwa mmoja ndiye ndiye mkuu. Ndivyo walivyoanza watakatifu Pacomi au Antonius, Mababa wa Jangwani.

Wachambuzi wa Historia wanatuonesha kwamba kuna hatua kuu nne ambazo zilizaa mitindo mipya zaidi, hasa upande wa Magharibi. Kwanza kabisa tunaona kuwa hadi karne ya XII ulitawala mtindo wa kimonaki ukifuatwa na ule wa kikanoniki, wao waliishi katika Jumuiya na kusali pamoja wakiwa chini ya Kanuni maalumu ya maisha iliyojisimika katika mashauri ya Injili. Kati ya karne ya XIII hadi ya XV yalitokea mashirika ya waombaji. Hawa walijiambua kabisa na mali, wakajitoa kumtumikia Mungu kwa mtindo wa pekee katika ufukara, huku wakimshuhudia Kristo fukara anayeshiriki maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Pamoja nao wapo pia wa-Domonikani walioanzishwa na Mtakatifu Dominiko. Hawa walijitoa kwa ajili ya kutangaza Neno la Mungu (yaani wahubiri) na kuungamisha. Shughuli ambayo wanaitenda hadi leo. Hivyo walijiambua kabisa na mali ili muda wote watekeleze wajibu huu mzito ndani ya Kanisa.

Kati ya karne ya XVI hadi ya XIX yalitokea mashirika mengi ya wakleri wenye kanuni maalumu ya maisha, wenye lengo lilelile la kuihubiri Injili. Sambamba nayo, yalitokea pia mashirika ya  maisha ya kitume na ya watoahuduma mbalimbali ndani ya Kanisa, kama vile  Mtakatifu  Ignasi wa Loyola. Na mwisho kabisa katika karne ya XX ambayo imetusogeza hata nyakati zetu hizi kumekuwepo na mashirika ya kiulimwengu na aina mpya ya mtindo wa maisha ya Kitawa. Wote hao wanaitika wito wa Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa, na wanatekeleza utume ndani ya Kanisa.

Kama tulivyowahi kusema, pale mwanzoni kabisa, maisha ya kitawa yalianza kwa juhudi binafsi tu, katika kujikamilisha katika maisha ya Kristo. Hivyo tunakuta kulikuwa na Ubikira Mtakatifu, wale wanawake walipenda kuishi maisha ya usafi mtakatifu kwa mfano wa Mama yetu Bikira Maria. Walikuwapo pia wanaume walioshi hali hiyo ya useja kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Na baadaye huko Misri, yalianza maisha ya Umonaki, uliokuwa na sura ya kuyakimbia malimwengu, ambapo baadhi ya watu, kwa kuchochewa na moto wa Injili, waligawa mali zao zote kwa masikini, wakawaacha ndugu na jamaa, wakaenda kuishi peke mahali pa utulivu jangwani, kusali, kufunga, kufanya toba na kumtafakari Mungu.

Mmonaki alitafuta upweke kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu, bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida ili moyo uweze kutulia kabisa na kumpenda Mungu bila ya kugawanyika. Miundo mipya ya umonaki ilitegemea mambo makubwa matatu yaani mwanzilishi, kanuni, upweke. Mtindo huo wa maisha ulisitawi zaidi baada ya dola ya Kirumi kuruhusu Ukristo kunako mwaka 313. Na kwa sasa wachambuzi wa masuala ya historia ya Umonaki wanatuambia, mtindo huu wa Maisha ambao ulianzia Afrika,  ndio mchango mkuu wa Afrika mintarafu maisha ya kitawa kwa Kanisa zima.

Anayetazamwa kama mwanzilishi wa mtindo huo wa maisha ya Kimonaki ni Mt. Anthoni Abate (251-356) ambaye kishaangazwa na maneno ya Injili  aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa ili awe huru kabisa kumfuasa na kumtumikia Mungu. Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi sehemu mbalimbali, naye Anthony aliwaongoza bila ya kuacha upweke wake. Maisha magumu ya makundi hayo yaliamsha Kanisa lifuate Injili kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ambapo ulihitajika ujasiri wa pekee hata mbele ya kifo.

Hivyo umonaki ulionekana aina mpya ya kifodini kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote. Wamonaki wale walijitoa kwa hali na mali, kufa na kupona, kumshuhudia Kristo na Injili yake hata katika hali ngumu sana. Na kwa sababu hiyo, wamonaki wamekuwa na mchango wa pekee sana katika usitawi wa Kanisa. Na kwa mtindo wa maisha yao, hadi leo watawa hawa wanaendelea kuwa wapiganaji wa kiroho, hazina ya Kanisa, mashuhuda wa imani tendaji na wahudumu ya mashauri ya Injili ya Kristo.

Tusikilizane tena kipindi kijacho. Kukuletea maneno haya ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, Mmonaki wa Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa Sumbawanga – Tanzania.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.