2015-11-28 09:43:00

Yale yaliyotabiriwa, kimbembe chake chaanza kuonekana!


Kuna jambo moja hapa duniani ambalo binadamu ana uhakika nalo kwa asiliamia miamoja kuwa haliwezi kubadilika. Watu wana uhakika kwa vyovyote kesho jua litachomoza kama ilivyokuwa juzi na jana. Uhakika huo umedumu kwa karne zote ingawaje kadiri ya maelezo ya mwana-historia Herodoto imewahi kutokea mara moja wakati wa mapigano kati ya mfalme Kyaksares wa Medi na mfalme wa Lidian Alyattes, jua lilizimika ghafla na kuwa giza totoro. Askari wakaingiwa na woga mkali wakidhani ni kiyama. Kumbe, wataalamu wa nyota – Astronomist – baadaye wakagundua kuwa jua lilipatwa, na siku hiyo ilikuwa tarehe 28 Mei 584. Kwa hiyo jua, mwezi na nyota ni mifano ya msimamo, ya uimara na ya udumifu kwa vile haiwezi kubadili mwendo wake. Kwa maana hiyo, hata siku ya kutawazwa mfalme wa Israeli aliombewa hivyo: “Ufalme wako udumu daima kama jua, kama mwezi ubaki daima. ufalme wako ujae amani na mwezi usizime.” (Zab 72:5).

Leo tutasikia utabiri wa kutisha sana wa mabadiliko ya mambo yasiyoweza kubadilika. Hebu tuone kwanza mazingira yaliyompelekea Yesu kutoa utabiri huo. Hii ni wiki ya mwisho ya Yesu kukaa hapa duniani, kwani atashikwa na kuhukumiwa kufa. Muda mwingi yuko Yerusalemu na “kila mchana anashinda hekaluni na usiku huenda kulala katika mlima uitwao wa Mizeituni.” (Lk.21:37). Anapokuwa hekaluni licha ya kufundisha, analitafakari hekalu kubwa la Yerusalemu jinsi lilivyojengwa kiufundi na wajenzi stadi wa Herode. Anazitafakari kuta za mawe ya thamani, nguzo imara zilizochongwa vizuri, sakafu ya marumaru inayong’aa na korido ndefu na pana. Anawaona mamia ya watu toka mbali na karibu wakiingia na kutoka hekaluni huku wakilistaajabu hekalu lilivyojengwa na kupambwa kwa vito vya thamani. Mshairi mmoja akalitungia utenzi hekalu hili: “Lo, Malango yenye vito, Yanameta na wazi; Kwa kugongwa na kusongwa, Mawe yake huundwa, kila mmoja na mahali pake linalingana.”

Hekalu la Yerusalemu lilikuwa ni fahari kubwa na umaana wote wa maisha ya Mwisraeli. Mfumo mzima wa kidini na siasa ya nchi vilitegemea Hekalu la Yerusalemu. Kwa hiyo, kuanguka kwa hekalu hilo ni kiyama, kwani ulimwengu usingeweza kuendelea tena.  Baada ya tafakari hiyo Yesu anaibuka na utabiri ufuatao: “Kutakuwa na ishara kwenye jua, mwezi na nyota zitatikisika.” (Lk. 21:25). Anatabiri juu ya kutikisika na kuyumba kwa vitu vinavyoonekana vidumifu na imara. Akimaanisha kuwa ulimwengu wa kidini uliojiimarisha na kujijengea mahusiano na Mungu, dini iliyochukuliwa kuwa ni imara na ya kudumu kama jua, mwezi na nyota, dini hiyo itatikisika na kuanguka. Mungu wa dini yao alikuwa wa kutisha, wa kulipiza kisasi, kumbe dini hiyo itatikisika. Kadhalika, zile sheria mbovu za kiuchumi, za watawala wanaotaka kuabudiwa walioonekana hawawezi kuanguka, sasa  wataanguka.

Mapato ya maanguko hayo: “watu watavunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu.” (Lk.21: 26). Hofu iliyopo inatokana na kuanguka kwa ulimwengu huo. Kwa vile watu walijenga maisha yao juu ya mihimili hiyo iliyodumu kwa miaka mingi. Sasa watu hao wana wasiwasi kwa vile kilichoonekana kuwa ni kitakatifu kumbe ni kibaya. Wasiwasi wa mtindo huo umewahi kuwakumba Wakatoliki kutokana na mabadiliko yaliyoletwa na Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani. Wengi wakaingiwa na wasiwasi kuwa dini imekufa. Kadhalika katika maisha ya kawaida watu wanaingiwa na woga wanaposikia kubadilika kwa chama tawala au kubadilika serikali nk.

