2015-11-29 09:00:00

Papa asante kwa Mwaka wa Watawa na Waraka wa Utunzaji bora wa mazingira!


Askofu John Bapist Kaggwa, Mwenyekiti wa Tume ya Malezi kwa Mapadre na Watawa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, Jumamosi, tarehe 28 Novemba 2015 wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Wakleri, Watawa na Majandokasisi wa Uganda, alimwambia kwamba, katika mkutano wake, kulikuwepo pia wajumbe kutoka katika nchi za AMECEA na kwa namna ya pekee Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na ujumbe wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si; maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani pamoja maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa Mapadre na Watawa kuwa kweli ni vyombo na wajumbe wa huruma ya Mungu kwa waja wake; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu bila kusahau tunu bora za maisha ya ndoa na familia.

Kwa upande wake Padre Mathew Okun- Lagoro, Rais wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Uganda, UNDIPA amesema ujio wa viongozi wakuu nchini Uganda daima limekuwa ni tukio la neema na baraka kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Uganda. Kwa mara ya kwanza Uganda ilipata Mapadre wazalendo kunako mwaka 1913. Hawa ni Padre Victor Mukasa na Padre Basilio Lumu. Hawa ni Mapadre wazalendo wa kwanza kabisa kupewa Daraja Takatifu Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tangu wakati huo wito wa maisha ya Kikristo, Kipadre na Kitawa umeongeza maradufu nchini Uganda.

Umoja wa Watawa Uganda kwa kifupi, ARU, ulianzishwa kunako mwaka 1968 ili kuwasaidia watawa kutekeleza dhamana na wito wao katika Makanisa mahalia, kwa kumwilisha karama za mashirika yao katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi mintarafu tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Wanatelekeza utume wao katika sekta ya elimu, afya, katekesi, huduma za kijamii na Ibada. Watawa wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wataendelea kuwa mashuhuda wa Injili ya furaha katika huduma.

Majandokasisi wamemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kuendelea kuwasaidia kwa hali na mali. Kanisa Katoliki nchini Uganda lina Seminari kuu sita zenye Majandokasisi 1,248. Wanashukuru malezi na majiundo makini wanayopata Seminarini na kwamba, wanaendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.