2015-11-28 07:54:00

Waamini iweni mashuhuda wa imani hata nyakati za hatari, tayari kutangaza Injili


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku ya Jumamosi asubuhi tarehe 28 Novemba 2015 kwa kutembelea Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda kutoka Kanisa Anglikana. Akiwa madhabahuni hapo amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu na baadaye akasali kwa kitambo kidogo na hatimaye, kuondoka kuelekea kwenye Madhabahu ya Namgongo kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuwa ni mashuhuda wa imani; mashuhuda hasa nyakati za hatari pamoja na kujitosa kimasomasko kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Baba Mtakatifu anasema tangu nyakati za Mitume wa Yesu hadi sasa hija ya maisha na utume wa Kanisa imetekelezwa kwa namna ya pekee na umati mkubwa wa mashuhuda wa imani, waliosaidia watu kukuza ari na upendo kwa Yesu sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, wameshuhudia nguvu ya Roho Mtakatifu ikitenda kazi ndani mwao.

Hii ndiyo dhamana ambayo Wakristo katika nyakati hizi wanaalikwa kuitenda kwa njia ya uwepo wa Roho Mtakatifu kati yao; Roho ambaye ni chemchemi ya hekima na nguvu kwa wengine. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini zawadi ili wao pia waweze kuwashirikisha wengine. Kwa namna ya pekee waamini wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa imani katika nyakati za hatari kama ilivyokuwa kwa mashahidi wa Uganda. Maisha yao pamoja na vijana waliokuwa wamedhaminishwa kwao yaliwekwa hatarini. Mashuhuda wa imani walikuwa wamejenga na kukuza imani na upendo wao kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, hawakuwa tena na woga wa kumpeleka Kristo kwa wengine, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Mashuhuda wa imani hadi leo hii ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwa mashuhuda wa imani, waamini leo hii wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa mitume wamissionari ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa familia, marafiki na wale wote wasiomfahamu Kristo, hususan wale ambao pengine kutokana na sababu mbali mbali wanaweza kukataa na hata wakati mwingine kuonesha kinzani. Katika nyakati za majaribu, familia ya Mungu inapaswa kushikamana na kusaidiana kwa hali na mali; kwa kulindana pamoja na kusindikizana ili kuweza kufikia utimilifu wa maisha. Huu ni mwaliko wa kuwa wakweli na wa wazi kwa wengine kwa kuanzia ndani ya familia na katika nyumba zao.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, kutoka kimasomaso maana yake ni kwamba wanaitwa kutoka ili kuwaendea wengine, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Hakuna sababu ya kuchakaza viatu ili kwenda mbali kwa ajili ya kutangaza Injili kama Wamissionari, bali kufungua macho, akili na mioyo kwa ajili ya kujibu kilio cha jirani zao wanaokutana nao katika jamii zao. Mashahidi wa Uganda wanaonesha njia kwani imani yao ilimwilishwa katika matendo kwa ajili ya mafao ya wengine bila kumsahau Mfalme Mwanga mwenyewe aliyewahukumu adhabu ya kifo kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema uaminifu kwa Mwenyezi Mungu haupunguzi kwa namna yoyote ile utunzaji bora wa ulimwengu huu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na wala si kama wapita njia wanaokaza uso wao kuelekea kwenye maisha ya mbeleni! Maisha ya hapa duniani iwe ni fursa ya kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kuendelea kushirikiana na wengine kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na kujenga Jamii inayokita katika haki na usawa. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake katika Ibada hii ya Misa iliyokuwa imefurika watu kutoka ndani na nje ya Uganda kwa kusema kwamba, kumbu kumbu ya mashuhuda wa imani ni changamoto ya kuendelea kumshuhudia Kristo katika medani mbali mbali za maisha: majumbani, kwa majirani, katika maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.