2015-11-29 07:17:00

Utambulisho na wito wenu unajikita katika huduma makini kwa watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 28 Novemba 2015 amekutana na kusali pamoja na Wakleri, Watawa na Majandokasisi kutoka Uganda kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Jimbo kuu la Kampala. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amegusia mambo makuu matatu: utambulisho wa Kipadre; umuhimu wa kujibidisha zaidi pamoja na kutoa ombi maalum kwa ajili ya Burundi ambayo kwa sasa inapitia kipindi kigumu sana katika historia yake.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakleri, Watawa na Majandokasisi nchini Uganda kutafakari kwa kina kuhusu utambulisho na wito wa Kipadre unaopaswa kujidhihirisha kwa njia ya huduma inayokita kwenye fadhila ya unyenyekevu. Kanisa nchini Uganda limejengeka chini ya msingi wa ushuhuda wa upendo kwa Yesu Kristo uliotolewa na waamini walei, makatekista, mapadre na watawa. Hapa wanapaswa kukumbuka kwamba, jibu lao la ndiyo kwa Kristo linawaambata waamini wanaowahudumia pamoja na kuhakikisha kwamba, malango ya Makanisa yawe wazi, lakini malango ya mioyo yao yanapaswa kuwa wazi zaidi kwa ajili ya kuwapokea Watu wa Mungu wanaobisha hodi kila siku.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri, Watawa na Majandokasisi kujibidisha zaidi katika mchakato wa maboresho ya maisha yao na kamwe wasiridhike na kiwango cha maisha na huduma walichofikia. Waendelee kujibidisha katika kutafuta maisha bora zaidi, haki, amani, msamaha na upatanisho. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake nchini Burundi ambako hali inaendelea kuwa tete kila kukicha. Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kusali kwa ajili ya Burundi, ili Mwenyezi Mungu aweze kuamsha tena ndani ya akili na mioyo ya viongozi na jamii katika ujumla wake, wazo la majadiliano na ushirikiano; amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri, Watawa na Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wito wao kwa kuachia nafasi nguvu ya Mungu ili iweze kutenda kazi kwa njia yao, lakini zaidi kwa kutoa nafasi kwa huruma ya Mungu iweze kuwagusa na kuwaponya waja wake. Huruma ya Mungu iwatendee wao kwanza kabla ya kuipeleka kwa wengine, hususan wale walioko pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, jambo hili si rahisi sana kutekelezeka kwani inaonekana kana kwamba watu wana mambo mengi ya kufanya na vipaumbele vya kutekeleza. Haya ni mambo yanayosumbua dhamiri, tabia na jinsi ya kufikiri na matokeo yake ni kutumbukia katika mchoko wa maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, wito wa Kristo Yesu ni wito unaofumbata furaha na huduma; mambo yanayopaswa kububujika kutoka katika sakafu ya mihimili ya Uinjilishaji. Baba Mtakatifu analipongneza Kanisa nchini Uganda kwa kuwa na idadi kubwa ya miito inayopaswa kulindwa na kuendelezwa zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake iliyoandikwa na baadaye kuwapatia Maaskofu  wa Uganda ili waweze kuisambaza kwa wakati muafaka amesema, analiona Bara la Afrika kuwa ni chemchemi ya matumaini yanayoambata neema ya Mungu kati yao. Anawaalika kusali kwa ajili ya kuombea mchakato wa Uinjilishaji, ari na moyo wa kitume, kwa kuwa na moyo wazi ili kujibu kilio cha familia ya Mungu inayowazunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.