Yesu anatabiri kuwa ni budi kutokee mabadiliko katika ulimwengu na katika mabadiliko hayo kutakuwa na kukata matumaini. Huo ni ufunuo na mwanzo wa mambo mapya kwani ulimwengu wa zamani utaanguka na kuanza upya. Yesu anasema:  “Wataona mwana wa binadamu akifika toka mawinguni” (Lk. 23: 27). Ufalme wa kinyama unaowakilishwa na sura saba za wanyama katika nabii Daniele utafifia na utatokea Utu wa binadamu na ulimwengu mpya. Kisha Yesu anaagiza mambo mawili ya kufanya yatakapotokea mabadiliko hayo: “changamkeni, mkaviiue vichwa vyenu.” Kwa kigiriki “anakupsate kai eparate tas kephalas” (Lk 21:28).

Agizo la kwanza anakupsate wamefasiri changamkeni, kumbe maana yake ni kuinuka au kunyooka yaani inukeni kama kuinuka kwa mtu mwenye kibiongo, aliyepinda mgongo kutokana na kufanya kazi ya kubeba mizigo mizito. Binadamu amepinda kutokana na kuelemewa na mizigo ya matatizo ya ulimwengu huu. Tangazo hili jipya ni taarifa kuwa sasa imetoka ruzuku ya kiinua mgongo. Tunaalikwa kujiweka tayari na tujipange kuweka vyema mahusiano yetu na Mungu. Mahali pengine ambapo Yesu anatumia neno hilo anakupsate au anakupsaiinuka – ni kwa mwanamke aliyepinda mgongo kwa miaka kumi na nane kutokana na kukandamizwa na mambo ya: kitamaduni, kimila, kishirikina na mapokeo ya kiutamaduni hata asiweze kuinuka (Lk. 13:11). Yesu anawaambia wote “jiwekeni sawa, mtapata kiinua mgongo na mtapumua tena vizuri.”

Agizo la pili ni kai eparate tas kephalas yaani, na inueni vichwa vyenu.” yaani kuangalia juu. Yatubidi kuangalia juu na kufikiria umaana wa maisha yetu. Katika biblia kuinua kichwa ni alama ya kuona jambo jema. Abraham aliambiwa: “Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini na nchi uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.” (Mwanzo 13:14). Hapo kuinua macho ni alama ya matumaini. Kadhalika Musa anainua kichwa na kuangalia nchi ya ahadi: “Bwana akasema na Musa siku hiyo, akamwambia, kwea katika mlima huu wa Abarimu, ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki.” (Kumb. Torati 32:49). Pia nabii Isaya anaialika Sioni kuinua kichwa na kutafakari watoto wake (Waisraeli) wanaorudi Yerusalemu kutoka utumwani Babeli. Hivi kuinua kichwa ili kuona mambo vizuri. Yesu anaagiza kuchangamka (kuinuka) na kuinua vichwa “kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” Lk. 21:25).

Yesu anatoa tena miongozo miwili  ya kufuata katika kuupokea ulimwengu mpya unaokuja: Mosi, “Basi, jiangalieni mioyo yenu isije ikaelemewa.” (Lk 21:34) Kwa vile moyo ni makao ya vionjo, unaweza kuchagua mambo mbalimbali yanayoupatia presha ya kuwania mitindo ya ovyo ya ulimwengu huu na kukuepusha usione mwelekeo mzuri wa maisha. Mambo yanayoweza kumpa mtu presha ni ulafi na ulevi: “Angalieni mioyo yenu isije ikaelemewa na ulafi na ulevi na maasumbufu ya maisha haya;” (Lk 21:34).

Pili, msijiachilie: kuvurugwa, kulimbikizwa na shughuli za hapa duniani. Ukweli wa ulimwengu huu wawezi kukupotosha hivi jihadhari usije ukavurugwa na mambo. Hatimaye Yesu anatuagiza kusali. “Salini” maana yake kujiweka sawa, kulingana na mawazo ya Mungu.  Ndugu zangu wengi wanadai mabadiliko katika maisha. Basi baada ya ujumbe huu wa kiufunuo, tujiandae kupokea mabadiliko yaletwayo na Yesu Kristu ajaye na ujumbe mzito unaotudai kubadili misimamo yetu binafsi iliyodumu kama jua. Heri kwa Kipindi cha  majilio, tayari kuanza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Wito ni kuambata na kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, tayari kuonesha imani tendaji!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.