2015-11-29 16:44:00

Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini akutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko akiwa Jijini Kampala, tarehe 27 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini. Padre Lombardi anasema, mazungumzo haya yanaonesha matumaini kwa Sudan ya Kusini moja ya mataifa machanga kabisa Barani Afrika kujipatia uhuru wake kunako mwaka 2011 kuanza tena safari ya haki, amani na upatanisho wa kweli.

Katika kipindi cha miaka mitano tangu Sudan ya Kusini ijipatie uhuru wake, kwa bahati mbaya, wananchi hawajawahi kuona amani na utulivu katika maisha yao, daima vita imekuwa ipamba moto kutokana na uchu wa mali na madaraka. Serikali na viongozi wa upinzani walikuwa wametiliana sahihi Mkataba wa Amani huko Arusha, Tanzania, lakini hadi sasa Mkataba huu haujaheshimiwa na kila upande unamshutumu mwingine kwa kutokuwa waamini kwa mkataba huo. Mkataba ulipania pamoja na mambo mengine kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambayo hadi sasa haijaundwa. Kumbe, bado kuna matumaini kwamba, viongozi wa Sudan ya Kusini watajikita tena katika mchakato wa majadiliano, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.