2015-11-29 08:10:00

Kiteni maisha yenu katika kumbu kumbu endelevu, uaminifu na sala!


Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na Wakleri, Watawa na Majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Jimbo kuu la Kampala, Uganda, Jumamosi jioni alimpatia Askofu John Baptist Kaggwa hotuba aliyokua ameandaa kwa ajili ya tukio hili na kuanza kutoa katekesi kuhusu maisha na wito wa Kipadre na Kitawa ndani ya Kanisa. Amekazia kwa namna ya pekee kabisa kumbukumbu; uaminifu na sala; mambo msingiĀ  kabisa katika umwilishaji wa utambulisho wa kikuhani unaojikita katika huduma.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakleri, Watawa na Majandokasisi kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie neema ya kumbu kumbu, ili kutambua ushuhuda wa imani uliotolewa na Mashahidi wa Uganda, ili waendelee kukua na kushamiri katika maisha na wito wao, tayari kuyatolea ushuhuda wenye mashiko na mvuto kama sehemu ya mchakato wa changamoto endelevu. Kanisa nchini Uganda halina budi kuendelea kuwa alama ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuendeleza utukufu ulioshuhudiwa na Mashahidi wa Uganda kwa sasa na kwa siku za baadaye.

Mihimili ya Uinjilishaji anakaza kusema Baba Mtakatifu inapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani kama ilivyokuwa kwa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ili kutekeleza dhamana hii, kuna haja kwa Mapadre na Watawa kuwa waaminifu kwa wito na utume wao ndani ya Kanisa, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu kama Wamissionari. Wawe wepesi kuona mahitaji ya Kanisa nchini Uganda, tayari kwenda kusaidia mahali ambapo kuna uhaba wa Mapadre au Watawa, ili Kanisa liendelee kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wamissionari wa Shirika la Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta kwa uaminifu wao kwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani huko ndiko wanakomhudumia Kristo Yesu kwa njia ya ushuhuda wa upendo. Mihimili ya Uinjilishaji, iwe tayari kujipyaisha katika maisha, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka kila kukicha! Vinginevyo hazina ya mashuhuda wa imani Barani Afrika itawekwa kwenye jumba la makumbusho.

Mapadre wawe ni wahudumu wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wao. Majimbo yaendelee kushirikishana rasilimali watu na nguvu kazi, ili Kanisa nchini Uganda liendelee kushamiri katika ari na mwamko wa kimissionari. Uaminifu unadumishwa pia katika maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu. Mapadre na watawa wanaoshindwa kusali kwa kisingizio cha kuwa na kazi nyingi, watambue kwamba hapo wanaanza kupoteza chachu ya uaminifu wao.

Mapadre na watawa wawe wepesi kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho pamoja na kujitahidi kuacha maisha ya undumila kuwili. Pale wanapotumbukia katika dhambi, wakimbilie huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, hata katika maisha yao bado wanaweza kuogelea katika dhambi. Mashuhuda wa imani walioimarisha msingi wa Kanisa la Uganda wawasaidie kusonga mbele kwa kuendeleza kumbu kumbu, uaminifu na maisha ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.