2015-11-28 16:25:00

Utume wa vijana nchini Uganda ni moto wa kuotea mbali!


Vijana kabla ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kololo wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya majaribio ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayofanyika Jimbo kuu la Cracovia, Poland, kunako mwaka 2016. Vijana wamesali, wameimba na kutoa shuhuda mbali mbali katika maisha na utume wa vijana ndani ya Kanisa na katika jamii kwa ujumla wake.

Wamesikiliza katekesi kuhusu umuhimu wa ushuhuda pamoja na kusomewa muhtasari wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Vijana Kijimbo kwa mwaka 2015. Siku hii imekuwa ni siku ya kusherehekea zawadi ya maisha na ujana. Pamoja na mambo mengine wasemali sala ya Mtakatifu Faustina kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, ili awawezeshe vijana kuwa na huruma kwa kuguswa na mahitaji ya jirani zao; kuwa na huruma wanapozungumza na vijana wenzao; kuwa na huruma pamoja na faraja kwa watu wanaoteseka; kuwa mikono yenye huruma kwa ajili ya kutenda matendo ya huruma; kuwa na huruma ya kuweza kuwasaidia jirani zao pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Askofu Paul Ssemogerere, Mweyekiti wa Tume ya Waamini Walei Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda amemwelezea Baba Mtakatifu kazi na huduma inayotolewa na tume yake kwa familia ya Mungu nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na kuratibu vyama na mashirika ya kitume miongoni mwa waamini walei; kutoa malezi, mafunzo na majiundo kwa wanachama ili waweze kutekeleza dhamana yao barabara kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ndani na nje ya Uganda.

Katika miaka ya hivi karibuni, Utume wa waaamini walei umejikita katika kuwahamasisha waamini walei kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha, imani, mapendo na matumaini kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Wameendelea kuimarisha umuhimu wa utawala bora, mafunzo kuhusu maadili na utu wema; tunu msingi za maisha ya Kiinjili; Mafundisho Jamii ya Kanisa; Utume wa familia na ufuasi wa Kristo; michezo, ujasiliamali na kujitegemea; Katekesi ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Maisha ya Sala, bila kusahamu michezo na huduma kwa watoto yatima na walemavu.

Askofu Ssemogerere anasema vijana leo hii wanakumbana na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu; kumong’onyoka kwa tunu bora za kimaadili; magonjwa yasiyokuwa na tiba wala kinga kama vile UKIMWI; ndoa za utotoni; ukosefu wa fursa za ajira na teknolojia ya kisasa; ukanimungu; uchumba sugu, ulevi wa kupindukia; matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na hali ya vijana kukata na kujikatia tamaa. Mama Kanisa anatambua na kuthamini umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana anataka kulalala sambamba na vijana katika safari ya maisha yao ya ujana akiwapatia imani, matumaini na mapendo.

Kwa upande wake, Emmanuel Odokonyero kutoka Uganda ameshirikisha jinsi ambavyo alitekwa nyara na kupelekwa mstari wa mbele kwenye Jeshi la Waasi wa Uganda. Huko alionja mateso na suluba katika  maisha yake na kwamba, baadhi ya rafiki zake waliuwawa kikatili na waasi. Lakini kwa bahati njema aliweza kutoroka na sasa anamshukuru Mungu aliyemwezesha kuvuka majaribu yote haya kwa imani na matumaini. Anaendelea kuwasikitikia wale ambao bado wametekwa nyara na waasi hao, wengi wao wakiwa ni Waseminari. Emmanuel Odokonyero anaendelea kusema kwamba, baada ya kurejea nyumbani aliendelea na shule na sasa amekwisha kupata shahada ya kwanza katika masuala ya biashara.

Bi Winnie Nansumba kutoka Uganda ameshuhudia jinsi alivyoambukizwa ugonjwa wa Ukimwi kwa vile alimpenda kijana ambaye baadaye alimwambukiza ugonjwa wa Ukimwi. Sasa anawaalika vijana wenzake kushikamana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa kuwa waaminifu kwa Mungu pamoja na kuendelea kuambata maadili mema. Vijana wawe tayari kuwasaidia waliokumbwa na Ukimwi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.